OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni zao la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Majukumu ya Ofisi hii yanaelezwa katika Ibara ya 59(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, na pia Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa mwaka 2018 pamoja na Tangazo la Serikali Namba 48 la mwaka 2018.
Pamoja na majukumu mengine, Ofisi hii inawajibika kutoa ushauri kwa Wizara, Idara za Serikali na Taasisi nyingine za Serikali na Mashirika ya Umma kuhusu mchakato wa kutunga sheria na ushauri wa kisheria katika masuala ya jumla na katika uandaaji wa miswada kwa ajili ya kupitishwa na Bunge ili kuwa sheria.
DIRA
Kuwa taasisi yenye ufanisi, kitaaluma na kuaminika katika kutoa huduma bora za Kisheria kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
DHIMA
Kutoa huduma za kisheria zenye ubora kwa njia ya kuandaa Sheria, Upekuzi na Majadiliano ya Mikataba pamoja na Ushauri wa Kisheria kwa Maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi na Kisiasa.
MAJUKUMU YA OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
1: URATIBU NA HUDUMA ZA KISHERIA
Kuratibu na kusimamia utoaji na uwiano wa huduma za kisheria katika Wizara, Idara, Wakala za Serikali (MDAs), Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs) na Wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na sera za nchi.
2: UPEKUZI WA MIKATABA
Kufanya upekuzi wa Mikataba, kutoa ushauri na kuendesha majadiliano kwa niaba ya Serikali katika Mikataba yote.
3: MAJADILIANO, USIMAMIZI WA MIKATABA NA UTATUZI WA MIGOGORO
Kutoa usimamizi mkuu wa majadiliano ya mikataba, usimamizi wa vihatarishi, na utatuzi wa migogoro inayohusisha Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala za Serikali (MDAs), Mamlaka za Serikali za Mitaa (LGAs), na huduma za taasisi na mashirika mengine ya Serikali.
