DAR-Leo Bohari ya Dawa (MSD) imefanikiwa kuingiza shehena ya kwanza ya dawa ya tiba ya uraibu wa pombe iitwayo Naltrexone. Hatua hii ni matokeo ya ushirikiano wa kimkakati kati ya MSD na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe katika kuimarisha matibabu ya uraibu wa pombe nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Bohari ya Dawa (MSD),Bi.Etty Kusiluka imeeleza kuwa, hatua hii pia ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa makubaliano ya uimarishaji huduma kati ya MSD na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili-Mirembe kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za udhibiti wa uraibu wa pombe.Dawa ya Naltrexone itapatikana na kuratibiwa na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe huku ikiwa ni bidhaa itakayo endelea kununuliwa na MSD kwa ajili ya taasisi hiyo.
Mapema mwezi huu, wakati wa mafunzo kuhusu matumizi ya dawa ya Naltrexone, yaliyoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Afya ya Akili, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe aliwaagiza MSD kuharakisha upatikanaji wa vidonge hivyo.
MSD imepokea na kuingiza shehena hii nchini ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha huduma za afya ya akili na tiba ya uraibu pombe.
Mafanikio haya yanaonesha juhudi za Serikali kupitia MSD na wadau wa sekta ya afya kuhakikisha bidhaa muhimu za afya na za kimkakati zinapatikana nchini kwa wakati.







