CMAG ya Jumuiya ya Madola yamuenzi mume wa Rais Dkt.Samia, hayati Hafidh Ameir Hassan

NA DIRAMAKINI

KUNDI la Mawaziri la Jumuiya ya Madola la Hatua za Kisiasa (CMAG) limefanya kikao chake cha 74 katika kikao maalumu mjini New York, Marekani ambapo limeutambua ushirikiano wa Tanzania na Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo katika masuala mbalimbali ya kitaifa.
Kikao hicho kimefanyika Septemba 20,2026 pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) na kiliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Masuala ya Ulaya wa Malta,Chris Fearne.

Pia, kikao hicho kilihudhuriwa na Naibu Waziri Mkuu wa Samoa, Mulipola Anarosa Ale Molio'o pamoja na mawaziri na wawakilishi kutoka Antigua na Barbuda, Botswana, Canada, Grenada, Malaysia, Mauritius na Zambia.

Katika kikao hicho, CMAG ilitenga muda kuomboleza kifo cha Hafidh Ameir Hassan, aliyekuwa mume wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyefariki dunia Septemba 7,2026.

Kwa mujibu wa taarifa ya hitimisho ya kikao hicho, wajumbe wa CMAG walikaa kimya kwa dakika moja kwa heshima ya marehemu.

Aidha, CMAG ilisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuzingatia misingi ya kisiasa ya Jumuiya ya Madola kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Jumuiya hiyo (Commonwealth Charter).

Vilevile, katika kikao hicho, CMAG ilifanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CMAG ilitambua ushirikiano wa Tanzania na Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, pamoja na ushirikiano wa hivi karibuni na vyama vya siasa na hatua zinazochukuliwa kuelekea maridhiano Zanzibar.

CMAG imeeleza kuwa, hatua hizo ni msingi mzuri wa kuendeleza mchakato wa maendeleo na ushirikiano zaidi.

Katika hatua nyingine, CMAG imehimiza Serikali ya Tanzania kuendelea kushirikiana na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, huku ikikubaliana Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa ajenda rasmi za kundi hilo.

Kikao hicho pia kilijadili masuala yanayohusu Uganda baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Adonia Ayebare.

CMAG imekaribisha kuendelea na kuimarishwa kwa ushirikiano wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuhusu masuala ya Uganda, pamoja na kurejea kwa shughuli za vyombo vya Nation Media Group nchini humo.

Kundi hilo pia limeipongeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kwa juhudi zake endelevu katika kuimarisha mazungumzo yenye kujenga na kujenga mazingira ya kuaminiana miongoni mwa nchi wanachama.

Kikao kijacho cha kawaida cha CMAG kinatarajiwa kufanyika Novemba 2026 nchini Antigua na Barbuda, sambamba na Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola.

Katika mkutano huo, CMAG pia inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake ya kila baada ya miaka miwili kwa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here