Rais Dkt.Samia azindua nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amezindua nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hatua inayolenga kuweka msingi wa Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na shindani pamoja na jamii yenye uwezo,maarifa na ustawi.


Uzinduzi huo umefanyika leo Agosti 3, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, ukiambatana na mazungumzo maalum kati ya Serikali na sekta binafsi kuhusu namna ya kushirikiana katika kuhakikisha malengo yaliyowekwa kwenye dira hiyo yanafikiwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt.Samia amesema,Tanzania imeanza utekelezaji wa Dira 2050 ikiwa na msingi mzuri wa kiuchumi unaotoa mazingira bora ya kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa kwa kipindi cha miaka 25 ijayo.

Amesema, uchumi wa nchi umeendelea kuwa himilivu, mfumuko wa bei umedhibitiwa, uwekezaji umeongezeka na Tanzania imeendelea kujenga nafasi yake kama lango muhimu la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Ukanda wa Maziwa Makuu na Kusini mwa Afrika.
“Ni muhimu kutambua tumeanza utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 tukiwa na msingi mzuri wa kiuchumi. Uchumi wetu umeendelea kuwa himilivu, mfumuko wa bei unadhibitiwa, uwekezaji umeongezeka na Tanzania imeendelea kujenga nafasi yake kama lango la biashara,”amesema.

Kwa mujibu wa Rais Dkt.Samia,msingi huo unaipa Tanzania fursa ya kusonga mbele katika kujenga uchumi shindani, jumuishi na himilivu, unaolenga kuhakikisha manufaa ya maendeleo yanafika kwa wananchi wote.

Serikali,sekta binafsi kushirikiana

Rais Samia amesisitiza kuwa,mafanikio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 hayawezi kufikiwa na Serikali pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa karibu na sekta binafsi pamoja na wadau wengine wa maendeleo.

Amesema, sekta binafsi ina nafasi muhimu katika kuchochea uwekezaji, uzalishaji, ajira na ukuaji wa uchumi, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria na kitaasisi kwa ajili ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt.Samia pia ameshuhudia utiaji saini wa matamko ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi katika utekelezaji wa Dira 2050.

Miongoni mwa waliosaini matamko hayo ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Alexander Mkumbo, kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Dkt. Juma Malik Akil.

Rais Dkt.Mwinyi

Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi ni nguzo muhimu katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na kujenga Tanzania yenye uchumi shindani, jumuishi na unaojitegemea.

Dkt.Mwinyi amempongeza Rais Dkt.Samia kwa uongozi na msukumo anaoutoa katika utekelezaji wa dira hiyo, ambayo inaweka mwelekeo wa maendeleo ya Tanzania na ustawi wa wananchi kuelekea mwaka 2050.

Amesema,dira hiyo inatoa msisitizo katika kujenga uchumi unaozingatia tija, ubunifu, matumizi ya teknolojia na ushiriki mkubwa wa sekta binafsi.
Amehimiza kuongeza uwekezaji katika viwanda, biashara, utalii, uchumi wa buluu, kilimo cha kisasa, huduma za kifedha, uchumi wa kidijitali na maendeleo ya rasilimali watu.

Dkt.Mwinyi amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana kikamilifu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhakikisha maeneo ya kimkakati yanapewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Amani ni mtaji wa uwekezaji

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula amepongeza jitihada za Serikali katika kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi, akisema mazingira hayo ni msingi wa maendeleo na mtaji muhimu wa uwekezaji.

Ngalula amesema,amani na utulivu vimekuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje kuendelea kutafuta fursa mbalimbali nchini.

“Sekta binafsi tunakupongeza kwa kuendelea kulinda amani, umoja na utulivu wa nchi yetu. Amani ndio msingi wa maendeleo yote ya taifa letu na ndio mtaji mkubwa wa uwekezaji,” amesema.
Amepongeza uongozi wa Rais Dkt.Samia kwa mageuzi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, yakiwemo maboresho ya sera na sheria, mifumo ya utoaji huduma, uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati na kuimarika kwa mazungumzo kati ya Serikali na sekta binafsi.

Ngalula amesema,utekelezaji wa Dira 2050 unatarajiwa kuhitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, ambayo kwa mujibu wake inatarajiwa kushiriki kwa takribani asilimia 70 katika utekelezaji wa dira hiyo.

Amesema,sekta binafsi inapaswa kuwa mshirika wa kimkakati katika kujenga Tanzania yenye uchumi imara, jumuishi na shindani.

Aidha, amepongeza hatua za kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kwa muda mrefu, akitolea mfano wa biashara za Kariakoo kuendelea kufanya kazi kwa saa 24, akisema hatua hiyo imeongeza fursa kwa wafanyabiashara.
Pia amempongeza Rais Dkt.Samia kwa uamuzi wa kusamehe kodi kwa biashara zinazoanza kwa kipindi cha mwaka mmoja, akisema hatua hiyo inaweza kuongeza hamasa ya ujasiriamali na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi.

Rais Dkt.Samia akabidhiwa tuzo

Vilevile, wadau wa sekta binafsi wamempongeza Rais Dkt.Samia kwa jitihada na mageuzi yanayolenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

Kwa kutambua mchango huo, Chemba ya Taifa ya Biashara (TNCC) imemkabidhi Rais Dkt. Samia tuzo maalum kama ishara ya kuthamini uongozi wake katika kujenga mazingira rafiki, yenye utabirika na yanayovutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Kwa ujumla, uzinduzi wa nyenzo za utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 umeweka msisitizo mpya katika ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi kama msingi wa kuharakisha uwekezaji, kuongeza uzalishaji, kukuza ajira na kuboresha maisha ya wananchi.
Dira hiyo inatoa mwelekeo wa maendeleo kwa Tanzania katika kipindi cha miaka 25 ijayo, huku utekelezaji wake ukitarajiwa kuhitaji mipango madhubuti, uwajibikaji, uwekezaji mkubwa, ubunifu na ushiriki wa pamoja wa Serikali, sekta binafsi na wananchi ili malengo yaliyowekwa yawe matokeo halisi katika maisha ya Watanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here