WMA yadhamiria kukomesha rumbesa ili wakulima wanufaike zaidi

DODOMA-Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla amewataka watendaji wa Wakala hiyo kuanza ukaguzi wa mazao ya shamba na kupambana zaidi na ufungashaji wa mazao hayo kwa mtindo wa rumbesa.Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo (WMA) wakiimba wimbo wa ‘Mshikamano Daima’ baada ya kuhitimisha kikao cha 37 cha Baraza hilo kilichofanyika Machi 27, 2026 jijini Dodoma.

Akifungua Mkutano wa 37 wa Baraza la Wafanyakazi wa WMA, Machi 27, 2026 jijini Dodoma, Kihulla amewasisitiza wajumbe wa Baraza hilo kufikisha ujumbe huo kwa watumishi wote katika maeneo yao kuanza kutekeleza jukumu hilo kikamilifu.

“Lakini tunapotekeleza majukumu haya, tuhakikishe haki katika biashara na kulinda mapato ya Serikali,”ametahadharisha.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wakala wa Vipimo (WMA) wakiimba wimbo wa ‘Mshikamano Daima’ baada ya kuhitimisha kikao cha 37 cha Baraza hilo kilichofanyika Machi 27, 2026 jijini Dodoma.

Amesema kuwa, katika kipindi cha kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, WMA imepata mafanikio mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake ya kumlinda mlaji kupitia uhakiki wa vipimo lakini pia kumekuwepo na changamoto kadhaa.

Akidadavua, amesema mafanikio yaliyopatikana yametokana na juhudi, weledi na ushirikiano wa watumishi wote wa Wakala hivyo amewapongeza kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya.Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA), Alban Kihulla (katikati) akiongoza kikao cha 37 cha Baraza la Wafanyakazi wa Wakala hiyo kilichoketi Machi 27, 2026 jijini Dodoma. Kulia ni Katibu wa Baraza, Meckytidicy Ngonyani na kushoto ni Katibu Msaidizi, Fadhil Msane.

“Pamoja na mafanikio hayo, bado tunakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na ongezeko la wigo wa majukumu yetu katika kumlinda mtoa huduma pamoja na mpokea huduma,” ameeleza.

Mtendaji Mkuu Kihulla amebainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na jukumu la uhakiki wa vipimo vinavyotumika kupima muda wa maongezi pamoja na uhakiki wa mita za maji na vilevile lumbesa; suala ambalo liliungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Sekta ya Afya (TUGHE), Ngazi ya Taifa, Rugemalira Rutatina ambaye pia alishiriki mkutano huo, akisema yako malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi katika maeneo hayo hivyo yanapaswa kushughulikiwa.

Kihulla amesisitiza kuwa, hata viongozi wakuu wa Wizara akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga wameielekeza WMA kupambana na ufungashaji mazao ya shamba kwa mtindo wa rumbesa ili kuwalinda wakulima.
Katika hatua nyingine, Mtendaji Mkuu amewahimiza wafanyakazi wote wa WMA kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo akiwataka kutambua kuwa kazi wanayofanya ina mchango mkubwa katika kulinda haki za wananchi pamoja na kukuza biashara ya ushindani na haki, ikiwemo pia kuongeza mapato ya Serikali.

“Kwa hiyo, niwaombe sana mkawasisitize watumishi waliopo katika vituo vyenu kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi na kubwa zaidi kujiepusha na vitendo vya rushwa.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la WMA, Isaac Birahi aliushukuru Uongozi wa Wakala hiyo kwa kuendelea kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji kazi kwa watumishi na kuomba hali hiyo iendelee kwa viwango vya juu zaidi.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Sera na Mipango, Nelson Ruturagala, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 16, 2026 alisema kuwa Wakala imefanikiwa kutekeleza Mpango Kazi wake kwa wastani wa zaidi ya asilimia 91.62

Akidadavua, aliyataja maeneo ya utekelezaji yaliyochangia kufikia wastani huo kuwa ni katika usimamizi wa vipimo, ukaguzi, uhakiki wa bidhaa zilizofungashwa zinazoingia nchini pamoja na ada kutokana na utolewaji wa huduma.

Katika kikao hicho cha 37, wajumbe wa baraza walipata pia fursa ya kujadili Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here