DAR-Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, ametembelea na kujionea maendeleo na maboresho yaliyofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia, ambapo ilitoa mkopo nafuu wa dola za marekani milioni 345, kwa ajili ya awamu ya kwanza ya maboresho ya Bandari hiyo.
Katika ziara hiyo Dkt. Diop akiambatana na Mwenyeji wake Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, alipongeza hatua kubwa iliyofikiwa katika maboresho hayo ambayo yameongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha nafasi ya Bandari hiyo kama lango muhimu la biashara kwa Tanzania na nchi jirani zisizo na bahari (Landlocked Countries).Dkt. Diop alisema,mradi wa kuboresha Bandari kwa awamu ya kwanza umeleta mabadiliko makubwa katika ufanisi wa Bandari, jambo linalosaidia kurahisisha biashara na usafirishaji wa mizigo kwa Tanzania pamoja na nchi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kama lango la kuingiza na kusafirisha bidhaa zao.
“Benki ya Dunia inaendelea kuangalia uwezekano wa kushiriki katika awamu ya pili ya maboresho ya Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha miundombinu ya biashara na usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Dkt. Diop.
Kwa upande Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari, TPA, Bw. Plasduce Mbossa aliishukuru Benki ya Dunia kwa kuwekeza kiasi hicho cha fedha kilichochangia kuboresha utoaji wa huduma pamoja na kuongeza ufanisi na ushindani wa Mamlaka ya Bandari kwa ujumla kupitia msaada wa kiufundi na kifedha ambao utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 85.
Kupitia mradi huo, uwezo wa Bandari kuhudumia mizigo umeongezeka kutoka Tani milioni 14 mwaka 2015/16 kabla ya mradi huo kuanza hadi kufikia Tani Milioni 32.8 mwaka 2025/26 kiwango ambacho ni cha juu cha ufanisi, huku maboresho ya miundombinu na mifumo ya utoaji huduma yakilenga kupunguza muda wa meli kukaa bandarini, kuongeza kasi ya upakuaji na upakiaji wa mizigo na kuboresha mazingira ya biashara.
Uwekezaji huo haujanufaisha Tanzania pekee, bali una umuhimu mkubwa kwa nchi sita zinazopakana na Tanzania ikiwemo Jamhuri ya Kongo, Burundi, Rwanda, Uganda, Zambia na Malawi, ambazo zinategemea bandari za Tanzania kupitisha mizigo yao.
“Bandari ya Dar es Salaam ni muhimu si kwa Tanzania pekee, bali kwa nchi jirani zisizopakana na bahari ambazo zinategemea miundombinu yetu katika kusafirisha bidhaa zao na hivyo, maboresho haya yana maana pana zaidi katika kukuza biashara na uchumi wa ukanda."
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar alieleza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo katika kuimarisha miundombinu ya kimkakati, hususan ile inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji, kupanua biashara na kuunganisha Tanzania na masoko ya kikanda na kimataifa.
Ziara ya Dkt. Diop katika Bandari ya Dar es Salaam ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu nchini Tanzania iliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia katika maeneo mbalimbali ya maendeleo.
Awali alifanya mazungumzo na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) ambapo walijadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza Ushoroba wa Kati (Central Corridor) na kuubadilisha kutoka kuwa njia ya usafirishaji na kuwa ushoroba wa kiuchumi wenye uwezo wa kuchochea uzalishaji, biashara, uwekezaji na ajira.
Ushoroba wa Kati una umuhimu mkubwa kwa Tanzania na nchi jirani zinazotumia miundombinu ya Tanzania kusafirisha bidhaa kutoka na kwenda katika masoko ya Kimataifa.
Tags
Balozi Khamis Mussa Omary
Bandari ya Dar es Salaam
Benki ya Dunia (WB)
Benki ya Dunia Tanzania
Dr Ndiame Diop
Habari
Kimataifa
Wizara ya Fedha Tanzania







