MSD kuanzisha kampuni tanzu kuimarisha usambazaji wa bidhaa za afya

NA GODFREY NNKO

BOHARI ya Dawa (MSD) iko katika hatua za mwisho za kuandaa mpango wa kuanzisha kampuni tanzu itakayolenga kuongeza ufanisi katika usambazaji wa bidhaa za afya nchini.
Sambamba na kuimarisha ushindani wa taasisi hiyo sokoni, pamoja na kunufaika na fursa mbalimbali za kibiashara zinazojitokeza ndani na nje ya nchi.
Mfamasia kutoka Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini katika Bohari ya Dawa (MSD),Bi.Bwiro Magesa ameyasema hayo Aprili 24,2026 wakati akiwasilisha mada kuhusu mafanikio na mwelekeo wa taasisi hiyo wakati wa semina kati ya MSD na wahariri wa vyombo vya habari iliyofanyika katika Ofisi za MSD Kanda ya Kati, Kizota jijini Dodoma.

Amesema,hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya kimkakati yanayolenga kuifanya taasisi hiyo kuwa na mfumo endelevu na wenye tija katika sekta ya afya.
Kuanzishwa kwa kampuni hiyo licha ya kuongeza mapato MSD itasaidia magari yanayosafirisha bidhaa zake kwenda maeneo mbalimbali kutojiendesha kwa hasara, kwani yatakuwa yanarudi na bidhaa zinazohusu afya kutoka kwa wadau mbalimbali ambao watalipia.

Aidha, Bi.Magesa ameeleza kuwa,pamoja na mafanikio yaliyopatikana, bado MSD inakabiliwa na changamoto ya upungufu wa magari ya usambazaji, ambapo magari 96 yenye thamani ya shilingi bilioni 33.9 yanahitajika ili kuboresha mfumo wa ugavi wa bidhaa za afya nchini.

Mahitaji hayo yanajumuisha magari makubwa ya mizigo na trela kwa ajili ya kuongeza uwezo wa usafirishaji kutoka makao makuu kwenda kanda mbalimbali, pamoja na kati ya kanda na kanda.
Aidha, alibainisha kuwa mpango huo unahusisha pia ununuzi wa magari ya ubaridi na yaliyofunikwa (refrigerated na insulated trucks) ili kuimarisha usambazaji wa bidhaa zinazohitaji mnyororo maalum wa ubaridi, pamoja na magari ya ukubwa wa kati na mdogo kwa ajili ya kufikia maeneo ya mbali na yenye miundombinu duni.

Pia,amesema matumizi ya magari yenye crane maalum (truck-mounted crane) yatasaidia kuongeza usalama na ufanisi katika upakuaji wa mizigo mikubwa.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, MSD tayari imeanza utekelezaji wa awamu ya kwanza ya ununuzi wa magari 15 mapya ya usambazaji.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uwezo wa usafirishaji, kupunguza ucheleweshaji wa bidhaa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuboresha mtiririko wa ugavi kwa ujumla.

Ununuzi huo umezingatia mahitaji ya kanda, hali ya miundombinu ya barabara pamoja na viwango vya ubora na usalama, ili kuhakikisha matumizi ya gharama nafuu na ufanisi wa muda mrefu.

Kwa sasa, MSD inatekeleza majukumu yake kupitia kanda 10 nchini, ikitumia jumla ya magari 196.
Hata hivyo, sehemu kubwa ya magari hayo imeanza kuchakaa kutokana na matumizi ya muda mrefu, hali inayochangia kuongezeka kwa gharama za matengenezo na kupunguza ufanisi wa utoaji huduma.

Magari mengi amesema yalianza kutumika tangu mwaka 2011, hivyo kuna mpango wa kuyabadilisha kwa magari mapya yenye teknolojia ya kisasa, ikiwemo matumizi ya nishati mchanganyiko kama gesi na umeme.

Sambamba na jitihada hizo, MSD imeendelea kushirikiana na sekta binafsi pamoja na mashirika ya umma, ikiwemo Shirika la Reli Tanzania na Shirika la Posta, kwa lengo la kuboresha kasi, ufanisi na gharama za usambazaji.

Bi.Magesa amesema, ushirikiano huo umeongeza wigo wa mbinu za usafirishaji na kuhakikisha bidhaa za afya zinafika kwa wakati katika vituo vya huduma.

Katika hatua nyingine, Serikali kupitia MSD inatarajia kutekeleza mradi wa matumizi ya nishati jadidifu wa umeme wa jua unaojulikana kama Green Project, unaokadiriwa kugharimu shilingi bilioni 38.1.

Amesema,tayari shilingi bilioni 9.5 zimepokelewa kutoka Global Fund kwa ajili ya usimikaji wa mifumo ya nishati ya jua katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Dar es Salaam, huku mchakato wa manunuzi ukiendelea.

Mradi huo unatarajiwa kusaidia kuhifadhi bidhaa za afya kwa ufanisi zaidi, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuendana na sera ya Serikali ya kuhimiza matumizi ya nishati mbadala na utunzaji wa mazingira.
"MSD inaendelea kutafuta rasilimali fedha ili kukamilisha utekelezaji wa mradi huo."

Kwa mujibu wa takwimu za MSD, hadi kufikia Desemba 2025, uhakiki wa mali umefanyika katika kanda zote na kubaini kuwa bidhaa zote zipo sawa na kumbukumbu zilizopo katika mfumo wa ERP Epicor 10.

Aidha, thamani ya bidhaa za afya ghalani imeongezeka katika makundi yote, jambo linaloimarisha uhakika wa upatikanaji wa bidhaa hizo katika nyakati za kawaida na wakati wa dharura.

Kwa ujumla, hatua zinazochukuliwa na MSD zinaashiria dhamira ya Serikali ya kuimarisha sekta ya afya kupitia mfumo madhubuti wa ugavi, unaolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa wakati na kwa ufanisi.

"Kwa Bohari ya Dawa kuwa na bidhaa za thamani hii kunatoa uhakika wa usalama wa afya katika kipindi cha kawaida, na pale
ambapo majanga yakitokea."

MSD ni nini?

Bohari ya Dawa (MSD) ni taasisi ya Serikali iliyoanzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.13 ya Mwaka 1993 na marekebisho yake kama idara inayojitegemea chini ya Wizara ya Afya.
Wakati wa uanzishwaji wake, MSD ilipewa majukumu matatu ambayo ni; Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya umma nchini na vile vilivyoidhinishwa na Wizara yenye dhamana ya Afya.

Kufuatia kuibuka kwa Uviko-19 na lengo la kuweza kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea katika uzalishaji wa bidhaa za afya, Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya MSD Sheria Na.4 ya Mwaka 2021 na kuipa hadhi ya kuwa taasisi kamili inayojitegemea (autonomous entity), kuongeza jukumu la nne la Uzalishaji wa bidhaa za afya pamoja na kuipa MSD sharti la kujiendesha kibiashara.

Mwaka 2024, yalifanyika marekebisho mengine kupitia Sheria Na. 2 ya mwaka 2024 na kuipa MSD mamlaka ya kuwekeza kwa kuzingatia maelekezo ya Msajili wa Hazina au mamlaka husika.

Hivyo, MSD inatekeleza majukumu ya msingi manne ambayo ni Uzalishaji, Ununuzi, Utunzaji na Usambazaji wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo vya umma vya kutolea huduma za afya na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara yenye dhamana ya Afya.

MSD inajiendesha kwa mfumo wa uzungushaji wa fedha (revolving fund) ambapo utaratibu huu unazingatia gharama zote muhimu kuanzia ununuzi, utunzaji na usambazaji na hivyo kuhakikisha taasisi inakuwa endelevu.

Mfumo huu unaihitaji MSD iwe na mtaji wa kuwezesha kutekeleza majukumu yake ya uendeshaji wa mnyororo wa ugavi,kwa sababu MSD haipokei ruzuku yoyote kutoka serikalini
ikiwemo mishahara ya watumishi.

Katika kutekeleza majukumu yake, MSD inatumia kanda zake 10 zilizowekwa kimkakati ili kurahisisha upatikanaji wa bidhaa za afya. 

Kanda hizo ni Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Dodoma, Tabora, Iringa, Mtwara, Kagera na Tanga.
Hadi kufikia mwezi Desemba 2025, idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya vinavyohudumiwa na MSD ni 8,893 kutoka vituo 2500 wakati inaanzishwa mwaka 1994 sawa na ongezeko la zaidi ya vituo 6,393.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here