BoT yaziagiza benki za biashara Manyara kupokea fedha zilizochakaa zenye vigezo

MANYARA- Benki za biashara mkoani Manyara zimeagizwa kuhakikisha zinapokea fedha zilizochakaa zinazokidhi vigezo vinavyokubalika, kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu baadhi ya benki kukataa kupokea fedha hizo.
Agizo hilo limetolewa na Meneja wa Uendeshaji wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Tawi la Arusha, Cletus Mwakalinga, wakati wa Maonesho ya Biashara ya Tanzanite Manyara yanayofanyika katika Viwanja vya Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara, kuanzia Oktoba 15 hadi 21, 2026.

Mwakalinga amesema, fedha zilizochakaa zinaweza kupokelewa iwapo ni halali, zimebaki nzima kwa angalau asilimia 75 ya sehemu yake ya awali na hazijaharibiwa kwa makusudi.
Aidha, amewahimiza wananchi kutunza fedha zao katika mazingira bora ili kuzuia zisichakae au kuharibika mapema. Amesisitiza umuhimu wa kuepuka kuhifadhi fedha katika sehemu zisizofaa zinazoweza kusababisha uharibifu wake.

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa maonesho hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati, Shaaban Mpendu, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Martin Shigela, amewahimiza wananchi kutumia maonyesho hayo kutangaza biashara zao, kujitangaza na kununua bidhaa mbalimbali zinazopatikana.
Mpendu amesema, maonesho hayo ni fursa muhimu kwa wafanyabiashara na wajasiriamali kukuza shughuli zao za kiuchumi, kutangaza bidhaa na huduma wanazozalisha, pamoja na kupanua wigo wa wateja.

Benki Kuu ya Tanzania inashiriki katika maonyesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake, pamoja na kupokea maoni na mrejesho kutoka kwa wananchi wa Manyara kuhusu utendaji wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here