Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani akutana na Naibu Kamanda wa Jeshi la Mashariki mwa Libya

NA DIRAMAKINI

WAZIRI wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio amekutana na Naibu Kamanda wa Jeshi la Taifa la Libya (LNA), Saddam Haftar katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha juhudi za kuleta umoja wa kisiasa na amani nchini Libya.
Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaunga mkono serikali yenye makao yake Mashariki mwa Libya, ambayo imekuwa ikishindania madaraka na Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayotambulika kimataifa yenye makao yake mjini Tripoli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, viongozi hao walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kukuza umoja wa kitaifa na kufanikisha amani ya kudumu nchini Libya.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa,Rubio amepongeza juhudi zinazofanywa na viongozi wa Libya katika kutafuta suluhisho la tofauti za kisiasa zinazoigawa nchi hiyo, huku akisisitiza kuwa Marekani itaendelea kuwa mstari wa mbele katika juhudi za kidiplomasia za kusaidia kuundwa kwa serikali moja yenye uhalali wa kidemokrasia.

“Marekani itaendelea kuunga mkono juhudi za kuijenga Libya iliyoungana na kuweka mazingira yatakayowezesha kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia na kuundwa kwa serikali itakayowaongoza wananchi wote wa Libya,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Katika miezi ya karibuni, Marekani imeongeza juhudi zake za kutafuta suluhu ya mgogoro wa kisiasa wa Libya. Mwezi Aprili mwaka huu, Washington ilisaidia kufanikisha makubaliano kati ya serikali mbili zinazoshindania uongozi kuhusu matumizi ya fedha za umma, ikiwemo malipo ya mishahara ya watumishi wa serikali na uendeshaji wa Shirika la Taifa la Mafuta la Libya.

Aidha, Marekani imekuwa ikihamasisha ushirikiano wa kijeshi kati ya majeshi yanayounga mkono pande zote mbili za mgogoro. Mwaka uliopita, vikosi kutoka mashariki na magharibi mwa Libya vilishiriki mazoezi ya pamoja na Jeshi la Marekani katika mji wa Sirte.

Libya imeendelea kukumbwa na mgogoro wa kisiasa na kiusalama tangu mwaka 2011 baada ya kuanguka kwa utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi, kufuatia uasi ulioungwa mkono na Muungano wa Kujihami wa NATO.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2014, mivutano ya kisiasa ilisababisha kuibuka kwa serikali mbili zinazoshindania uhalali wa kuongoza nchi hiyo, huku upande wa mashariki ukiungwa mkono na Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Khalifa Haftar, ambaye amekuwa akidhibiti sehemu kubwa ya mashariki mwa Libya tangu mwaka 2016.

Mwaka 2019, jeshi hilo lilianzisha operesheni ya kuuteka mji mkuu wa Tripoli, lakini juhudi hizo zilizimwa na vikosi vinavyounga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano mwaka 2020, ingawa mgawanyiko wa kisiasa umeendelea kuwepo.

Katika siku za karibuni, Saddam Haftar, ambaye anatajwa kuwa mrithi wa baba yake katika uongozi wa LNA, amekuwa akifanya ziara za kidiplomasia na kukutana na viongozi mbalimbali duniani, akiwemo Waziri wa Ulinzi wa Misri na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron.

Wakati huo huo, utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump umeendelea kuimarisha juhudi za kidiplomasia nchini Libya kupitia mshauri wa Ikulu ya White House, Massad Boulos ambaye anaongoza mpango wa kuzikutanisha serikali mbili zinazoshindania madaraka.

Kwa mujibu wa Boulos, pande zote za mgogoro zinatarajiwa kualikwa mjini Washington, D.C., kusaini makubaliano ya mwisho endapo mazungumzo yanayoendelea yatafikia mwafaka, huku Marekani ikisisitiza kuwa itaendelea kuunga mkono wananchi wa Libya katika juhudi za kumaliza zaidi ya miaka 15 ya migogoro na mgawanyiko wa kisiasa.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here