DODOMA-Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limeendelea kutumia Maonesho ya Wakulima, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayoendelea Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela Nzuguni jijini Dodoma kuwa jukwaa la kutoa elimu na ushauri wa kitaalamu kwa wananchi kuhusu fursa za makazi, ununuzi na upangishaji wa nyumba pamoja na uwekezaji katika sekta ya nyumba.
Kupitia banda lake lililopo Barabara ya Maonesho, ndani ya Tenti la Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, NHC inawakutanisha wananchi na wataalamu wake ili kuwapa taarifa sahihi kuhusu huduma, miradi na fursa mbalimbali zinazotolewa na shirika.
Banda hilo limeendelea kuwa sehemu muhimu kwa wananchi wanaotaka kufahamu hatua za kumiliki nyumba, aina za nyumba zinazopatikana, taratibu za ununuzi na upangishaji pamoja na fursa za uwekezaji zinazotolewa na NHC.
Kwa mujibu wa maafisa wa NHC, upatikanaji wa taarifa sahihi na ushauri wa kitaalamu ni hatua muhimu katika kumsaidia mwananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu mahitaji yake ya makazi na uwekezaji.
Ushiriki wa NHC katika maonesho hayo pia unalenga kuwawezesha wananchi kupata majibu ya maswali mbalimbali ambayo wamekuwa nayo kuhusu namna ya kumiliki nyumba, fursa za uwekezaji na huduma zinazotolewa na shirika.
WANANCHI WAFUNGUKA
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la NHC wameeleza namna walivyopata ufafanuzi wa maswali yao baada ya kuzungumza na wataalamu wa shirika.
Grayson Matuma mkazi wa Dodoma amesema, awali alikuwa akiamini kuwa mchakato wa kupata nyumba za NHC ni mgumu, lakini amebadilisha mtazamo wake baada ya kutembelea banda hilo na kupata maelezo ya kina.
Amesema,wataalamu wa NHC wamemuelekeza hatua kwa hatua kuhusu namna nyumba za shirika zinavyopatikana, jambo lililomsaidia kuelewa mchakato huo kwa urahisi zaidi.
“Kwa muda mrefu nilikuwa nafikiri kupata nyumba ya NHC ni mchakato mgumu sana. Lakini baada ya kufika hapa bandani, nimeelekezwa vizuri hatua kwa hatua na sasa nimeelewa namna nyumba za NHC zinavyopatikana,” amesema Matuma.
Ameongeza kuwa,ameridhishwa na huduma aliyopata, akisema maelezo yaliyotolewa na wataalamu wa shirika yamemsaidia kuondokana na dhana aliyokuwa nayo awali kuhusu ugumu wa kupata nyumba za NHC.
Matuma pia amepongeza NHC kwa kujenga nyumba zenye viwango na kuahidi kuwa balozi wa kuhamasisha wananchi wengine kufahamu fursa zinazopatikana kupitia Shirika hilo.
NIMEPATA MAJIBU YA MASWALI YANGU
Kwa upande wake, Bi. Antonia mkazi wa Dodoma amesema, ziara yake katika banda la NHC imemsaidia kupata majibu ya maswali mbalimbali aliyokuwa nayo kuhusu namna ya kupata nyumba za shirika.
"Nimependa huduma zinazotolewa hapa. Nilikuwa na maswali mengi kuhusu namna ninavyoweza kupata nyumba za Shirika la Nyumba, lakini baada ya kufika kwenye banda la NHC nimeweza kujibiwa maswali yangu yote,” amesema.
Ushuhuda wa Antonia unaonesha umuhimu wa wananchi kutumia maonesho kama fursa ya kukutana moja kwa moja na wataalamu wa taasisi mbalimbali na kupata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi yanayohusu makazi au uwekezaji.
Aidha, wataalamu wa NHC wamewataka wananchi wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kutumia fursa hiyo kupata taarifa sahihi moja kwa moja kutoka kwao badala ya kutegemea taarifa zisizo rasmi kuhusu huduma na fursa za makazi.
Shirika limeeleza kuwa,hatua kubwa ya maisha inaweza kuanza na taarifa sahihi, swali moja au mazungumzo mafupi na mtaalamu.
Pia, banda la NHC halitumiki kama eneo la maonesho pekee, bali pia kama sehemu ya elimu, ushauri na kuwaunganisha wananchi na fursa zinazohusiana na sekta ya makazi na uwekezaji.
Wananchi wanaendelea kupata fursa ya kuuliza maswali kuhusu namna ya kuanza safari ya kumiliki nyumba, aina za nyumba zinazoweza kukidhi mahitaji yao na fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana kupitia NHC.
Shirika limewahimiza wananchi wanaohudhuria Maonesho ya Nanenane kutembelea banda lake, kusikiliza maelezo ya wataalamu na kufanya maamuzi baada ya kupata uelewa wa kutosha.
Kwa mujibu wa NHC, kupata taarifa sahihi kunaweza kumsaidia mwananchi kutambua fursa zinazomfaa na kupanga hatua zake kwa uelewa zaidi ili kupata huduma bora za makazi.






