NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetangaza bei kikomo mpya za bidhaa za mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa, zitakazoanza kutumika leo Jumatano, Oktoba 7, 2026 kuanzia saa 6:01 usiku.
Kwa mujibu wa taarifa ya EWURA yenye Kumb. Na. PPR/2026-10/01, mabadiliko ya bei yanatokana na mwenendo wa soko la mafuta duniani, ambapo bei za mafuta ghafi zimeongezeka katika kipindi cha Septemba 2026, hali iliyochangiwa na ongezeko la uzalishaji, upatikanaji na usafirishaji wa mafuta duniani.
EWURA imesema, kutokana na hali hiyo, kwa mwezi Oktoba 2026, bei za petroli, dizeli na mafuta ya taa nchini zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotangazwa kwa mwezi Septemba 2026.
Katika jiji la Dar es Salaam, bei kikomo ya rejareja kwa lita moja ya petroli imefikia Sh4,057, dizeli Sh4,086, huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa bei ya juu isiyozidi Sh4,067 kwa lita.
Kwa mwezi Septemba 2026, katika Bandari ya Dar es Salaam bei ya Petroli ilikuwa ni Shilingi 3,796 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,877 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,713 kwa lita.
Kwa upande wa Tanga kwa mwezi Oktoba, bei kikomo ya petroli ni Sh4,123 kwa lita, dizeli Sh4,152, na mafuta ya taa Sh4,133 kwa lita.
Aidha, kwa Septemba katika Bandari ya Tanga, bei ya Petroli ilikuwa ni Shilingi 3,872 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,953 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,789 kwa lita.
Mtwara, bei kikomo ya petroli ni kwa mwezi Oktoba ni Sh4,170 kwa lita, dizeli Sh4,199, huku mafuta ya taa yakiwa Sh4,180 kwa lita.
Aidha, katika Bandari ya Mtwara bei ya Petroli kwa Septemba ilikuwa ni Shilingi 3,909 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,990 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,825 kwa lita.
EWURA imesema, bei hizo ni viwango vya juu vinavyoruhusiwa kwa wafanyabiashara wa mafuta, huku wafanyabiashara wakiwa huru kuuza bidhaa hizo kwa bei iliyo chini ya viwango vilivyotangazwa, kwa kuzingatia ushindani na gharama zao za uendeshaji.
Aidha, kwa bei za jumla, Dar es Salaam imewekewa kikomo cha Sh3,909.62 kwa lita ya petroli, Sh3,937.91 kwa dizeli na Sh3,920.05 kwa mafuta ya taa.
Tanga, bei ya jumla ya petroli ni Sh3,906.19 kwa lita na dizeli Sh3,934.06, wakati Mtwara petroli ni Sh3,905.70 na dizeli Sh3,932.94 kwa lita.
Vilevile,kwa mwezi Septemba 2026, bei kikomo za jumla za bidhaa za mafuta ya petroli katika Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara zilikuwa kama ifuatavyo:
Katika Bandari ya Dar es Salaam bei ya Petroli ilikuwa ni Shilingi 3,649.09 kwa lita, Dizeli ni Shilingi 3,729.79 kwa lita na Mafuta ya Taa ni Shilingi 3,566.34 kwa lita.
Bandari ya Tanga bei ya Petroli ilikuwa ni Shilingi 3,670.26 kwa lita na Dizeli ni Shilingi 3,726.81 kwa lita, huku Bandari ya Mtwara bei ya Petroli ilikuwa ni Shilingi 3,653.33 kwa lita na Dizeli ni Shilingi 3,727.62 kwa lita.
EWURA imewataka wafanyabiashara wa bidhaa za mafuta kuzingatia bei zilizotangazwa, huku ikitoa onyo kwamba hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya mfanyabiashara yeyote atakayekiuka agizo hilo.
HIZI HAPA BEI ZA MAFUTA OKTOBA 2026
Tags
Bei ya Mafuta
Bei ya Mafuta Juu
Bei ya Mafuta Tanzania
Diezeli na Petroli
EWURA
EWURA Tanzania
Habari
Mafuta ya Taa
Uchumi wa Tanzania







