Wanahabari wa Tanzania na Oman wafungua ukurasa mpya wa ushirikiano, waazimia mambo 11

NA GODFREY NNKO

WAHARIRI na waandishi wa habari kutoka Tanzania na Oman wamekubaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya habari kwa kuanzisha mifumo ya pamoja ya kubadilishana uzoefu, mafunzo, taarifa na maudhui, huku wakilenga kutumia historia na urithi wa pamoja kama msingi wa kukuza uhusiano katika uchumi, uwekezaji, utalii na maendeleo.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika kongamano la wanahabari wa Tanzania na Oman lililofanyika leo Oktoba 1,2026 jijini Dar es Salaam, huku likiwakutanisha wahariri na waandishi wa habari kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Chama Cha Wafanyakazi Waandishi wa Habari (JOWUTA) na Chama cha Wanahabari cha Oman (OJA).

Mkutano huo umewakutanisha wadau hao wa sekta ya habari kutoka nchi hizo mbili kujadili namna ambavyo uandishi wa habari unaweza kutumika kuimarisha uhusiano wa kihistoria na wa sasa kati ya Tanzania na Oman, pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano katika maeneo mbalimbali.

Baada ya majadiliano ya kina, washiriki wamepitisha maazimio 11 yanayolenga kuweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu na wenye utekelezaji kati ya taasisi za habari na wanahabari wa Tanzania na Oman. Miongoni mwao maazimio hayo ni;

Mfumo wa pamoja wa ushirikiano wa vyombo vya habari

Wanahabari hao wameazimia kuunda mfumo au mtandao wa kisheria na kitaalamu wa ushirikiano wa habari kati ya Tanzania na Oman, utakaounganisha Jukwaa la Wahariri Tanzania, Chama cha Wanahabari cha Oman pamoja na taasisi na vyama vingine vya wanahabari vya nchi hizo.

Mfumo huo unalenga kuweka mazingira rafiki ya kubadilishana uzoefu, taarifa na maudhui ya habari, huku ukiimarisha mawasiliano na mahusiano ya kitaaluma kati ya wanahabari wa pande zote mbili.

Mpango wa kila mwaka wa kubadilishana uzoefu na mafunzo

Pia, washiriki wamekubaliana kutekeleza mpango wa mwaka wa kubadilishana ujuzi na uzoefu kwa wanahabari na vyombo vya habari.

Mpango huo utahusisha ziara za kubadilishana uzoefu, programu za mafunzo na warsha za pamoja zitakazolenga kuongeza uwezo wa wanahabari katika maeneo mbalimbali ya taaluma.

Aidha, mpango huo unatarajiwa kusaidia kupunguza upotoshaji wa taarifa kuhusu misingi ya kihistoria, kitamaduni, kiuchumi na kitalii baina ya nchi hizo mbili.

Uzalishaji wa maudhui ya pamoja

Mkutano umeazimia pia kuandaa na kuzalisha maudhui ya pamoja ya kihistoria na kidiplomasia, pamoja na nyaraka zitakazohifadhi kumbukumbu za historia ya Oman katika Afrika Mashariki.

Maudhui hayo yataangazia kwa kina uhusiano wa Oman na Tanzania, hususan kupitia Zanzibar, pamoja na urithi wa baharini, utamaduni na mambo ya kibinadamu yanayowaunganisha wananchi wa pande hizo mbili.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha historia hiyo inafikishwa kwa kizazi cha sasa na kuhifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Tafiti za pamoja za kihistoria

Katika eneo la elimu na utafiti, washiriki wamekubaliana kuchochea tafiti za pamoja za kihistoria na za vyombo vya habari kati ya taasisi za kitaaluma na utafiti za Oman na Tanzania.

Utafiti huo unatarajiwa kusaidia kujenga uelewa mpana wa historia ya pamoja na kupunguza utegemezi wa simulizi zilizotawanyika, huku ukitoa marejeo ya pamoja yenye msingi wa kitaaluma na kisayansi.

Jukwaa la fursa za uwekezaji na utalii

Vilevile, mkutano huo umeazimia kuanzisha tovuti au jukwaa maalum la habari kuhusu fursa za uwekezaji na utalii katika nchi hizo mbili.

Jukwaa hilo litatoa taarifa kuhusu mazingira ya uwekezaji, vivutio, vichocheo na fursa zinazopatikana Tanzania na Oman.

Maudhui yanatarajiwa kutolewa kwa Kiarabu, Kiingereza na Kiswahili ili kufikia hadhira pana zaidi na kuwapa wawekezaji na watalii taarifa zinazohitajika kabla ya kufanya maamuzi.

Ushirikiano katika uandishi wa habari za utalii

Wahariri na wanahabari hao wamekubaliana kuongeza ushirikiano katika uandishi wa habari za utalii kupitia kampeni na uzalishaji wa maudhui ya pamoja yanayoangazia vivutio vya Tanzania na Oman.

Msisitizo utawekwa katika kukuza utalii wa kihistoria na kitamaduni, pamoja na urithi wa baharini unaounganisha jamii za nchi hizo mbili.

Njia za utalii wa kitamaduni na kihistoria

Mkutano huo, pia umeazimia kuendeleza njia za utalii wa kitamaduni na kihistoria zitakazobainisha maeneo yenye uhusiano na historia ya Oman katika Afrika Mashariki.

Lengo ni kugeuza urithi huo wa pamoja kuwa bidhaa endelevu ya utalii na utamaduni itakayoweza kuvutia watalii, watafiti na wadau wengine, huku ikitoa fursa za kiuchumi kwa jamii zinazohusika.

Sekta binafsi kuhusishwa

Washiriki pia, wamependekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya taasisi za utalii, vyombo vya habari na sekta binafsi katika nchi zote mbili.

Ushirikiano huo utalenga kuandaa mipango ya pamoja ya kukuza utalii na uwekezaji, kutangaza fursa zilizopo na kuvutia wageni pamoja na wawekezaji.

Hatua hiyo inalenga kutumia nguvu ya vyombo vya habari katika kutangaza fursa za kiuchumi na kitalii kwa hadhira pana zaidi.

Mtandao wa mawasiliano ya haraka

Mkutano umeazimia pia kuanzisha mtandao wa mawasiliano kati ya wanahabari na vyombo vya habari vya Tanzania na Oman.

Mtandao huo utarahisisha kubadilishana habari, ripoti, picha na maudhui mengine, pamoja na kurahisisha ushirikiano katika masuala yenye maslahi ya pamoja.

Diplomasia ya vyombo vya habari

Washiriki wamekubaliana kutumia diplomasia ya vyombo vya habari, habari na utamaduni kama nyenzo ya kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman.

Kwa mujibu wa maazimio hayo, vyombo vya habari vinaweza kusaidia kujenga uelewa mpana wa uhusiano wa nchi hizo mbili na kuonesha namna historia na urithi wa pamoja unavyoweza kutumika kama msingi wa malengo ya maendeleo ya kisasa.

Hatua hiyo pia inalenga kuimarisha uhusiano wa watu kwa watu na kujenga uelewa wa pamoja kupitia taarifa na maudhui yanayozingatia usahihi na muktadha.

Timu ya pamoja ya ufuatiliaji

Ili kuhakikisha maazimio hayo yanatekelezwa, mkutano umeazimia kuunda timu ya pamoja ya ufuatiliaji itakayojumuisha wawakilishi kutoka vyombo vya habari na wanahabari wa nchi hizo mbili.

Timu hiyo itakuwa na jukumu la kuweka ratiba ya utekelezaji, kufuatilia hatua zinazochukuliwa na kupima matokeo ya shughuli zitakazotekelezwa kwa mujibu wa makubaliano.

Hatua hiyo inalenga kuzuia maazimio hayo kubaki kwenye nyaraka pekee na badala yake kuhakikisha yanageuzwa kuwa shughuli zinazoonekana na zenye manufaa kwa sekta ya habari na jamii kwa ujumla.

Mbali na hayo, washiriki wamethibitisha kuwa vyombo vya habari na uandishi wa habari vinaweza kuwa washirika wa kimkakati katika kuendeleza uhusiano wa Tanzania na Oman.

Wamesema, urithi wa kihistoria na kitamaduni wa pamoja unaweza kutumika kama jukwaa la kujenga ushirikiano wa kisasa katika maeneo ya uchumi, uwekezaji, utalii na maendeleo.

Maazimio hayo yameweka msisitizo kwamba kalamu, kamera na teknolojia za kisasa za habari zinaweza kuwa madaraja ya kuunganisha watu, taasisi na fursa za nchi hizo mbili, huku zikisaidia kuhifadhi urithi wa pamoja na kuufanya kuwa chachu ya maendeleo ya kisasa.

Kongamano hilo ambalo limefunguliwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Abdallah Kilima, pia limewaleta pamoja baadhi ya wanadiplomasia na viongozi wa Serikali.

Balozi Kilimo amewataka wanahabari wa Tanzania na Oman kutumia nafasi waliyonayo kuandika na kusambaza taarifa sahihi, za kina na zenye kuelimisha umma kuhusu historia, utamaduni na fursa zilizopo katika uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Naye Balozi wa Usultani wa Oman katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Saudi bin Hilal Al-Shidhan amesema, kuimarishwa kwa ushirikiano katika sekta ya habari na utamaduni kunatoa fursa muhimu ya kuwakutanisha wadau wa nchi hizo mbili, kubadilishana uzoefu na kuendeleza uhusiano uliopo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari wa Oman (OJA), Dkt. Mohamed bin Mubarak Al Araimi amesema, uhusiano kati ya Oman na Tanzania hauishii katika historia ya kidiplomasia pekee, bali umejengwa kwa misingi ya watu, utamaduni, lugha na kumbukumbu za pamoja zilizodumu kwa karne nyingi.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw.Deodatus Balile amesema, mkutano huo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kiutamaduni kati ya Tanzania na Oman kupitia sekta ya habari.

Bw.Balile amesema, ushirikiano huo unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha weledi, umakini na ufanisi wa vyombo vya habari, hususan katika kipindi ambacho sekta hiyo inakabiliwa na mabadiliko makubwa yanayotokana na teknolojia na maendeleo ya kidijitali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here