Mapato ya STAMICO yafikia Bilioni 147.8 kutoka Bilioni 1.3

NA GODFREY NNKO

SHIRIKA la Madini la Taifa (STAMICO) limepiga hatua kubwa katika mageuzi ya kiutendaji na kifedha, likiongeza mapato yake ya ndani kutoka Shilingi bilioni 1.3 katika mwaka wa fedha 2018/19 hadi Shilingi bilioni 147.8 katika mwaka wa fedha 2025/26 sawa na ongezeko la asilimia 11,269.

Hatua hiyo inaashiria mabadiliko makubwa katika uwezo wa shirika hilo kujiendesha na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa huku likitekeleza kikamilifu Falsafa ya 4R ya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO, Dkt. Venance Mwasse ameyasema hayo leo Oktoba 16, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini, chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Akiwasilisha mafanikio ya shirika hilo, Dkt. Mwasse amesema, ongezeko la mapato linaakisi mabadiliko yaliyofanywa katika usimamizi wa biashara, uwekezaji, uimarishaji wa miradi na matumizi ya rasilimali zilizopo ili kuongeza tija na ushindani wa shirika katika Sekta ya Madini nchini.

Dkt. Mwasse amesema, mapato ya STAMICO yameongezeka kutoka Shilingi bilioni 1.3 mwaka 2018/19 hadi Shilingi bilioni 147.8 mwaka 2025/26, huku thamani ya mali za shirika ikipanda kutoka Shilingi bilioni 45 hadi Shilingi bilioni 360.

Ukuaji huo unaonesha kupanuka kwa uwezo wa shirika katika kuzalisha mapato na kujenga msingi wa uwekezaji wa muda mrefu, hususan katika sekta ya madini ambayo ni miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania.

UTEGEMEZI WA SERIKALI BASI

Vilevile, STAMICO imepunguza kwa kiasi kikubwa utegemezi wake wa fedha za uendeshaji kutoka Serikalini.

Dkt. Mwasse amesema, wakati wa kuanza kwa mageuzi hayo, takribani asilimia 89 ya mahitaji ya shirika yalitegemea fedha za Serikali.

Hata hivyo, kwa sasa, shirika limefikia mwaka wa nne mfululizo bila kutegemea fedha za matumizi ya kawaida ya Serikali (OC) kwa ajili ya uendeshaji wake, huku likifikisha miaka mitatu mfululizo likigharamia mishahara ya watumishi wake kupitia mapato ya ndani.

Hatua hiyo inaashiria kuimarika kwa uwezo wa STAMICO kugharamia shughuli zake za msingi, kupunguza shinikizo kwa bajeti ya Serikali na kuelekeza nguvu zaidi katika uwekezaji na upanuzi wa shughuli za kibiashara.

Aidha, shirika hilo limetoa gawio la jumla ya Shilingi bilioni 11 kwa Serikali, jambo ambalo, kwa mujibu wa Dkt. Mwasse linaonesha mabadiliko katika uwezo wake wa kuzalisha faida na kurejesha sehemu ya matokeo ya uwekezaji kwa mwanahisa wake.

STAMICO pia limeendelea kupata hati safi za ukaguzi wa hesabu, ishara ya kuzingatiwa kwa taratibu za uwajibikaji na usimamizi wa fedha za shirika.

MIRADI YAONGEZA UWEZO WA KIBIASHARA

Akifafanua sababu zilizochangia ukuaji huo, Dkt. Mwasse amesisitiza umuhimu wa miradi ya kibiashara katika kuhakikisha shirika linaendelea kuwa na vyanzo endelevu vya mapato.
Amesema, STAMICO imepanua shughuli zake kwa kuingia katika mikataba mipya ya uchorongaji, ikiwemo mkataba wa muda mrefu na kampuni ya Geita Gold Mining (GGM), hatua inayolenga kuongeza fursa za kibiashara na kuimarisha mapato yatokanayo na huduma za kitaalamu katika sekta ya madini.

Amesema, idadi ya mitambo ya uchorongaji inayotumika katika shughuli za shirika imeongezeka kutoka mitambo mitatu hadi 18.

Vilevile, shirika limewekeza katika ununuzi wa mashine 15 za uchorongaji kwa ajili ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini, maarufu kama Artisanal and Small-scale Miners (ASM) ili kupata huduma zinazohusiana na shughuli zao za uchimbaji.

Uwekezaji huo unaonesha kuwa, shughuli za STAMICO hazilengi kuongeza mapato pekee, bali pia kupanua huduma zinazotolewa kwa wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji wadogo ambao ni sehemu muhimu ya mnyororo wa thamani wa madini nchini.

AJIRA ZAONGEZEKA KUTOKA 111 HADI 800

Mbali na mafanikio ya kifedha, STAMICO imeongeza pia idadi ya watumishi wake kutoka takribani 111 hadi karibu 800, kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi Mtendaji.

Ongezeko hilo linaonesha namna upanuzi wa shughuli za shirika unavyoweza kwenda sambamba na kuongezeka kwa fursa za ajira kwa Watanzania.

Dkt. Mwasse amesema, mafanikio ya shirika hayapaswi kupimwa kwa faida na mapato pekee, bali pia kwa mchango wake katika kutengeneza ajira na kuwawezesha Watanzania kushiriki katika kutumia rasilimali za madini kwa manufaa ya taifa.

Aidha, katika kuboresha mazingira ya kazi, shirika limechukua hatua mbalimbali zinazohusisha kuimarisha maslahi ya watumishi, kuboresha ofisi na kuongeza vifurushi vya bima ya afya.

Hatua hizo zinalenga kuimarisha ustawi wa watumishi na kuweka mazingira yanayowezesha utekelezaji wa majukumu ya shirika kwa ufanisi zaidi.

MADINI YA KIMKAKATI

Dkt. Mwasse amesema, mafanikio ya sasa yanapaswa kuunganishwa na uwekezaji wa kimkakati utakaoliwezesha shirika kuendelea kuwa na nafasi katika soko la madini kwa miaka ijayo.

Amesema, STAMICO imepata leseni 20 zinazohusiana na madini mbalimbali ya kimkakati yakiwemo bati, grafiti, lithiamu, madini adimu ya ardhini (rare earth elements), manganizi, kobalti, shaba, nikeli na dhahabu.

Dkt. Mwasse amesema, madini hayo yana umuhimu katika uchumi wa kisasa kutokana na matumizi yake katika viwanda, teknolojia, uzalishaji wa betri, nishati safi na shughuli nyingine za viwandani.

Hivyo, uwekezaji katika madini ya kimkakati unaweza kuipa STAMICO fursa ya kupanua shughuli zake zaidi ya huduma za uchorongaji na kuimarisha nafasi yake katika shughuli za utafiti, uendelezaji na uchimbaji wa madini.

Dkt. Mwasse amesema, shirika limeingia pia katika mikataba minne ya ubia inayohusisha madini ya kimkakati, hatua inayolenga kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji na kuongeza uwezo wa kutekeleza miradi yenye tija.

Mikataba hiyo ni sehemu ya mkakati wa shirika wa kujenga vyanzo vya mapato vya muda mrefu, badala ya kutegemea mafanikio ya kifedha ya kipindi kifupi pekee.

KUENDELEZA MIGODI MIKUBWA MITATU

Katika mkakati wake wa muda mrefu, STAMICO imeweka lengo la kuendeleza migodi mikubwa mitatu, ikiwemo migodi miwili ya dhahabu na mmoja wa madini ya msingi.

Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema, shirika linaendelea na hatua za maandalizi ya miradi hiyo ikiwemo kukamilisha tafiti zinazohitajika ili kuweka msingi wa utekelezaji wake.

Mpango huo unaonesha nia ya STAMICO kuongeza ushiriki wake wa moja kwa moja katika shughuli za uchimbaji na uendelezaji wa migodi, badala ya kutegemea zaidi huduma na mikataba ya kibiashara.

Iwapo miradi hiyo itatekelezwa kwa mafanikio, inaweza kufungua fursa mpya za ajira, kuongeza mapato ya shirika na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo yatakayohusika.

Hata hivyo, utekelezaji wake utategemea kukamilika kwa tafiti, maandalizi ya uwekezaji na hatua nyingine muhimu za kitaalamu na kibiashara.

MAGEUZI YANAVYOENDANA NA DIRA YA TAIFA

Dkt. Mwasse amesema, mafanikio yaliyopatikana yametokana na juhudi za Watanzania katika kubadilisha namna shirika linavyoendeshwa, akihusisha mageuzi hayo na falsafa ya 4Rs inayohimiza mageuzi, ujenzi upya, maridhiano na ustahimilivu.

Amesisitiza kuwa, taasisi za umma zina uwezo wa kuimarisha ufanisi, kushindana katika mazingira ya kibiashara na kuchangia mapato ya taifa iwapo zitasimamiwa kwa misingi ya uwajibikaji, ubunifu na mikakati endelevu.

Amesema, STAMICO inaendelea kujiandaa kutekeleza mipango yake kwa kuzingatia mwelekeo wa maendeleo ya taifa, hususan katika sekta ya madini, ambayo ina nafasi muhimu katika ukuaji wa uchumi na upanuzi wa viwanda.

Mkakati huo umepewa kaulimbiu ya “Make STAMICO Shine Again”, inayolenga kuifanya STAMICO kuwa shirika lenye nguvu zaidi katika uwekezaji wa madini, uzalishaji wa mapato na mchango wake kwa uchumi wa nchi.

TUZO ZAONGEZA TASWIRA YA SHIRIKA

Katika kuonesha mafanikio ya kiutendaji, STAMICO imeeleza pia kupata tuzo mbalimbali katika majukwaa ya kitaaluma na maonesho ya biashara.
Miongoni mwa mafanikio yaliyotajwa ni kushinda nafasi ya mshindi wa jumla katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu kama Sabasaba pamoja na tuzo nyingine zinazohusiana na utendaji wa kampuni na taasisi.

Dkt. Mwasse amesema, mafanikio hayo yanapinga mtazamo kwamba taasisi za umma haziwezi kushindana na kampuni binafsi katika mazingira ya biashara.

Amesema, uzoefu wa STAMICO unaonesha kuwa, taasisi za umma zinaweza kuboresha utendaji na kuimarisha ushindani iwapo zitaweka mkazo katika mageuzi ya ndani, uwekezaji na matumizi bora ya rasilimali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here