Kituo cha Taarifa cha Nandete kupata msukumo mpya, jiwe la msingi lawekwa katika kilele cha kumbukizi ya miaka 121 ya Vita vya Maji Maji

LINDI-Serikali imeendelea kuweka msukumo katika kuhifadhi na kuendeleza historia ya Vita vya Maji Maji kwa kuweka jiwe la msingi katika jengo la Kituo cha Taarifa cha Nandete kilichopo Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi, linalotarajiwa kukamilika mwakani na kuwa sehemu muhimu ya utoaji wa taarifa kuhusu historia na urithi wa eneo hilo.
Jiwe hilo la msingi limewekwa jana katika kilele cha Maadhimisho ya Miaka 121 ya Kumbukizi ya Vita vya Maji Maji, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohamed Nyundo, alikuwa Mgeni Rasmi katika hafla hiyo iliyowakutanisha viongozi, wananchi, wazee wa mila pamoja na wadau mbalimbali wa uhifadhi wa historia na urithi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Nyundo amesema uwekezaji huo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha historia na urithi wa mashujaa wa Vita vya Maji Maji unatunzwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Amesema kituo hicho kitakuwa na umuhimu mkubwa katika kutoa taarifa na kuibua historia ya Vita vya Maji Maji, hususan matukio yaliyohusisha eneo la Nandete, huku kikitarajiwa pia kuchochea shughuli za utalii na uchumi wa wananchi.
Mhe. Nyundo amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutumia fursa zitakazotokana na uwekezaji huo, ikiwemo kuendelea kujenga nyumba za kulaza wageni na kuboresha huduma mbalimbali ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea Nandete na kunufaisha jamii kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, amewashukuru wananchi wa Nandete na Kilwa kwa kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kwa namna walivyolipokea na kulishiriki suala la uhifadhi wa historia ya Vita vya Maji Maji.

Dkt. Lwoga amesema, mwitikio mkubwa wa wananchi unaonesha kuwa historia ya Vita vya Maji Maji bado ina nafasi muhimu katika jamii na kwamba ushirikiano wa wananchi ni msingi mkubwa katika kuhakikisha urithi huo unahifadhiwa na kuendelezwa.

Amesema Kituo cha Taarifa cha Nandete kitakapokamilika kitakuwa nyenzo muhimu ya kutoa elimu kwa wananchi, wanafunzi, watafiti na wageni kuhusu historia ya Vita vya Maji Maji, pamoja na kuwa sehemu ya kuimarisha utalii wa urithi katika eneo la Kilwa.
"Tunawashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi na kulipokea suala hili. Ushiriki wenu unaonesha wazi kwamba historia hii ni ya wananchi na inapaswa kuhifadhiwa na kurithishwa kwa vizazi vijavyo,” amesema Dkt. Lwoga.

Maadhimisho hayo ya miaka 121 yamefanyika chini ya kaulimbiu 'MAJIMAJI NA URITHI WA KILWA', ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi mashujaa wa Vita vya Maji Maji, kuimarisha uhifadhi wa maeneo ya kihistoria na kutumia urithi wa Kilwa kama fursa ya kukuza utalii, elimu na uchumi wa jamii.

Kuwekwa kwa jiwe la msingi la Kituo cha Taarifa cha Nandete kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kutoa msukumo mpya kwa uhifadhi wa historia, urithi na utalii wa Kilwa, huku kituo hicho kikitarajiwa kukamilika mwaka 2027.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here