Tanzania itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji kukuza biashara na Oman-Naibu Waziri Londo

MUSCAT-Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza utayari wa kuendelea kuweka mazingira bora na rafiki ya uwekezaji ili kukuza sekta ya biashara na kuleta manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania na Usultani wa Oman.
Hayo yameelezwa leo Septemba 29, 2026 na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb.), alipotembelea ofisi za Wekeza Oman na kuzungumza na Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Kukuza Uwekezaji (MoCIIP) anayeshughulikia Biashara na Viwanda Mhandisi Ghalib Al Maamari, mjini Muscat.

Mhe. Londo ameeleza kuwa,ingawa takwimu za biashara kati ya nchi hizo mbili zimekua kutoka Dola za Marekani Milioni 18 mwaka 2017 hadi kufikia Dola Milioni 160.8 mwaka 2025, Tanzania imejipanga kuondoa vikwazo vya kiuwekezaji na kutumia nafasi yake ya kimkakati kijiografia kufungua masoko mapya.
Akiwasilisha fursa zilizopo Tanzania, Mhe. Londo alibainisha kuwa Tanzania inatoa lango kuu la kibiashara linaloiunganisha Oman na soko kubwa la zaidi ya watu Milioni 700 katika Ukanda wa Nchi za Afrika Mashariki (EAC) na Kusini mwa Afrika (SADC).

“Tunawakaribisha kuwekeza katika Sekta mbali mbali ikiwemo machinjio ya kisasa, uchakataji wa nyama na mazao ya baharini, pamoja na kilimo cha biashara ili kuimarisha salama wa chakula na kuongeza kiasi cha bidhaa za Tanzania zinazouzwa katika soko la Oman na Nchi za Ghuba,” amesema Mhe. Londo.
Kwa upande wake, Mhandisi Al Maamari ameelezea nia ya Oman kuendelea kuwekeza Tanzania katika Sekta mbalimbali za Kimkakati kwa manufaaa ya mataifa yote mawili.

Mbali na mazungumzo hayo, Mhe. Londo ametembelea ofisi za Mamlaka ya Uwekezaji Oman (OIA) na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Idara hiyo Mhe. Mulham bin Basheer Al Jarf.
Mazungumzo yao yalijikita katika kubadili uhusiano baina ya Tanzania na Oman kutoka undugu wa kihistoria pekee na kuwa ushirika wa kiuchumi wenye manufaa kwa pande zote mbili kupitia kuanzisha miradi ya ushirikiano wa pamoja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here