DAR-Wizara ya Fedha imeibuka mshindi wa pili wa jumla katika kundi la Wizara zilizoshiriki Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), kufuatia utoaji wa huduma bora na elimu kwa wananchi.
Tuzo hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, na kupokelewa kwa niaba ya Wizara ya Fedha na Afisa Habari Mwandamizi, Bw. Ramadhan Kissimba, aliyemwakilisha Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Bw. Benny Mwaipaja.Ushindi huo umetokana na dhamira thabiti ya Wizara ya Fedha na Taasisi zake ya kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi, ubunifu katika utoaji wa elimu kuhusu sera na mageuzi ya sekta ya fedha, pamoja na ushirikiano madhubuti wa Viongozi na Watumishi wake katika kutekeleza majukumu kwa weledi, uwajibikaji na ufanisi.
Kwa ujumla, ushindi huo pia unaonyesha matokeo ya jitihada za Wizara ya Fedha, katika utoaji bora wa huduma kwa wananchi kupitia mawasiliano ya moja kwa moja, elimu ya kifedha na ushirikishwaji wa Taasisi zake katika kutoa suluhisho linalokidhi mahitaji ya wananchi.
Mafanikio hayo yanadhihirisha pia mchango wa Wizara katika kuendeleza ajenda ya Serikali ya kujenga uchumi shindani, jumuishi na unaowezeshwa na wananchi wenye uelewa wa fursa na huduma za kifedha zinazotolewa na Serikali.
Wananchi waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha walieleza kuridhishwa na huduma walizopata, wakibainisha kuwa wataalamu wa Wizara walitoa elimu kwa uwazi kuhusu huduma za kifedha, matumizi ya mifumo ya kidijitali, namna ya kujiunga na vyuo bora vilivyoko chini ya Wizara, mikopo ya riba nafuu, uwekezaji, takwimu za kiuchumi, deni la taifa, masoko ya mitaji na fursa mbalimbali zinazowezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi.
Kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, Wizara ya Fedha iliendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuwafikia wananchi moja kwa moja kwa kutoa elimu, kuongeza uelewa kuhusu sera na huduma za kifedha, pamoja na kuwawezesha kutumia fursa za kiuchumi zinazochangia maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Aidha, Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha mawasiliano kati ya Serikali na wananchi kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu sera, mipango na huduma zinazotolewa na taasisi za umma, hatua inayochochea uwajibikaji, uwazi na ushirikiano katika utekelezaji wa agenda ya maendeleo.
Katika Maonesho hayo ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Wizara ya Fedha ilitoa huduma kupitia Idara, Vitengo na Taasisi zilizo chini yake, zikiwemo Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Benki ya Maendeleo TIB, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Hazina SACCOS, Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA), Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).
Taasisi nyingine zilizoshiriki kutoa huduma ni Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA), Mfuko wa Dhamana na Uwekezaji Tanzania (UTT AMIS), Mfuko wa SELF, Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA), Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini (IRDP), Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Taasisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi (TOST), Mamlaka ya Rufaniy a Zabuni za Umma (PPAA), pamoja na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), ambazo kwa pamoja zilitoa elimu na huduma mbalimbali zilizowawezesha wananchi kupata uelewa mpana kuhusu fursa za kifedha na maendeleo ya uchumi.
Maonesho hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. J.K Nyerere, jijini Dar es Salaam, yamefungwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ally Mwinyi.







