BoT yaibuka mshindi wa jumla Maonesho ya Tanzanite 2026 Manyara

MANYARA- Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeibuka mshindi wa jumla katika Maonesho ya Nne ya Biashara ya Tanzanite Manyara yaliyohitimishwa leo Oktoba 21, 2026 katika Viwanja vya Tanzanite Kwaraa, Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la BoT wakati wa maonesho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Bw. Ephraim Balozi Mafuru, aliyemwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, katika hafla ya kufunga maonesho hayo, ameipongeza Benki Kuu kwa mchango wake katika kukuza uchumi wa nchi na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa manufaa ya Taifa.

Bw. Mafuru ameeleza kuwa miongoni mwa mafanikio yanayochangia maendeleo ya uchumi ni juhudi za Benki Kuu katika kuratibu ununuzi wa dhahabu, hatua iliyochangia kuimarisha akiba ya fedha za kigeni nchini.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya chapa ya “Made in Tanzania” miongoni mwa wajasiriamali, hususan katika sekta ya madini, kwa lengo la kukuza biashara za ndani na kuimarisha utambulisho wa bidhaa za Tanzania.

Kwa upande wake, Meneja wa Uendeshaji, Tawi la BoT Arusha, Bw. Cletus Mwakalinga, amesema kuwa maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuwasiliana moja kwa moja na wananchi, kujibu maswali yao na kuongeza uelewa kuhusu majukumu ya Benki Kuu katika kusimamia sekta ya fedha na kuchangia utulivu wa mfumo wa fedha nchini.
Ushiriki wa BoT katika Maonesho ya Tanzanite Manyara unaakisi dhamira ya Benki Kuu ya kuimarisha elimu kwa umma, kujenga uhusiano imara na wadau na kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here