MOROGORO-Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb) ameiagiza Menejimenti ya Hazina Saccos kuhakikisha fedha za wanachama zinalindwa kwa kiwango cha juu, huku akiwataka kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji, ukaguzi wa ndani na udhibiti wa mikopo pamoja na urejeshaji wake.
Mheshimiwa Munde ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 13 wa Hazina Saccos Ltd uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Hoteli ya Morena mjini Morogoro.
Amesema kuwa, ili chama kiwe imara ni muhimu kiwe na mfumo mzuri wa ukaguzi wa ndani ambao utajumuisha usimamizi wa vihatarishi na kuendelea kuimarisha usalama wa mifumo na usiri wa taarifa za wanachama, sambamba na kutoa elimu kuhusu matumizi salama ya huduma hizo.
‘’Ninawaelekeza viongozi na Menejimenti ya Hazina SACCOS kuhakikisha kuwa, fedha za wanachama zinalindwa kwa kiwango cha juu. Kila muamala lazima uwe na nyaraka stahiki, uthibitisho na ufuatiliaji unaostahili,"amesema Mheshimiwa Munde.
Mhe. Munde ameongeza kuwa, ili kufikia mafanikio Hazina Saccos inatakiwa kuongeza juhudi za kuwafikia vijana, wanawake na makundi mengine ambayo bado hayajatumia kikamilifu huduma za kifedha ili makundi hayo yaweze kujikwamua kiuchumi.
Aidha, Mhe. Munde amesema kuwa,Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na vyama vya ushirika na Saccos katika kukuza uchumi wa wananchi.
‘’Serikali inatambua kuwa Vyama vya Ushirika na SACCOS vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa wananchi. Kupitia SACCOS wananchi wanaweza kuweka akiba, kupata mikopo kwa masharti nafuu, kukuza biashara na kuimarisha ustawi wa familia,’’ ameongeza Mhe. Munde.
Pia, Mhe. Munde ametumia mkutano huo kuwataka wanachama wa Hazina Saccos kutimiza wajibu wao kwa kuweka akiba kwa utaratibu na kurejesha mikopo kwa wakati na kuwasisitiza kuwa SACCOS haiwezi kukua ikiwa Wanachama hawataweka akiba na kutimiza masharti ya mikopo.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo Afisa Mtendaji Mkuu wa Hazina Saccos, Dkt. Festo Mwaipaja amesema,mkutano mkuu wa 13 unatoa fursa ya kutathmini chama kilipotoka, kilipo na kinapotaka kwenda, hivyo mkutano huo utatumika kujadili taarifa mbalimbali za chama.
Dkt.Mwaipaja amewataka wanachama kushiriki kikamilifu na kutoa maoni kwa uwazi, nidhamu na heshima na kuwahakikishia wanachama kuwa kila hoja itazingatiwa kwa maslahi mapana ya Hazina Saccos na wanachama wake.‘’Mkutano huu wa 13 unatupa fursa ya kutathmini tulikotoka, tulipo na tunakotaka kwenda. Tutapokea na kujadili taarifa mbalimbali, kupitia hali ya kifedha ya Chama, kutathmini utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita na kuweka vipaumbele vya kipindi kijacho,’’amesema Dkt. Mwaipaja.
Dkt.Mwaipaja ameongeza kuwa,chama kimeendelea kuimarisha utamaduni wa kuweka akiba, kutoa huduma za mikopo, kusimamia marejesho, kulinda mali zake na kuboresha mifumo ya ndani hatua ambazo zimeendelea kuifanya Hazina Saccos kuwa miongoni mwa Taasisi ya Kifedha imara, inayotegemewa na inayoweka maslahi ya wanachama mbele.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Bodi wa Hazina Saccos, Bi.Neema Mwakitalima amesema kuwa, Hazina Saccos imeendelea kukua kwa kasi na kutoa huduma za kifedha kwa wanachama zaidi ya elfu kumi na moja kutoka mafungu (Vote) 432 serikalini.
Bi. Mwakitalima ameongeza kuwa,katika kipindi cha Januari hadi Agosti 2026, jumla ya wanachama 1,367 walijiunga na chama, na kufanya idadi ya wanachama kufikia 11,507 kutoka wanachama 10,326 mwishoni mwa mwaka 2025.
Aidha, Bi.Mwakitalima amesema katika kipindi hicho mali za chama zimeongezeka na kufikia zaidi ya shilingi bilioni 63, wakati akiba na amana za wanachama zimefikia zaidi ya shilingi bilioni 50.
Mkutano Mkuu wa 13 wa Hazina Saccos umewakutanisha wawakilishi wa wananchama kutoka mafungu 432 na unafanyika ili kutoa fursa kwa wanachama kusimamia mwelekeo wa chama na wanachama kupokea taarifa ya utendaji, kutathmini maendeleo, kujadili changamoto na kufanya maamuzi yatakayoongoza mustakabali wa chama.







