Soma habari zote muhimu leo Oktoba 16, 2026 kutoka katika magazeti makubwa ya Tanzania kama Mwananchi, HabariLeo, Majira, Nipashe, Zanzibar Leo, Raia Mwema, Mwanahalisi, Uhuru, Pambazuko, Jamhuri na mengineyo kila siku bila malipo.
Gazeti la Mwananchi leo Ijumaa, Oktoba 16, 2026 lina habari kuu ya ripoti kubaini ahadi nono zinazowatumbukiza Watanzania kwenye kazi za shuruba zisizo na staha, huku hatua za Serikali zikielezwa.
Ndani ya habari hiyo, vijana 58 wanadaiwa kusafirishwa kwa madai ya kazi nje ya nchi na kusababisha changamoto kubwa, huku tahadhari ikitolewa dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu.
Pia ndani: Alipo Pambalu bado kitendawili na Chadema kwenda mahakamani, Bagonza ataka mfumo wa haki ubadilishwe kukomesha mauaji, Kweka kortini mauaji ya Jeni Magembe kesi yake kuendelea, Mikopo chechefu inavyoibua hofu kwenye Saccos, na hatari ya dawa kwa wanaopitia ukomo wa hedhi.
Gazeti la Mtanzania Leo leo Jumaa, Oktoba 16 2026. Umoja wa Afrika (AU) umesaini mkataba na Hospitali ya Shifaa Pan African ya Dar es Salaam kwa ajili ya kushirikiana katika sekta ya afya, ambapo wagonjwa kutoka mataifa 54 wanatarajiwa kuja kutibiwa nchini kwa huduma za kibingwa. Hatua hii inaiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia katika utalii tiba. Gazetini pia: Kamati ya Bunge ya Bajeti yaipongeza TRA, Rais Samia apokea hati za Balozi wa Ufaransa na Ecobank yafungua ofisi China.
Gazeti la Majira leo Ijumaa, Oktoba 16, 2026 limeangazia habari kuu ya Waziri wa Fedha Tanzania, Balozi Omar akisema ajira ni suala la kipaumbele kwa Tanzania, ambapo amesisitiza kuwa, Tanzania inaunga mkono mkakati maalum wa Benki ya Dunia (WB) kusaidia mipango ya maendeleo na miradi itakayochochea ajira kwa pamoja na Afrika.Pia ndani ya Majira: Tanzania yajipambanua kimataifa katika uimarishaji wa mifumo ya maafa, Tanzania yaimarisha diplomasia ya kibunge, Rukwa kunufaika na mradi wa umeme, Serikali kutokuwa kikwazo kwa wawekezaji wa miradi ya maendeleo na Mwigulu ataka Afrika kuimarisha usafiri wa majini.
Katika kurasa za michezo, Majira lina habari kuu ya Timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 'Serengeti Boys' kupigwa chini katika michuano ya AFCON U-17 kwa kufungwa na Somalia, hivyo kukosa fursa ya kusonga mbele.Habari nyingine ni Azam FC kucheza leo kwenye michuano ya CAFCC ambapo viongozi wametia hamasa, na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuimarisha sekta ya utalii kuelekea AFCON 2027.
Gazeti la Biashara Leo leo Ijumaa, Oktoba 16, 2026 limeipa uzito habari ya Kamati ya Bunge ya Bajeti kuipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ukusanyaji wa mapato bila kuvutana na wananchi na kwa matumizi ya mifumo ya kidijitali.Kamati hiyo imepata mafunzo kuhusu mifumo ya IDRAS na TANCIS, pamoja na mpango wa mamlaka hiyo wa kufunga Scanner za ukaguzi wa mizigo kwenye mipaka yote kwa lengo la kuboresha huduma za kodi na kudhibiti mapato.
Pia ndani: Tanzania yaweka mkazo ajira kwa vijana katika mkutano wa Benki ya Dunia nchini Thailand kupitia Waziri wa Fedha Balozi Khamis Musa Omar, Ecobank yafungua ofisi China, na Hospitali ya Shifaa Pan African ya Dar yasaini mkataba na Umoja wa Afrika (AU).
Gazeti la Sauti Yetu leo Ijumaa, Oktoba 16, 2026 limempa kipaumbele Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Juma Mwenda ambapo Mfumo wa IDRAS wa TRA umetua kwa wabunge.
CG Mwenda ameongoza timu kutoa darasa kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na wameridhishwa na ufanisi wa mifumo hiyo.
Pia, katika toleo hili: Tanzania imeweka mkazo mkakati maalum ajira kwa Vijana kupitia Waziri wa Fedha Balozi Khamis Musa Omar katika mkutano wa IMF na Benki ya Dunia nchini Thailand, Luhaga Mpina ataka kuwaburuza Mawaziri wawili Mahakamani, na TANECU kuanza minada ya korosho leo.
Katika Gazeti la Mwananchi Huru leo Ijumaa Oktoba 16, 2026 habari kuu ni Tanzania yazidi kung'ara kimataifa kwenye sekta ya Utalii Tiba.
Gazeti la Mwananchi Huru leo lina habari kuu ya Umoja wa Afrika (AU) kusaini mkataba na Hospitali ya Shifaa Pan African ya Dar es Salaam, ambapo wagonjwa kutoka mataifa 54 wanatarajiwa kuja kutibiwa katika hospitali za Tanzania.
Dk Adamu Isah amempongeza Rais Samia kwa uwekezaji sekta ya afya akisema "Hakuna haja tena ya kupeleka wagonjwa Ujerumani wala India".
Pia ndani: Tanzania yaweka mkazo ajira kwa vijana mkutano na Benki ya Dunia (WB) kupitia Waziri wa Fedha Balozi Khamis Musa Omar nchini Thailand, Kamati ya Bunge yaipongeza TRA kwa ufanisi ukusanyaji mapato na matumizi mazuri ya mifumo ya kidijitali, REA yatoa bil 10.78 kuwasha Bugando Solar 5MW, na Ecobank yafungua ofisi yake China.
Gazeti la Raia Mzalendo leo Ijumaa Oktoba 16, 2026 habari kuu ni Hospitali ya Shifaa yaipaisha Tanzania kwenye Utalii Tiba.
Raia Mzalendo leo lina habari kuu ya Hospitali ya Shifaa Pan African ya Kinondoni Dar es Salaam kusaini mkataba na Umoja wa Afrika (AU), ambapo wagonjwa kutoka mataifa 54 wanatarajiwa kuja kutibiwa nchini kwa huduma za kibingwa. Uongozi wa hospitali hiyo umempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya afya.
Pia ndani ya toleo hili: Ujenzi wa nyumba 66 za watumishi wafikia 45%, Aliyemuua mkewe kwa risasi Dar afikishwa mahakamani, Ecobank Group yazidi kujitanua ikifungua ofisi zake China, na Kamati ya Bunge ya Bajeti yafurahishwa na kasi ya TRA.
Gazeti la Wamachinga leo Oktoba 16, 2026 lina habari kuu ya Tanzania kuanza kuiuzia umeme nchi ya Zambia, ambapo Mkoa wa Rukwa unatarajiwa kugeuka kitovu cha biashara hiyo.
Makamu wa Rais amesema mradi wa umeme wa Malangali wa Shilingi bilioni 161.9 utafungua fursa kubwa za viwanda, ajira na uwekezaji.
Ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 85.17 na majaribio ya mitambo yanatarajiwa kuanza Novemba, huku mkoa ukipokea MW 16 pekee dhidi ya mahitaji ya MW 30.
Pia ndani: REA yatoa bilioni 10/- kuongeza Megawati 5 kwenye Gridi ya Taifa Mwanza, Waziri Mwigulu Nchemba azitaka Saccos kugeuza akiba kuwa uwekezaji na ajira huku akihimiza huduma za kidijitali na usimamizi madhubuti, Tanzania yaweka mkazo ajira kwa vijana na uwekezaji wa ndani katika mkutano wa Benki ya Dunia nchini Thailand kupitia Balozi Omar, na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan apokea Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Jean-Marc Pisani, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kwenye kurasa za michezo, Wamachinga Spoti leo lina habari moto. Habari kuu ni mchezo wa Agosto na Simba SC kupigwa Oktoba 20 katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.
Pia kuna sakata la Sure Boy kuidai Yanga SC na kuiburuza TFF, huku timu ya Taifa ya vijana Serengeti Boys ikitolewa kwa kurusha shilingi kwenye michuano ya AFCON U-17.
Ndani zaidi: Azam FC yaifuata ZED FC ya Misri ikiwa na mashabiki wake kwenye michuano ya CAF, na Kocha Minziro asema wamejipanga kuwafunga Pamba Jiji.
Gazeti la Habari Leo leo Ijumaa Oktoba 16, 2026 lina habari kuu kuhusu mageuzi ya Vyama vya Akiba na Mikopo nchini (Saccos), ambapo akiba na amana zimefikia Shilingi trilioni 1.22 na rasilimali trilioni 1.69, huku Saccos 1,016 zikiwa zimepewa leseni.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba ametaka akiba hizo zitumike kwa uwekezaji, huku Waziri Chongolo akiagiza Saccos ziwezeshe uzalishaji.
Pia ndani: Tanzania kuanza kuuza umeme Zambia, Dkt. Samia apokea Hati za Utambulisho za Mabalozi watano akiwemo Balozi wa Marekani nchini William Trachman Ikulu Dar es Salaam, Bilioni 59/- kujenga miundombinu ya maji Dar es Salaam, Ulega ataka ubora wa mafunzo ya Uanasheria, na Kenya yatangaza mgonjwa wa pili wa Ebola.
Gazeti la Habari Leo Michezo leo lina habari kuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kuipatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ruzuku ya Shilingi bilioni 1.8 (Dola 700,000) kutokana na mchango wake wa soka barani Afrika.
Kwenye Ligi Kuu Bara leo, Geita Gold kuikabili Dodoma Jiji na Fountain Gate kuivaa Pamba Jiji. Kocha wa Azam FC, Florent Ibengé, amejipa imani ya kushinda dhidi ya ZED FC ya Misri kwenye michuano ya CAF, huku bahati ya kurusha shilingi ikiwaondoa Serengeti Boys kufuzu AFCON U-17, na kiungo wa Senegal akistaafu soka.

ZANZIBAR LEO - Ijumaa Oktoba 16, 2026
Gazeti la Zanzibar Leo leo lina habari kuu ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akihimiza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Armenia, alipokutana na Rais wa Jamhuri ya Armenia, Vahagn Khachaturyan, jijini Yerevan.
Pia ndani: Dkt. Mwinyi kufungua kongamano la vijana, Dkt. Mwigulu azitaka nchi za Afrika ziimarishe ushirikiano wa usafiri wa majini, Wakaazi wa Mwantenga na Ziwa Maboga kulipwa fidia, Rais amzawadia bajaji muimbaji wa nyimbo za uzalendo Issa Bugondo, na Msemaji wa White House akingiwa kifua.
Gazeti la Zanzibar Leo Michezo leo lina habari kuu ya Wawakilishi wa Tanzania Azam FC kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) watakapoikabili ZED FC ya Misri leo ugenini. Azam inahitaji ushindi au sare yenye mabao baada ya suluhu ya kwanza Dar.
Pia ndani: Kizimkazi Marathon 2026 kukimbizwa Disemba 19 ambapo Mbio hizo zinatarajia kuleta fursa ya kiuchumi na kutangaza utalii, UVCCM na ACT-Wazalendo kutoana jasho, na Sanaa ni roho ya taifa kukuza utamaduni - Kadilin.
MWANASPOTI - Ijumaa Oktoba 16, 2026
Gazeti la MwanaSpoti leo lina habari kuu ya Kocha wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, kupunguza presha kuelekea mechi ya CAF Champions League, akisema wapinzani wao CFFA hawataweza kuwazuia. Yanga inatarajia kucheza kesho saa 9:00 alasiri Uwanja wa Azam Complex.
Pia ndani: Mastaa Yanga waliamsha kuelekea mechi dhidi ya CFFA, Oura: Yanga imetupa mzuka CAF, Azam mguu sawa Misri kuwania kufuzu saa 2:00 dhidi ya ZED FC, Warithi wa Motsepe U17 watajwa, EPL kesho Everton vs Chelsea saa 8:30 mchana.
TANZANIA LEO - Ijumaa Oktoba 16, 2026
Gazeti la Tanzania Leo leo lina habari kuu ya mtazamo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kukuza bandari umeanza kuleta fursa kubwa za uwekezaji.
Waziri Mkuu anasema Dar es Salaam ni lango la Waafrika wote, huku Prof. Mkumbo akiwakaribisha wawekezaji wa India kuitumia.
Pia ndani: TAZARA yaweka mkakati wa kujitegemea kifedha na kufufua reli kwa dola Mil. 207 kuwekezwa, Dkt. Samia aweka historia ya mazingira safi ya uwekezaji,
Mwigulu: SACCOS zisigeuze akiba kuwa uwekezaji na ajira akisisitiza huduma za kidijitali, Uwekezaji wa Dkt. Samia kuifungua Rukwa kiuchumi na kuuza umeme nchi jirani - Ndejembi asema ni fursa kwa wananchi, na Jela miaka 30 kwa kumbaka shangazi yake wa miaka 63.
Gazeti la Tanzania Leo Michezo leo lina habari kuu ya Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi kukutana na viongozi wa klabu ya Real Madrid na Unicorn Sports na kujadili kuinua vipaji Zanzibar. Makubaliano hayo yatafungua fursa kwa vijana na kukuza soka visiwani.
Pia ndani: Barker avujisha siri ya ushindi wa Simba SC dhidi ya Yanga mabao 2-1, Serengeti Boys yaondolewa CECAFA U17 kwa shilingi kurusha, Vini Jr afungiwa mechi nne kuikosa El Clasico, Sure Boy aishitaki Yanga.
MWANAHABARI - Ijumaa Oktoba 16, 2026
Gazeti la Mwanahabari leo lina habari kuu ya mradi wa TAZA wa kuunganisha gridi za umeme za Tanzania na Zambia, ambapo Makamu wa Rais, Ndejembi amesema ni uwekezaji utakaoimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kufungua fursa mpya. Kwa sasa Mkoa wa Rukwa hupokea megawati 16 dhidi ya mahitaji ya megawati 30.
Pia ndani: TARURA yachukua hatua kukabiliana na El Nino na wananchi watakiwa kulinda miundombinu, REA yatoa bilioni 10/- kufanikisha mradi wa Bugando Solar Power Mwanza, Dkt. Mwigulu azielekeza SACCOS Afrika katika uwekezaji wenye tija ili kukuza biashara na ajira, na Dkt. Mwinyi: Tanzania na Armenia kushirikiana katika teknolojia, elimu na utalii.
Gazeti la Mwanahabari Michezo leo lina habari kuu ya Simba SC kuanza maandalizi ya mechi yake dhidi ya Agosto Luanda itakayochezwa Oktoba 20, huku kikosini hali ikiwa juu baada ya ushindi wa mabao 6-1.
Pia ndani: Sure Boy aishitaki Yanga TFF, Azam yaifuata ZED kibabe Misri kwenye CAFCC, Baleke: Kwa Simba hii ningefunga sana, na Kaze awataka mashabiki Kagera kutulia.














