NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Mawaziri ya Ngazi ya Juu ya Mageuzi ya Kiuchumi nchini Sudan Kusini imeamua kuondoa kikomo cha sasa cha kuweka na kutoa fedha kwa sarafu ya nchi hiyo, huku ikielekeza walipakodi kulipa kodi kwa fedha taslimu kupitia akaunti za Mamlaka ya Mapato ya Sudan Kusini (SSRA).
Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha dharura cha Kamati hiyo kilichofanyika Juba, kikihudhuriwa na Wakurugenzi Wakuu wa Benki za Biashara, uongozi wa Crawford Capital Pay, pamoja na maofisa kutoka Benki Kuu ya Sudan Kusini na Mamlaka ya Mapato ya Sudan Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, Waziri wa Utumishi wa Umma na Maendeleo ya Rasilimali Watu, Ezekiel Lol Gatkuoth ambaye ni Kaimu Katibu wa Kamati hiyo amesema,kikao kimeazimia kuondoa kikomo kilichokuwepo cha utoaji na uwekaji wa fedha kwa kutumia Pauni ya Sudan Kusini.
Amesema,hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za kukabiliana na changamoto ya kuongezeka kwa upungufu wa ukwasi katika Benki Kuu ya Sudan Kusini, hali ambayo imekuwa ikiathiri mzunguko wa fedha na shughuli za kiuchumi nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Julai 21,2026 na Idara ya Mawasiliano na Habari,Wizara ya Fedha na Mipango, Sudan Kusini imefafanua kuwa,kamati hiyo imewaelekeza walipakodi kulipa kodi zao kwa fedha taslimu kupitia akaunti za Mamlaka ya Mapato ya Sudan Kusini, kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa fedha na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Pamoja na uamuzi huo, Kamati imesisitiza kuwa mchakato wa matumizi ya teknolojia katika ulipaji wa kodi na mageuzi ya mfumo wa kidijitali utaendelea kutekelezwa chini ya mpango unaosimamiwa na Crawford Capital Pay.
Hatua hiyo inaashiria kuwa Serikali ya Sudan Kusini inalenga kutumia njia mseto katika ukusanyaji wa mapato, ambapo malipo ya fedha taslimu yataendelea kutumika sambamba na mifumo ya kidijitali katika kuimarisha ufanisi wa mfumo wa kodi.
Katika kikao hicho, Waziri Ezekiel pia amepewa jukumu la kuongoza kamati ndogo itakayoendelea kupitia na kutathmini mifumo ya utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa.
Kamati hiyo ndogo itashughulikia, miongoni mwa mambo mengine, mikakati ya kuongeza mtaji wa Benki Kuu ya Sudan Kusini, kuboresha mfumo wa benki nchini humo na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hatua hizo zinalenga kuhakikisha Serikali inapata mapato ya kutosha kwa wakati, ikiwa ni pamoja na kuwezesha ulipaji wa mishahara ya watumishi wa umma kwa wakati.
Kamati ya Mawaziri ya Ngazi ya Juu ya Mageuzi ya Kiuchumi imesema kuimarisha mfumo wa benki, kuongeza ukusanyaji wa mapato na kuendelea na mageuzi ya kidijitali ni hatua muhimu katika kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kujenga mfumo imara zaidi wa fedha nchini Sudan Kusini.



