NA DIRAMAKINI
BRIGEDIA Jenerali David Msakulo amesisitiza ushirikiano kati ya wazazi na walimu katika malezi ya watoto wakati wa mahafali na uzinduzi wa mabweni Shule ya Innovate Mlandizi mkoani Pwani.
Ametoa kauli hiyo leo wakati wa mahafali ya wanafunzi wa darasa la awali katika Shule ya Innovate ambapo pia ameshiriki uzinduzi wa mabweni ya shule hiyo na zoezi la upandaji miti.
Amesema, malezi ya mtoto si jukumu la shule pekee, bali yanahitaji ushirikiano kati ya wazazi, walimu na walezi, hususani katika kufuatilia maendeleo ya kielimu, kitabia na kimaadili.
"Lazima kuwe na ushirikiano kati ya wazazi, walimu na walezi. Hatuwezi kuwaachia walimu jukumu lote la kulea watoto, kwa sababu ili tupate viongozi bora wa taifa, kila upande lazima utekeleze wajibu wake."
Aidha, Brigedia Msakulo ameshiriki kupanda mti kama sehemu ya kuhamasisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kutunza mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya Innovate, Gorge Ndaki amesema, shule hiyo hailengi kutoa elimu ya darasani pekee, bali kuwajengea wanafunzi uwezo wa kutumia maarifa wanayopata katika mazingira halisi.
Amesema, shule hiyo pia inaweka mkazo katika sayansi na teknolojia ili kuwaandaa wanafunzi kukabiliana na mahitaji ya dunia ya sasa.
Ndaki ameongeza kuwa, uzinduzi wa mabweni ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya kujifunzia na malezi ya wanafunzi, alisema mazingira bora yanachangia kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Tags
Brigedia David Msakulo
Habari
Habari za Mlandizi
Mahafali ya Asali Innovate
Malezi ya Watoto na Viongozi
Shule ya Innovate Mlandizi
Uzinduzi wa Mabweni Pwani




