ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zina matumaini makubwa kwa Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA) katika kuimarisha na kueneza matumizi ya Kiswahili kikanda na kimataifa.
Ameyasema hayo katika maadhimisho ya miaka 10 ya Kamisheni hiyo yaliyofanyika Zanzibar, wakati akiwasilisha salamu za pongezi kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar,Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za kukuza lugha hiyo.
Amesema,maadhimisho hayo ni fursa ya kutathmini mafanikio tangu kuanzishwa kwa Kamisheni mwaka 2016, hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na kusisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuimarisha mabaraza ya Kiswahili.
Aidha, amepongeza uamuzi wa UNESCO kukitambua Kiswahili kama mojawapo ya lugha rasmi za kazi kuanzia Novemba 2025, akieleza kuwa ni hatua muhimu kwa hadhi ya lugha hiyo kimataifa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa KAKAMA, Dkt. Caroline Asiimwe, amesema Kamisheni itaendelea kupanua matumizi ya Kiswahili katika elimu, sayansi, teknolojia na majukwaa ya kidijitali kwa kushirikiana na nchi wanachama.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa kitaifa na kikanda, mawaziri, mabalozi na wadau wa lugha, huku msisitizo ukiwa ni utekelezaji madhubuti wa mikakati ya kuendeleza lugha ya Kiswahili.














