NA DIRAMAKINI
MKUU wa Wilaya ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam, Wakili Albert Msando amewaonya watu wanaowazuia au kuwakatisha tamaa wengine kujitokeza kutoa ushahidi kwa Tume ya Jaji Lila, akisisitiza kuwa kufanya hivyo kunawanyima wananchi haki yao ya kikatiba na kisheria.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, Wakili Albert Msando akizungumza leo kuhusu Tume ya Jaji Lila.Msando ametoa wito huo leo alipokuwa akizungumza ofisini kwake, akiwahimiza wakazi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kutoa maelezo, ushahidi na taarifa zao kwa tume hiyo.
Tume hiyo ipo Ubungo kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha takribani wiki moja au zaidi, kutegemea aina na wingi wa ushahidi utakaopokelewa.
Amesema, wananchi wanapaswa kuwa huru kutumia fursa hiyo kueleza wanachokifahamu au kuwasilisha malalamiko yao ili yaweze kusikilizwa na kufanyiwa kazi na tume.
“Ni haki ya kila mmoja wetu kufika mbele ya tume. Mtu anapotoa kauli zinazoweza kumzuia mwingine kutumia fursa hiyo, tunakuwa tunamnyima haki yake,” amesema Msando.
Aidha, amewataka viongozi wa dini, vyama vya siasa, taasisi na asasi za kiraia kusaidia kusambaza taarifa kuhusu uwepo wa tume hiyo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kushiriki katika mchakato huo.
Amesisitiza kuwa kila mwananchi anapaswa kuruhusiwa kutumia haki yake ya kikatiba na kisheria kuwasilisha ushahidi au malalamiko yake bila kuzuiwa na mtu mwingine.
Msando amesema Serikali ya Wilaya ya Ubungo imepokea kwa utayari ujio wa tume hiyo na kuwataka wananchi kutumia muda itakaokuwa katika eneo hilo kufikisha taarifa zao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.