NA GODFREY NNKO
SEKTA ya michezo nchini Tanzania inahitaji kuongeza kasi ya matumizi ya mifumo ya kisheria ya umiliki bunifu ili kulinda na kuongeza thamani ya mali za wanamichezo, vilabu na taasisi mbalimbali za michezo, huku ikielezwa kuwa sekta hiyo ina fursa kubwa ya kuzalisha ajira, mapato na utajiri wa muda mrefu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa amesema hayo leo Oktoba 6, 2026 wakati akizungumza katika warsha kuhusu Umiliki Bunifu na Michezo iliyofanyika katika Ukumbi wa King Jada Hotel jijini Dar es Salaam.
Bw.Nyaisa amesema, licha ya Tanzania kuwa na mashabiki wengi wa michezo, hususan soka pamoja na vilabu vyenye ushawishi mkubwa kama Simba na Yanga na timu za taifa, bado kuna changamoto ya kiuchumi inayotokana na kutotumia kikamilifu fursa zinazotokana na umiliki bunifu.
Amesema, umiliki bunifu ni eneo muhimu linaloweza kuwa chanzo kikubwa cha mapato kwa wanamichezo na vilabu endapo litasimamiwa kwa weledi na kulindwa kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Bw. Nyaisa, umiliki bunifu ni sawa na “shamba la bibi” lisilochumwa, akimaanisha kuwa kuna fursa kubwa ambazo bado hazijatumika ipasavyo katika sekta ya michezo na ambazo zinaweza kubadilisha maisha ya wanamichezo pamoja na kuimarisha uchumi wa vilabu.
“Umiliki bunifu ni shamba la bibi ambalo halijachumwa. Likisimamiwa vizuri lina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha ya wanamichezo na kuziendesha klabu zetu kwa tija na uendelevu,” amesema.
Bw.Nyaisa amesema,umiliki bunifu ni nyanja pana inayogusa maeneo mbalimbali ya maisha na shughuli za kiuchumi, ikiwemo sekta ya michezo.
Amesema, katika michezo, umiliki huo unahusisha ulinzi na usajili wa alama za biashara, nembo za vilabu, miundo bunifu, pamoja na haki mbalimbali zinazotokana na ubunifu na shughuli za kibiashara zinazofanywa ndani ya tasnia hiyo.
Ameonya kuwa, wanamichezo na viongozi wa vilabu wanaweza kupoteza fursa kubwa za kifedha iwapo wataendelea kuuchukulia mchezo kama burudani pekee badala ya kuuona kama shughuli ya kiuchumi inayoweza kuzalisha mitaji na kujenga utajiri wa kudumu.
“Wanamichezo wengi wanapoteza mamilioni ya fedha kwa sababu wanachukulia michezo kama burudani pekee na kusahau kuwa ni biashara kubwa inayoweza kuzalisha mitaji na utajiri wa kudumu,” amesema.
Amesema, vilabu vikubwa nchini ikiwemo Simba na Yanga, tayari vinapata mapato kupitia mauzo ya jezi, skafu na bidhaa nyingine zenye alama na nembo za vilabu hivyo.
Hata hivyo, amesema kuwepo kwa wazalishaji na wauzaji wa bidhaa bandia kunapunguza mapato ambayo yangepaswa kwenda kwa wenye haki, huku pia kukiathiri thamani ya chapa za vilabu.
Amesema, usajili wa alama za biashara kupitia BRELA ni hatua muhimu inayovipa vilabu ulinzi wa kisheria na uwezo wa kuchukua hatua dhidi ya watu au taasisi zinazotumia alama hizo bila ruhusa.
Bw.Nyaisa amesema, hatua hiyo pia inaweza kusaidia vilabu kuongeza thamani ya chapa zao, kuvutia wawekezaji na wadhamini na kujenga mifumo endelevu ya mapato nje ya mapato ya siku ya mechi.
Kwa upande mwingine, Bw.Nyaisa amesema, baadhi ya wanamichezo nchini bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu haki zinazoweza kupatikana kutokana na majina, picha, taswira na ubunifu wao.
Amesema, hali hiyo imekuwa ikiwafanya baadhi yao kusaini mikataba bila kupata ushauri wa kutosha kutoka kwa wataalamu wa sheria za umiliki bunifu, jambo linaloweza kusababisha kupoteza haki na mapato yanayotokana na matumizi ya utambulisho wao kibiashara.
Amesema, majina, picha na taswira za wachezaji zinaweza kuwa mali yenye thamani kubwa kibiashara, hasa pale zinapotumiwa katika matangazo, bidhaa, kampeni za kibiashara na shughuli nyingine za uuzaji.
Hivyo, Bw.Nyaisa amewataka wanamichezo kuhakikisha wanapata ushauri wa kitaalamu kabla ya kusaini mikataba inayohusu matumizi ya majina, picha au taswira zao.
Amesema, ulinzi huo unaweza kumwezesha mwanamichezo kunufaika na thamani ya jina na taswira yake hata baada ya kustaafu.
Bw.Nyaisa amesema, sekta nyingine za ubunifu, hususan muziki na burudani, zimeanza kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kusajili na kulinda kazi, majina na alama zao.
Amesema, uzoefu huo unaweza kuwa mfano kwa sekta ya michezo, ambayo inapaswa kuhakikisha mali zote zinazohusiana na utambulisho wa klabu, wachezaji na taasisi zake zinalindwa kisheria.
Pia, amesisitiza kuwa, usajili wa haki hizo si suala la kuongeza urasimu, bali ni uwekezaji unaoweza kuzuia upotevu wa mapato, kupunguza migogoro na kuongeza thamani ya biashara ya michezo.
BRELA imeendelea kutoa wito kwa wadau wa sekta ya michezo wakiwemo wanamichezo, viongozi wa vilabu, mashirikisho na taasisi nyingine zinazohusika kutumia huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo kupata elimu na kusajili mali zao za umiliki bunifu.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Bw. Nyaisa itasaidia kupunguza mianya ya unyonyaji, kuimarisha ulinzi wa kisheria na kuweka mazingira bora ya kuifanya sekta ya michezo kuwa chanzo endelevu cha ajira, uwekezaji na mapato.
Amesema, Tanzania ina uwezo mkubwa wa kutumia michezo kama sehemu ya uchumi wa taifa iwapo wadau wataanza kuiona sekta hiyo kwa mtazamo mpana zaidi, unaozingatia biashara, uwekezaji na ulinzi wa haki za wabunifu na wenye mali bunifu.
Vilevile, amesema ni wakati kwa wanamichezo na viongozi wa vilabu kuachana na mtazamo unaoiona michezo kama burudani pekee na badala yake kutambua kuwa michezo ni biashara inayohitaji uwekezaji, usimamizi na ulinzi wa kisheria.
Amesema, uwekezaji katika umiliki bunifu ni miongoni mwa hatua muhimu za kuhakikisha thamani inayozalishwa na michezo inawanufaisha zaidi wanamichezo, vilabu na uchumi wa taifa kwa ujumla.






