Pepe Minambo agusia mambo muhimu kuelekea C-CEOs Forum 2026, asema hakuna kutegeana utekelezaji Dira 2050

NA GODFREY NNKO 

WAKATI Tanzania ikijielekeza katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, umuhimu wa kubadili mifumo ya uongozi, utamaduni wa utendaji kazi na kuongeza tija katika mashirika ya umma umeibuka kuwa miongoni mwa maeneo muhimu yatakayoamua mafanikio ya safari hiyo.
Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw.Alex Malanga (kushoto) akiongoza Podcast hiyo.
Msisitizo huo umetolewa wakati viongozi wakuu wa mashirika ya umma na wadau wengine wakikutana jijini Arusha kuanzia Septemba 28 hadi 30 katika Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026 chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Mkutano unaolenga kujadili namna taasisi hizo zinavyoweza kuendana na malengo ya kitaifa ya kukuza uchumi na kuongeza ushindani wa Tanzania.

Dira 2050 inaweka matarajio makubwa ya kuibadilisha Tanzania kuwa taifa lenye uchumi shindani, jumuishi na unaostahimili misukosuko ya ndani na nje, huku lengo likiwa ni kukuza uchumi wa nchi kutoka takribani Dola bilioni 100 hadi Dola trilioni moja katika kipindi cha miaka 24 ijayo.

Aidha, kutokana na ukubwa wa lengo hilo, wataalamu wanaeleza kuwa, mifumo ya kawaida ya uendeshaji wa taasisi haitoshi, bali yanahitajika mabadiliko makubwa katika utamaduni wa taasisi, uwezo wa kutekeleza mikakati, uwajibikaji na ubora wa uongozi.

Mtaalamu wa Kimataifa wa Mikakati ya Biashara, Bw.Pepe Minambo akizungumza kupitia Podcast ya Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kuelekea mkutano huo amesema, kufikia uchumi wa Dola trilioni moja yanahitajika mabadiliko ya msingi katika namna taasisi zinavyojiendesha, viongozi wanavyowajibika na watumishi wanavyotekeleza majukumu yao.

Pia, katika mjadala huo ulioongozwa na Afisa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bw.Alex Malanga, imeelezwa kuwa, Tanzania haianzi safari hiyo bila mifano ya kujifunza kutoka mataifa mengine duniani ambayo tayari yamefanikiwa kujenga uchumi wenye thamani ya Dola trilioni moja au zaidi.

Vilevile, mjadala huo umegusia kuwa, mataifa 20 duniani yana uchumi unaofikia kiwango hicho, hivyo uzoefu wa mataifa hayo unaweza kutoa mafunzo muhimu kuhusu mabadiliko ya kimuundo,usimamizi wa taasisi, tija na utekelezaji wa sera za maendeleo.

Hata hivyo,imesisitizwa kuwa kufikia ukuaji wa uchumi mara 10 hakutategemea takwimu za ukuaji wa uchumi pekee. Badala yake, mafanikio yatategemea pia uwezo wa taasisi kutafsiri mipango ya kitaifa kuwa vitendo, kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuweka mifumo madhubuti ya uwajibikaji.

Moja ya hoja kuu iliyosisitizwa ni umuhimu wa kubadili utamaduni wa taasisi, hususan katika mashirika na taasisi za umma.

Bw.Minambo amenukuu kauli maarufu ya mtaalamu wa usimamizi wa taasisi, Bw.Peter Drucker inayosisitiza kuwa, “utamaduni hula mkakati wakati wa kifungua kinywa”, akieleza kuwa hata mkakati bora unaweza kushindwa iwapo hautaungwa mkono na utamaduni unaohimiza uwajibikaji,ubunifu, nidhamu na utekelezaji.

Pia, Dira 2050 inaweza kuchukuliwa kama ramani ya safari ya taifa, lakini utamaduni wa taasisi ndio unaotoa nguvu ya kuitekeleza.

Hivyo, mashirika ya umma yanapaswa kujenga mazingira ya kazi yanayowahamasisha watendaji kuwa wabunifu, kuwajibika kwa matokeo na kuelewa namna majukumu yao ya kila siku yanavyochangia katika kufikia malengo mapana ya taifa.

Mjadala huo pia umeweka mkazo katika nafasi ya uongozi katika kuleta mabadiliko ya taasisi.

Kauli nyingine iliyotumika ni kwamba “kila kitu huinuka au kuanguka kutokana na uongozi”, ikisisitiza kuwa uwezo wa taasisi kukua na kufikia malengo yake unahusiana kwa kiasi kikubwa na ubora wa uongozi unaoisimamia.

Ndiyo maana, viongozi wa mashirika ya umma wanapaswa kuimarisha viwango vya utawala bora, uadilifu wa taasisi, uwajibikaji na uwezo wa kutazama mbele katika kupanga na kutekeleza mikakati.

Uongozi unaozingatia matokeo pia unatajwa kuwa muhimu katika kuhakikisha kuwa mipango haibaki kwenye nyaraka za kimkakati, bali inatekelezwa kwa kuweka malengo yanayopimika, muda wa utekelezaji na mifumo ya kufuatilia matokeo.

Katika eneo la mapato, mashirika ya umma na taasisi zilizo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) kwa sasa zinatajwa kuchangia takribani asilimia 3 hadi 4 ya mapato yote yasiyo ya kodi, huku malengo mapana yakilenga kuongeza mchango huo hadi kufikia takribani asilimia 10.

Ili kufikia lengo hilo, inahitajika kukabiliana na changamoto za kiutendaji zinazoweza kupunguza ufanisi na tija ya taasisi.

Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni kuhuisha na kuboresha michakato ya kiutendaji, kwa kuondoa taratibu zinazojirudia, kupunguza urasimu usio wa lazima na kutumia rasilimali watu kwa ufanisi zaidi.

Aidha, taasisi zinapaswa kuelekeza nguvu zaidi katika utekelezaji wa mipango badala ya kuishia katika uandaaji wa mikakati na mipango mizuri isiyotekelezwa kikamilifu.

Mjadala huo umeeleza kuwa, moja ya changamoto kubwa katika maendeleo ya Afrika si ukosefu wa dira, sera au mipango, bali ni pengo kati ya mipango na utekelezaji wake.

Aidha,mafanikio ya Dira 2050 yatategemea uwezo wa taasisi kuweka mifumo madhubuti ya kuhakikisha kuwa mipango inatekelezwa kwa wakati, rasilimali zinatumika ipasavyo na viongozi pamoja na watendaji wanawajibika kwa matokeo wanayopata.

Hatua hiyo inahitaji pia kuwepo kwa mifumo ya kupima utendaji, tathmini za mara kwa mara na uwazi katika kufuatilia utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.
Kujenga nguvu kazi yenye dhamira ya kitaifa

Katika kuhakikisha Dira 2050 inatekelezwa kwa ufanisi, pia kuna umuhimu wa kujenga nguvu kazi inayotambua uhusiano kati ya majukumu yake ya kila siku na malengo ya maendeleo ya taifa.

Vilevile, kila mtumishi katika taasisi ya umma anapaswa kuelewa namna kazi yake inavyochangia katika kuongeza tija, kuboresha huduma kwa wananchi, kuongeza mapato na kuimarisha ushindani wa Tanzania.

Hii inahitaji taasisi kuweka utamaduni wa kazi unaozingatia matokeo, ubunifu, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali.

C-CEOs Forum 2026 itawakutanisha zaidi ya wajumbe 700, wakiwemo wenyeviti wa bodi, maofisa watendaji wakuu wa mashirika, viongozi wa sekta binafsi na maofisa wa Serikali.

Mkutano huo unalenga kujenga uelewa na mwelekeo wa pamoja miongoni mwa viongozi wa taasisi katika kuoanisha mikakati ya mashirika yao na ajenda pana ya maendeleo ya taifa.

Hata hivyo,utekelezaji wa Dira 2050 utahitaji ushirikiano wa Serikali, mashirika ya umma, sekta binafsi na wananchi, huku kila taasisi ikitakiwa kutambua nafasi yake katika kujenga Tanzania yenye uchumi shindani, jumuishi na unaostahimili changamoto za dunia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here