PEMBA- Wanafunzi zaidi ya 310 wa Shule ya Sekondari Mtangani, iliyopo Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, watanufaika na ujenzi wa matundu 23 ya vyoo uliofadhiliwa na Serikali ya Canada kupitia Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), kwa ushirikiano na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
CPA Mwanahamis Chambega, Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi TEA akikagua maendeleo ya Ujenzi wa matundu 23 ya vyoo Shule ya Sekondari Mtangani Wilaya ya Mkoani Pemba.Mradi huo wenye thamani ya Sh milioni 144.8 unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, baada ya shule hiyo kukabiliwa na changamoto ya kutokuwa na vyoo, hali iliyowalazimu walimu na wanafunzi kutumia vyoo vya shule ya msingi iliyokuwa umbali wa takribani mita 150.
Akizungumza wakati wa ziara ya Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA CPA Mwanahamis Chambega, mwakilishi wa Msimamizi Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba Mohamed Hassan Ally alisema, ukosefu wa vyoo shuleni hapo ulikuwa ukiathiri mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, pamoja na kuhatarisha afya na usalama wa walimu na wanafunzi.
Alisema, changamoto hiyo pia ilikuwa ikichangia kushuka kwa maendeleo ya kitaaluma na kuongezeka kwa utoro miongoni mwa wanafunzi.
"Tunaishukuru sana TEA, Serikali ya Canada na UNICEF kwa kufanikisha mradi huu. Ujenzi wa vyoo hivi ni mkombozi kwa walimu na wanafunzi ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vyoo," alisema Ally.
Aliongeza kuwa, upatikanaji wa vyoo hivyo utasaidia kuboresha mazingira ya shule, kuongeza mahudhurio ya wanafunzi na kuimarisha maendeleo ya kitaaluma.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA CPA Mwanahamis Chambega alisema, ameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo akisisitiza kuwa umezingatia viwango vya ubora.
Aliwataka viongozi wa shule, walimu na wanafunzi kuhakikisha wanatunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu na kuwanufaisha hata vizazi vijavyo.
Katika ziara hiyo, Chambega pia alikagua miradi mingine ya uboreshaji miundombinu ya elimu inayotekelezwa na TEA Pemba ikiwamo, ujenzi wa Shule ya Amali ya Kangagani Wilaya ya Wete, pamoja na ukarabati wa maabara za sayansi katika Shule za Sekondari Piki na Kangani.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi Mamlaka ya Elimu Tanzania, CPA Mwanahamis Chambega akimsikiliza mkandarasi Ally Omary Khamis anayejenga matundu 23 ya vyoo Shule ya Sekondari Mtangani Wilaya ya Mkoani Pemba.
Muonekano wa Maabara ya Sayansi Shule ya Sekondari PIKI inayokarabatiwa kwa ufadhili wa UNICEF kwa kushirikiana na TEA wilaya ya Wete Pemba.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi TEA, CPA Mwanahamis Chambega akikagua ukarabati wa maabara ya Sayansi Shule ya Sekondari Kangani Wilaya ya Mkoani Pemba.
Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi TEA, CPA Mwanahamis Chambega akizungumza na baadhi ya viongozi wa Wizara ya Elimu Pemba, mara baada ya kukagua ukarabati wa maabara ya Sayansi Shule ya Sekondari Kangani Wilaya ya Mkoani.TEA imesaini makubaliano ya ushirikiano na UNICEF kwa ajili ya kutekeleza jumla ya miradi 20 ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu visiwani Zanzibar ambapo awamu ya kwanza inahusisha miradi 15 ambayo tayari imeanza kutekelezwa na ipo katika hatua mbalimbali za umaliziaji.
Miradi hiyo inalenga kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia hususan katika masomo ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia (STEM).
Tags
Elimu Zanzibar
Habari
Habari za Zanzibar
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA)
Shule ya Sekondari Mtangani
Ujenzi Vyoo Shule
UNICEF


