RC Chalamila atangaza mkakati mpya wa usafi, miundombinu na biashara Dar

NA GODFREY NNKO

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila ametangaza mwelekeo mpya wa kuifanya Dar es Salaam kuwa jiji la kisasa na lenye hadhi ya kimataifa, akieleza kuwa hatua hiyo itajikita katika usimamizi wa taka, utunzaji wa mazingira, uboreshaji wa miundombinu na kuweka mpangilio rasmi wa shughuli za biashara.
RC Chalamila ameyasema hayo leo Septemba 17,2026 jijini Dar es Salaam katika mkutano na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ulioandaliwa kupitia ofisi hiyo na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Mkutano huo pia, umewaleta pamoja viongozi wa mkoa na taasisi zinazohusika na usimamizi wa mazingira ambapo ameweka bayana hatua mbalimbali ambazo mkoa unakusudia kuzichukua katika kukabiliana na changamoto za usafi wa mazingira, biashara zisizo rasmi pembezoni mwa barabara na matumizi yasiyopangiliwa ya maeneo ya umma.

Amesema,kasi ya ukuaji wa Dar es Salaam inalazimisha mabadiliko katika fikra, mifumo na namna ya kusimamia jiji hilo, akisisitiza kuwa maeneo muhimu yatapewa kipaumbele, ambayo ni usafi wa mazingira, uboreshaji wa miundombinu na mpangilio rasmi wa biashara.

RC Chalamila amesema, Serikali ya Mkoa inalenga kubadilisha mtazamo kuhusu taka kutoka kuwa mzigo unaotakiwa kuondolewa na kutupwa, na badala yake kuzitambua kama rasilimali na malighafi inayoweza kutumika katika shughuli za uzalishaji viwandani.

Amesema, mwelekeo wa muda mrefu ni kujenga mfumo ambao wananchi hawatakuwa walipaji pekee wa huduma za ukusanyaji taka, bali wanaweza kunufaika kiuchumi kwa kutenganisha taka na kuziwasilisha katika mfumo rasmi wa ukusanyaji na urejelezaji.

“Taka ni rasilimali na malighafi ya viwanda,” amesema RC Chalamila, akieleza kuwa mfumo huo utahitaji ushiriki wa wananchi, taasisi na wafanyabiashara.

Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa Mkoa, mpango huo utahusisha uwekezaji na uwepo wa vyombo maalumu vya taka katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye nyumba, vyombo vya usafiri wa umma na binafsi, stendi, shule, hospitali, nyumba za ibada na mitaa.

Vyombo hivyo vitatengwa kulingana na aina ya taka ili kurahisisha ukusanyaji, uchakataji na urejelezaji.

Amesema,timu za wataalamu na viongozi tayari zimetembelea baadhi ya nchi zilizopiga hatua katika usimamizi wa taka zikiwemo Korea Kusini, Uholanzi, India na China, kwa lengo la kujifunza mifumo na teknolojia inayoweza kutumika katika mazingira ya Dar es Salaam.

Wakati huo huo, RC Chalamila ametoa maagizo kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha maeneo ya kijani yaliyopo kando ya Barabara ya Nyerere yanatunzwa ipasavyo.
Amesema, barabara hiyo ni sehemu muhimu ya sura ya Dar es Salaam kwa kuwa inawaunganisha wasafiri na wageni wanaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Ametaka maeneo ya nyasi, miti na bustani kuanzia Terminal One hadi Terminal Two ya uwanja huo yaendelee kuwa katika hali nzuri wakati wote.

RC Chalamila pia ametangaza hatua za kudhibiti biashara zinazofanyika kiholela kando ya barabara kuu pamoja na maegesho yasiyoruhusiwa ya malori.

Amesema,hatua hizo hazilengi kuwazuia wananchi kujitafutia kipato, bali kuweka utaratibu unaolinda matumizi sahihi ya miundombinu na maeneo ya umma.

Amesema,biashara kama upikaji wa chakula barabarani na shughuli nyingine zinazofanyika katika maeneo yasiyotengwa rasmi zitatakiwa kuondolewa.

Kwa wafanyabiashara wadogo (wamachinga), RC Chalamila amesema,Serikali itaanza kampeni ya elimu kwa umma ya wiki mbili ambapo Wakuu wa Wilaya watakuwa mstari wa mbele kuongoza kampeni hiyo kwa lengo la kuwahamasisha wafanyabiashara kuhamia na kutumia maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya biashara.
"Lengo letu si kumfukuza mtu au kuzuia yeyote asitafute riziki, bali ni kuweka nidhamu na utaratibu utakaowezesha kila mjasiriamali kukua."

RC Chalamila pia amesema,kutakuwa na mtazamo mpya kuhusu wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao ndani ya maeneo rasmi ya Soko la Kariakoo.

Amesema,mfanyabiashara aliyeingia au kupanga duka au eneo rasmi la biashara katika Soko la Kariakoo hatatambulika tena kama “
machinga, bali atachukuliwa kama mfanyabiashara rasmi.

Hatua hiyo, amesema inalenga kutenganisha dhana ya biashara ndogo inayofanyika katika maeneo yasiyopangwa na biashara inayofanyika ndani ya maeneo rasmi.

Vilevile, katika kuongeza nafasi za wafanyabiashara, RC Chalamila amesema, Serikali inaendelea kutumia mfumo wa Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika kuendeleza majengo ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Amesema, uwekezaji huo utasaidia kujenga majengo ya kisasa yatakayotoa nafasi zaidi za biashara na kupunguza msongamano wa shughuli za kibiashara katika maeneo yasiyopangwa.

Aidha, amesema mkoa utashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuoanisha mifumo ya utambuzi wa wafanyabiashara kwa kuzingatia ukubwa wa miamala yao.

Lengo ni kuweka utambulisho unaotofautisha mjasiriamali mdogo, mfanyabiashara wa kati na mfanyabiashara mkubwa.

Usafi ni wajibu wa kila mwananchi

Kwa upande wake, Meneja wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Mashariki Kusini, Bi.Glory Kombe amesema,suala la usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mwananchi na linapaswa kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo.

Bi.Kombe aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa NEMC katika mkutano huo wa RC Chalamila na wahariri amesema, kanda hiyo inasimamia maeneo ya Ilala, Temeke, Ubungo na Kigamboni.

Amesema,Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, pamoja na marekebisho yake, inaweka msingi wa haki ya kuishi katika mazingira bora, safi na salama huku pia ikiweka wajibu kwa kila mtu kushiriki katika kulinda mazingira.

“Kila mmoja wetu ana wajibu wa kufanya ili kuhakikisha mazingira yetu yanakuwa safi, bora na salama,”amesema.

Amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuitisha kikao hicho, akisema ushirikiano wa viongozi, taasisi, vyombo vya habari na wananchi ni muhimu katika kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa jiji safi, salama na endelevu.

Usafi usiwe kampeni ya msimu

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile amesema, changamoto za mazingira na usafi wa Dar es Salaam zinahitaji mfumo endelevu badala ya hatua zinazochukuliwa wakati wa majanga au changamoto maalumu.



Bw.Balile amesema,mabadiliko ya tabianchi na matukio ya hali mbaya ya hewa yanaendelea kuonesha umuhimu wa miji kuwa na mifumo imara ya kukabiliana na athari za mazingira.

AmesemaDar es Salaam inapaswa kujenga utaratibu ambao usafi unakuwa sehemu ya maisha ya kila siku badala ya kuwa kampeni inayofanyika baada ya kutokea changamoto.

“Je, hatuwezi kuweka utaratibu, miundombinu na mfumo utakaowezesha Dar es Salaam kuwa safi kila siku na usafi utakaokuwa utamaduni badala ya kuwa kampeni," amehoji.

Bw.Balile pia amezungumzia tabia ya baadhi ya wananchi kutupa taka katika maeneo ya umma, akitoa mfano wa mtu aliyedai kumwona akitupa chupa ya maji katika barabara ya mwendokasi.

Amesema, changamoto hiyo inaonesha umuhimu wa kuweka mifumo ya uwajibikaji na utekelezaji wa sheria ili watu watambue gharama za kutupa taka kiholela.

Pia, Bw.Balile amependekeza kuwepo kwa mashindano ya usafi katika halmashauri za Dar es Salaam kuanzia ngazi ya kata hadi jiji, ambapo maeneo yatakayofanya vizuri yaweze kutambuliwa na kupewa hamasa.

Pia amependekeza kuimarishwa kwa mfumo wa faini za papo kwa papo kwa watu wanaokiuka kanuni za usafi, akitolea mfano wa utaratibu unaodaiwa kutumika Moshi ambapo mtu anayekiuka sheria za usafi anaweza kutozwa faini.

Aidha, alisema suluhisho la taka halipaswi kutegemea kuzifukia pekee, bali Tanzania inapaswa kuangalia teknolojia zinazowezesha taka kuchakatwa na kuzalisha nishati pamoja na bidhaa nyingine.

Amesema baadhi ya nchi, ikiwemo China, zimewekeza katika teknolojia za kuchakata taka kwa njia zinazoweza kuzalisha nishati na kutumia mabaki katika uzalishaji wa bidhaa za ujenzi.

Bw.Balile amesema, matumizi ya teknolojia yanaweza kusaidia kupunguza mzigo katika maeneo ya kutupia taka ikiwemo Dampo la Pugu.

Dar es Salaam yazalisha taka kila siku

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam,Bw. Abdul Rajabu Mhinte amesema,ukubwa na idadi ya watu zikiwemo shughuli za kiuchumi katika jiji hilo unafanya uzalishaji wa taka kuwa jambo lisiloepukika.
Amesema, Dar es Salaam ni miongoni mwa mikoa yenye mkusanyiko mkubwa wa watu nchini, huku idadi hiyo ikiendelea kuongezeka kutokana na watu kuingia jijini kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

“Wananchi wa Dar es Salaam kila siku wanazalisha takataka, na hatuwezi kuepuka hilo. Lililobaki ni kuzidhibiti ili maisha yaendelee katika hali ya usafi."

Bw.Mhinte amesema, licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali na wadau wengine, utekelezaji wa baadhi ya mipango ya usafi bado haujaendana kikamilifu na kiwango cha uwekezaji kinachohitajika.

Amesema, hali hiyo ndiyo sababu ya kuhitajika ushirikiano mpana wa kamati na taasisi mbalimbali katika kutafuta suluhisho la kudumu la changamoto za taka na usafi wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here