NA ASYA HASSAN
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wanaume nchini kuungana na kutumia nafasi zao katika jamii kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia, mmomonyoko wa maadili na changamoto zinazowakabili vijana na familia.
Waziri wa Kazi, Ajira, Vijana na Uwezeshaji, Ali Suleiman Ameir ameyasema hayo Rahaleo wakati wa uzinduzi wa Umoja wa Wanaume Tanzania, akisisitiza kuwa wanaume wana wajibu mkubwa katika kujenga familia na jamii yenye amani, mshikamano na maendeleo.
Amesema, wanaume wanapaswa kutambua nafasi zao kama wazazi, walezi, viongozi na wasimamizi wa familia, hivyo wanatakiwa kutumia nafasi hizo kulinda ustawi wa familia na jamii badala ya kushiriki vitendo vinavyosababisha madhara.
Ameir amesema, wanaume wanapaswa kuwa mstari wa mbele kukemea ukatili dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo vipigo, unyanyasaji na kutelekeza familia, akiwataka kutokaa kimya wanaposhuhudia vitendo hivyo.
"Tunapomuona mwanamke anapigwa, anatendewa ukatili au kutelekezwa, tusikae kimya. Sisi wanaume tunapaswa kukemea vitendo hivyo na kuhakikisha jamii yetu inalindwa,”amesema.
Aidha, amewataka wanaume kushirikiana katika kupambana na umaskini na changamoto za kiuchumi kwa kushiriki kikamilifu katika uzalishaji, ajira, biashara na fursa nyingine za maendeleo ili kujenga familia zenye uwezo kiuchumi.
Amesema, vijana wa kiume wanahitaji kupewa nafasi na kuandaliwa vyema ili washiriki katika maendeleo, akibainisha kuwa baadhi yao wanakabiliwa na ukosefu wa ajira, kuacha masomo, matumizi ya dawa za kulevya na kukosa shughuli za kuwaingizia kipato.
Ameir pia amesisitiza umuhimu wa wanaume kuwajibika katika familia na kuwajali wazee, watoto na makundi mengine ya jamii, akisema maendeleo endelevu hayawezi kupatikana iwapo kundi lolote litaachwa nyuma.
Amesema, Umoja wa Wanaume haupaswi kuwa chombo cha kupambana na wanawake, bali jukwaa la ushirikiano kati ya wanawake na wanaume katika kutatua changamoto za familia, kupunguza ukatili na kujenga jamii yenye usawa, amani na maendeleo.
Amewataka viongozi wa umoja huo kufanya tafiti na kuandaa mipango ya utekelezaji itakayobainisha changamoto zinazowakabili wanaume na vijana wa kiume, pamoja na kutafuta suluhisho kwa kushirikiana na serikali na wadau wa maendeleo.
Ameir amesema, umoja huo unatakiwa kuwa “umoja wa kitendo, si umoja wa jina,” akiwataka wanachama kupanga, kutekeleza na kuwajibishana katika yale watakayokubaliana ili kujenga familia imara na jamii yenye maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanaume Tanzania, Claude Benedict Kimu amesema, umoja huo unalenga kuimarisha malezi na maadili, kuwawezesha wanaume kiuchumi, kuhamasisha afya na ustawi, kulinda amani na mshikamano pamoja na kuhakikisha wanaume wanatimiza wajibu wao katika familia na jamii.
Kimu amewataka wanaume kuamka na kuacha tabia ya kutelekeza familia, akiwahimiza kujitokeza kujiunga na umoja huo kwa lengo la kujenga familia imara na taifa lenye amani, mshikamano na maendeleo.
Amesema, jamii inahitaji wanaume wenye msimamo, ujasiri na uwezo wa kusimamia majukumu ya kifamilia, akisisitiza kuwa uimara wa familia una mchango mkubwa katika malezi bora ya watoto na ustawi wa jamii.
Akisoma risala ya umoja huo, Katibu John Sagata amewataka wanaume kuongeza usimamizi na malezi ya watoto wa kiume ili kuwajenga kuwa wanaume wenye maadili, uwajibikaji na uwezo wa kuwa baba bora katika familia na jamii.
Sagata amesema watoto wa kiume hawapaswi kulelewa bila uangalizi na mwongozo unaofaa tangu utotoni, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kujenga kizazi chenye maadili na kulinda mustakabali wa jamii na taifa.
Aidha, ameiomba serikali kuitambua rasmi taasisi hiyo na kuwashirikisha wanaume katika mipango na maamuzi mbalimbali ya maendeleo ya taifa, kwa lengo la kuimarisha familia na jamii.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Khatib Mwadini Khatib amesema, umoja huo unapaswa kuzingatia maadili mema katika malezi ya watoto na vijana, sambamba na kulinda mila na desturi za Kizanzibari.
Naibu Meya wa Jiji la Zanzibar, Khaitham Muhidin Khamis amesema, ushirikiano kati ya Umoja wa Wanaume na Umoja wa Wanawake ni muhimu katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana, hususan watoto wa kiume, na kuimarisha malezi yao.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mjini, Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Dkt. Said Haji Mrisho amesema, serikali itaendelea kuweka mazingira salama kwa wananchi na kuunga mkono mashirika yasiyo ya kiserikali yanayoshirikiana na serikali katika shughuli za maendeleo.
Umoja huo hadi sasa umeenea katika mikoa 28 ya Tanzania Bara na Zanzibar, ukiwa na zaidi ya wanachama 1,850, huku ukilenga kufika katika mikoa yote ifikapo Desemba mwaka huu.
Tags
Habari
Tanzania
Umoja wa Wanaume Tanzania
Unyanyasaji wa Kijinsia
Wanaume Mshikamane
Wanaume Tanzania
Wanaume Zanzibar
Zanzibar






















