Balozi Kilima awataka waandishi wa habari Tanzania na Oman kutumia historia kujenga uhusiano mpya

NA GODFREY NNKO

SERIKALI ya Tanzania imewataka waandishi wa habari wa Tanzania na Oman kutumia nafasi waliyonayo kuandika na kusambaza taarifa sahihi, za kina na zenye kuelimisha umma kuhusu historia, utamaduni na fursa zilizopo katika uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima ametoa wito huo leo Oktoba 1,2026 jijini Dar es Salaam wakati akifungua kongamano la waandishi wa habari kutoka Tanzania na Oman.

Balozi Kilima amesema,Tanzania na Oman zina uhusiano wa muda mrefu uliojengwa katika misingi ya historia, utamaduni, biashara na undugu, huku Bahari ya Hindi ikiwa kiungo muhimu kilichowezesha mwingiliano wa watu wa pande hizo mbili kwa vizazi vingi.

Amesema,katika kipindi hicho, watu kutoka Oman walipovuka Bahari ya Hindi kuelekea Afrika Mashariki, hawakuleta bidhaa pekee, bali pia walileta lugha, maarifa, mila na utamaduni ambao kwa muda mrefu umekuwa sehemu ya historia ya jamii za Tanzania.

Hata hivyo, amesema pamoja na historia hiyo ndefu, bado kuna uelewa mdogo miongoni mwa baadhi ya wananchi wa Tanzania na Oman kuhusu ukubwa na thamani ya uhusiano huo.

Balozi Kilima amesema, wanahabari wana wajibu mkubwa wa kuufanya uhusiano huo ujulikane zaidi, hususan kwa kizazi kipya, kwa kuandika na kusambaza taarifa zinazojenga uelewa kuhusu historia na fursa zinazotokana na mahusiano ya Tanzania na Oman.

“Kuna wajibu mkubwa kwa waandishi wa habari kuupa urafiki huu maana mpya kwa vijana wetu kwa kuandika na kusambaza habari sahihi kuhusu uhusiano wetu huu,"amesema.

Balozi Kilima amesema, Serikali inatambua nafasi ya vyombo vya habari katika kujenga uelewa wa wananchi, kuibua hoja za kijamii na kuhakikisha masuala muhimu ya umma yanafika kwa wahusika na watunga sera.

Amesema,vyombo vya habari vinapotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, vinaweza kusaidia wananchi kuelewa masuala mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, huku vikitoa nafasi kwa jamii kueleza mahitaji na changamoto zake.

Pia, amesema uandishi wa habari una jukumu muhimu katika uchunguzi na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali, kwa kutoa taarifa zinazosaidia wananchi kupata picha halisi ya matukio na kujenga uelewa mpana.

Balozi Kilima amelipongeza Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania kwa kushiriki katika kuanzisha na kuwezesha kongamano hilo, akisema ni hatua inayoweza kufungua milango mipya ya ushirikiano kati ya wanahabari wa nchi hizo mbili.

Aidha, Balozi Kilima amewataka wanahabari kutoka Oman kutumia ziara yao nchini Tanzania kutembelea maeneo mbalimbali yenye umuhimu wa kihistoria, kitalii na kiuchumi ili kupata uelewa mpana zaidi wa Tanzania.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro, pamoja na maeneo mengine yanayotoa fursa katika utalii, michezo ya maji na uwekezaji.

Amesema, ziara hizo zitawasaidia wanahabari wa Oman kupata uzoefu wa moja kwa moja kuhusu Tanzania na hivyo kuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuandika habari zinazohusu nchi kwa uhalisia na kina.

Balozi Kilima ameongeza kuwa, mahusiano ya watu wa nchi mbili hayawezi kuimarishwa kwa mikutano pekee, bali yanahitaji wananchi na wataalamu wa pande zote kutembeleana, kubadilishana uzoefu na kuelewa mazingira ya wenzao.

Katika hotuba yake, Balozi Kilima pia ametumia fursa hiyo kueleza namna michezo inavyoweza kuwa nyenzo ya kuimarisha urafiki na kubadilishana utamaduni kati ya Tanzania na Oman.

Amesema, wakati Oman ikiwa katika mashindano ya Kombe la Ghuba (Gulf Cup), Tanzania nayo inajiandaa kuwa mwenyeji wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

Amewatakia kila la heri wanamichezo wa Oman katika mashindano hayo na kusema matukio ya michezo yanaweza kuwa jukwaa muhimu la kuwakutanisha watu wa mataifa mbalimbali na kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu na tamaduni.

Vilevile amesema,bado kuna changamoto ya taarifa kuhusu matukio hayo kwa wananchi wa pande zote mbili, akitoa mfano kwamba baadhi ya Watanzania huenda hawana taarifa za kutosha kuhusu mashindano yanayoshirikisha Oman, huku baadhi ya wananchi wa Oman huenda hawafahamu kikamilifu maandalizi ya Tanzania, Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa AFCON.

Hivyo, amewataka wanahabari kutumia nafasi yao kusambaza taarifa kuhusu matukio hayo ili kuongeza uelewa na kutumia michezo kama daraja la kujenga mahusiano mapya.

Balozi Kilima amewataka wanahabari na taasisi zao kuanzisha ushirikiano wa kudumu na wenzao wa Oman, ukiwemo mpango wa kubadilishana uzoefu na kufanya ziara za kitaaluma katika nchi hizo mbili.

Amesema, ziara za kitaaluma zinawapa wanahabari nafasi ya kujifunza mazingira mapya, mitazamo tofauti na mbinu mbalimbali za utendaji ambazo zinaweza kuimarisha taaluma yao wanaporejea katika vituo vyao vya kazi.

Amesema, Tanzania na Oman zinaweza pia kushirikiana katika mafunzo ya uandishi wa habari wa kidijitali, uhakiki wa taarifa, matumizi sahihi ya teknolojia na kuwapa nafasi zaidi wanahabari vijana, hususan wanawake.

Balozi Kilima amesema, maeneo hayo yana umuhimu mkubwa kutokana na mabadiliko ya haraka yanayotokea katika sekta ya habari kutokana na maendeleo ya teknolojia na ongezeko la matumizi ya majukwaa ya kidijitali.

Pia,amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha makubaliano yanayofikiwa na taasisi za wanahabari wa Tanzania na Oman yanatekelezwa badala ya kubaki kwenye hati za makubaliano pekee.

Amesema, uzoefu unaonesha kuwa wakati mwingine taasisi huwa zinasaini makubaliano ya ushirikiano, lakini utekelezaji wake hauendi sambamba na matarajio yaliyowekwa.

Hata hivyo, amesema amefurahishwa na mkakati wa kuwa na mpango wa utekelezaji wa miezi 12 baada ya kusainiwa kwa makubaliano kati ya wadau wa habari wa Tanzania na Oman.

Amesema, utekelezaji wa mpango huo ndio utakaokuwa kipimo muhimu cha mafanikio ya ushirikiano huo.

“Tutawapima kwa utekelezaji wa huo mpango kazi ambao watakuwa wamejiwekea,”amesema Balozi Kilima.

Amesema, mpango huo unaweza kusaidia kuweka ratiba ya shughuli za pamoja, ziara, mafunzo, uzalishaji wa maudhui na shughuli nyingine za kitaaluma zitakazowahusisha wanahabari wa pande zote mbili.

Balozi Kilima ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wadau na taasisi zilizochangia kufanikisha kongamano hilo, ikiwemo Media Council of Tanzania, OmanTel, Oman Air na Inspire Tanzania.

Amewashukuru pia mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali waliotenga muda wao na kuhudhuria mkutano huo, akisema uwepo wao unaonesha umuhimu unaotolewa kwa juhudi za kuanzisha ushirikiano mpya kati ya vyombo vya habari vya Tanzania na Oman.

Aidha, amewashukuru waandishi wa habari kutoka Oman na Tanzania pamoja na washiriki wengine waliohudhuria kongamano hilo, akisema ushiriki wao ndio unaoipa shughuli hiyo uzito na umuhimu.

Amesema,anaamini mkutano huo utakuwa mwanzo wa hatua mpya katika kujenga ushirikiano wa muda mrefu kati ya wanahabari wa nchi hizo mbili, huku historia ya pamoja ikitumika kama msingi wa kuendeleza mahusiano ya kizazi cha sasa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here