Waziri Mkuu akagua ujenzi wa barabara ya mchepuo ya Mji wa Iringa

■Asema mradi huo utafungua fursa mpya za uchumi na kupunguza msongamano wa magari mjini Iringa

■Aagiza wakandarasi kuwalipa kwa wakati wadaiwa wao

IRINGA-Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika miradi ya kimkakati ya miundombinu ili kuboresha usafiri, kuongeza ufanisi wa uchukuzi na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi nchini.
“Barabara hii ni muhimu kwa uchumi wa Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla. Itasaidia kupunguza msongamano wa magari, kuongeza biashara na kuchochea ukuaji wa mji wa Iringa,”amesema Dkt. Nchemba.

Amesema hayo leo Jumamosi, Mei 23, 2026 wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Mchepuo ya Mji wa Iringa (Iringa Municipal Bypass) yenye urefu wa kilomita 7.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Iringa.
Mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya SINOHYDRO Corporation Limited kwa usimamizi wa TANROADS kupitia kitengo chake cha TECU, unagharimu shilingi bilioni 41.6.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza miradi mikubwa ya barabara nchini kwa lengo la kuimarisha uchumi na kurahisisha huduma za usafiri na uchukuzi.

Amesema barabara hiyo itakuwa suluhisho la kudumu la msongamano wa magari katika mji wa Iringa hususan katika eneo la mlima wa Ipogoro ambalo limekuwa likikumbwa na ajali na changamoto za usafiri kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu, magari na vyombo vingine vya usafiri.

“Ndugu zangu wana Iringa, Mheshimiwa Rais amejipambanua kuwa ni Rais wa matokeo. Akisema jambo analitekeleza, na ndiyo maana mnaendelea kuona miradi mikubwa ya barabara ikitekelezwa karibu kila kona ya nchi,”amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Serikali kuhakikisha wanawalipa kwa wakati wakandarasi wadogo, mafundi na vibarua wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kadri wanavyopata fedha, wawalipe wale wanaotekeleza mradi pamoja nao. Sio vizuri mradi ukamilike wakati wengine waliotoa huduma wanadai malipo yao,”amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kujenga barabara za mchepuo katika miji mikubwa ili kupunguza msongamano wa magari na kuongeza ufanisi wa usafiri wa mizigo nchini.

Amesema Serikali pia inaendelea kutekeleza miradi mingine ya barabara za mchepuo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Dodoma, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Arusha na Tanga.
Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hosea Machaka amesema utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 38.5 huku kazi mbalimbali zikiendelea ikiwemo ulipuaji wa miamba, ujazaji wa kifusi, ujenzi wa makalavati pamoja na ujenzi wa njia za mchepuo.

Amesema wananchi 186 walioathiriwa na mradi huo wamelipwa fidia yote yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4.6, hatua iliyosaidia kuondoa changamoto za upatikanaji wa eneo la mradi.

Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo amesema wananchi wa Iringa wameupokea mradi huo kwa matumaini makubwa kutokana na mchango wake katika kuboresha usafiri na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika mji huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here