NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema, inaendelea kubaini na kuchunguza mbinu mbalimbali zinazotumika kukwepa malipo sahihi ya kodi katika uingizaji na usajili wa magari nchini kwa udanganyifu wa taarifa za magari ikiwemo kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu aina, modeli, mwaka wa kutengenezwa na thamani ya magari.
Sambamba na matumizi yasiyo sahihi ya misamaha ya kodi, matumizi mabaya ya utaratibu wa uingizaji wa magari kwa muda (temporary importation) pamoja na udanganyifu unaohusisha namba za chassis/VIN na nyaraka za magari.
Hayo yamebainishwa leo Septemba 28,2026 kupitia taarifa iliyotolewa na Idara ya Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano ya TRA.Kwa mujibu wa taarifa hiyo,operesheni za ufuatiliaji wa ukwepaji kodi za magari zimeendelea kufanyika nchi nzima, ambapo Septemba 26, 2026, TRA ilifanya operesheni katika eneo la Palm Beach Casino jijini Dar es Salaam.
Katika operesheni hiyo, ilibaini gari aina ya Mercedes-Benz G-Wagon iliyokuwa imeegeshwa katika eneo la Palm Beach Casino bila namba za usajili.
Uchunguzi wa kitaalamu wa gari hilo uliwezesha kuthibitisha Vehicle Identification Number (VIN) WDB4632762X322756.
Uhakiki wa taarifa katika Mfumo wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) ulionesha kuwa, nyaraka zilizowasilishwa wakati wa taratibu za forodha zilionesha kuwa gari hilo lilikuwa Modeli: Mercedes-Benz G-Class G350 yenye mwaka wa kutengenezwa 2020.
Hata hivyo, uchunguzi wa kisayansi wa Forensic ulithibitisha kuwa Modeli halisi ya gari hiyo kuwa Mercedes-AMG G63 yenye mwaka wa kutengenezwa 2018 ambayo ina thamani kubwa kuliko iliyowasilishwa na mmiliki wa gari.
Utofauti wa taarifa hizo unaonesha uwepo wa udanganyifu uliopelekea kupungua kwa uthamini wa forodha na kiwango halisi cha kodi kinachopaswa kulipwa.
"TRA inapenda kuujulisha umma kuwa uchunguzi wa tukio hili na mengine yanayofanana na hili unaendelea.
"Aidha, uchunguzi wa tukio hilo pamoja na gari hilo lilosajiliwa kwa jina la OMARY FARAJI NYEMBO (Ommy Dimpoz) ambalo limekamatwa na TRA bado unaendelea na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi na sheria husika. Aidha, tunatambua na kuheshimu ushirikiano alioutoa."
TRA imefafanua kuwa, chini kifungu cha 157(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na kifungu cha 139(1) cha sheria ya Forodha (Management and Tarrif) sura ya 403, vinampa mamlaka afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania kuingia na kukagua sehemu yoyote wakati wa mchana au usiku.
Ni ambayo anaamini kuwepo kwa bidhaa iliyoingia nchini bila kufuata utaratibu wa forodha au nyaraka zinazohusiana na bidhaa iliyoingia nchini bila kufuata utaratibu wa forodha chini ya sheria ya usimamizi wa Forodha ya Afrika Mashariki na sheria ya Forodha (Management and Tarrif) sura ya 403.
Aidha, katika kufanya hivyo anaweza kuongozana na afisa mwingine au kuomba usaidizi wa ofisa wa polisi kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria hii kwa kutumia nguvu ya kawaida.
Sambamba na mamlaka hayo, sheria za Forodha zinampa Afisa uwezo wa kukagua, kuthibitisha taarifa au nyaraka na kuchukua hatua pale inapobainika kuwa kuna ukiukwaji wa taratibu za Forodha.
TRA inawakumbusha walipakodi kuwa mamlaka ya ukaguzi na uchunguzi hayaondoi haki zao.
"Mmiliki wa mali iliyokamatwa ana haki ya kupewa taarifa ya maandishi na sababu za kukamatwa kwa mali hiyo kwa mujibu Kifungu cha 162(1) cha sheria ya Forodha (Management and Tarrif) sura 403.
"Kwa upande mwingine, mlipakodi ana wajibu wa kutoa taarifa sahihi, kamili na za kweli, kuwasilisha nyaraka halali, kujibu maswali yanayohusiana na mali au muamala unaochunguzwa na kushirikiana na Maafisa wa TRA wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwa mujibu wa kifungu cha 139(2) (d) cha sheria ya Forodha (Management and Tarrif) sura 403."
Aidha, Kifungu cha 21(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi sura 438 kina mtaka mtu yeyote aliyekuwa ameajiriwa au aliyepewa majukumu ya kuisaidia Mamlaka ya Mapato Tanzania kutunza kwa USIRI taarifa na nyaraka ambazo amewahi kuwa nazo au kuzijua wakati wa kutekeleza matakwa ya ajira yake au majukumu aliyopewa zinazohusiana na aina yoyote ya kodi ikiwemo ukaguzi huu wa magari.
Vilevile, kifungu cha 21(2), 21(3) na 21(5) cha Sheria ya Utawala wa Kodi, Sura 438, vinaruhusu kutolewa kwa taarifa za mlipakodi kwa majukumu maalumu na watu maalumu wakiwemo walioruhusiwa na mlipakodi husika baada ya kuidhinishwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka.
Wakati huo huo, TRA imetoa wito kwa wamiliki wa magari, wafanyabiashara, waagizaji wa magari na walipakodi wote kuhakikisha kuwa taarifa zinazowasilishwa wakati wa uingizaji wa magari ikiwemo modeli, mwaka wa kutengenezwa, thamani, VIN/chassis na utaratibu wa uingizaji ni sahihi na zinaambatana na nyaraka halali.
Aidha, TRA inapenda kuwakumbusha wananchi wote kuwa wanapotaka kununua gari kutoka kwa mtu mwingine, wanashauriwa kuhakiki taarifa za gari hilo kwenye mifumo na ofisi za TRA zilizopo nchi nzima kabla ya kununua ili kujiridhisha kama kodi zote stahiki zililipwa wakati wa uingizaji gari hilo nchini na hakuna changamoto nyingine zikiwemo za udanganyifu wa taarifa kuhusu gari husika.
"TRA inawakumbusha umma kuwa, kwa mujibu wa Kifungu cha 96(1) cha Sheria ya Usimamizi wa Kodi, ni kosa la jinai kwa mtu yeyote asiyehusika kuzuia usimamizi au utekelezaji wa sheria ya kodi."
Aidha, kwa mujibu wa Kifungu cha 96(3), vitendo vya kuzuia usimamizi wa sheria ya kodi vinajumuisha, pamoja na mambo mengine, kumshambulia, kumzuia au kujaribu kumshambulia Afisa anapokuwa akitekeleza kazi yake chini ya sheria ya kodi; kumzuia au kujaribu kumzuia Afisa huyo katika utekelezaji wa majukumu yake; kurekodi video au kuchukua picha kwa nia ovu ya kumuogopesha asitekeleze majukumu yake; au kuingilia kitu chochote kinachotumiwa na Afisa huyo katika kutekeleza majukumu yake.
"TRA inawahakikishia wananchi kuwa hatua hizi zinalenga kuhakikisha usawa katika ulipaji wa kodi, kulinda mapato ya Serikali na kujenga mazingira ya biashara yenye uwazi, uadilifu na ushindani wa haki. Pia itaendelea kutoa Elimu ya Kodi ili kurahisisha uwajibikaji wa kodi."
TRA imewahakikishia wananchi kuwa hatua hizi zinalenga kuhakikisha usawa katika ulipaji wa kodi, kulinda mapato ya Serikali na kujenga mazingira ya biashara yenye uwazi, uadilifu na ushindani wa haki.
Pia, itaendelea kutoa elimu ya kodi ili kurahisisha uwajibikaji wa kodi, na kuwahakikishia walipakodi na wananchi wote kuwa TRA pamoja na WATUMISHI WAKE WOTE wataendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi na kanuni za utumishi wa umma ambazo ni, WELEDI, UWAJIBIKAJI na UADILIFU huku ikiendelea kutoa HUDUMA BORA kwa HESHIMA, HAKI na USAWA bila kujali hadhi ya mtu, kama walivyoonesha watumishi katika tukio hilo.
"Pamoja Tunajenga Taifa Letu"