Watanzania wataendelea kumuenzi hayati Dkt.John Pombe Magufuli-Rais Dkt.Mwinyi

GEITA-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema,Watanzania wataendelea kumkumbuka na kumuenzi Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya Taifa na uongozi ulioacha alama ya kudumu.
Akizungumza Machi 17,2026 katika Kumbukizi ya Miaka Mitano ya Hayati Dkt. Magufuli yaliyofanyika Viwanja vya JS, Chato, Mkoa wa Geita, Rais Dkt. Mwinyi amesema njia bora ya kumuenzi ni kuendeleza misingi ya uwajibikaji, kuwajali wananchi hususan wanyonge, na kusimamia rasilimali za nchi kwa manufaa ya wote.
Ameeleza kuwa, Hayati Dkt. Magufuli alikuwa muumini wa dhati wa Muungano, huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza maono yake, na kusisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, aliyemwakilisha Rais Dkt. Samia, amesema Hayati Dkt. Magufuli ataendelea kukumbukwa kwa uchapakazi, kujituma na uthubutu katika maamuzi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amechangia shilingi milioni 100 kwa ujenzi wa Makumbusho ya Hayati Dkt. Magufuli, huku katika harambee ya ujenzi wa Kanisa la Parokia ya Mt. Yohana Muzeyi, michango mbalimbali ikikusanywa ikiwemo milioni 50 kutoka kwa Rais Dkt. Samia, milioni 30 kutoka kwa Rais Dkt. Mwinyi, na milioni 29 kutoka kwa Makamu wa Rais, Dkt. Nchimbi na kukusanya jumla ya shilingi milioni 474,000,000.
Rais Dkt. Mwinyi, akiwa na Mama Mariam Mwinyi, pia alishiriki kuweka shada la maua katika kaburi la Hayati Dkt. Magufuli pamoja na viongozi wengine.

Kumbukizi hiyo imehudhuriwa na viongozi wa Serikali zote mbili, viongozi wa dini, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here