Wananchi Ubungo wahamasishana kutoa ushahidi mbele ya Tume ya Jaji Lila

NA DIRAMAKINI

WANANCHI wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam wamewahimiza wenzao kujitokeza kwa wingi kutoa ushahidi na kueleza maoni yao mbele ya Tume ya Uchunguzi wa Vurugu na Uvunjifu wa Amani zilizotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakieleza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kubaini changamoto zilizojitokeza na kuweka msingi wa kuzuia matukio kama hayo kujirudia.
Mwanakombo Kijazi, mkazi wa Wilaya ya Ubungo.

Wito huo wameutoa leo Oktoba 14, 2026 kwa nyakati tofauti wakati tume hiyo, inayoongozwa na Mwenyekiti wake, Jaji mstaafu Shaban Lila ikiendelea na shughuli za ukusanyaji wa taarifa na ushahidi katika Wilaya ya Ubungo kupitia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.

Tume hiyo imepanga kufanya kazi katika eneo hilo kwa muda wa siku kadhaa kuanzia Oktoba 11 hadi 16, 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusikiliza maoni, malalamiko na maelezo ya wananchi kuhusu matukio yaliyotokea katika kipindi cha uchaguzi uliopita.

Aidha, tayari tume imeshasikiliza wananchi wa Wilaya ya Ilala, Kigamboni na Temeke na sasa ni zamu ya Ubungo kabla ya kuelekea maeneo mengine.

Wananchi waliozungumza wameeleza kuwa, ni muhimu kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ya Ubungo wakiwamo vijana, wazee na makundi mengine ya jamii, kutumia fursa hiyo kueleza kile wanachokifahamu kuhusu matukio hayo ili kusaidia tume kupata taarifa zinazoweza kufanyiwa uchambuzi.

Mwanakombo Kijazi, mkazi wa Wilaya ya Ubungo amewahimiza wananchi wenye taarifa kuhusu vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi kujitokeza na kuziwasilisha kwa tume, akisema ni muhimu kila mwenye maelezo au malalamiko yanayohusiana na matukio hayo kupata nafasi ya kuyafikisha kwa wahusika.
Bonaventura Ansokolo, mkazi wa Msewe Ubungo.

“Nawahamasisha wananchi wenzangu wa Ubungo, vijana na wazee, kujitokeza kwa wingi mbele ya Tume ya Jaji Lila. Kama kuna mtu mwenye taarifa kuhusu vurugu zilizotokea wakati wa uchaguzi au changamoto alizozishuhudia, atumie fursa hii kueleza alichokiona ili kiweze kufanyiwa kazi,” amesema Kijazi.

Amesema, uwepo wa tume hiyo katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo unatoa nafasi kwa wananchi kuwasilisha taarifa na kueleza kero zao zinazohusiana na matukio yanayochunguzwa.

Kwa upande wake, Bonaventura Ansokolo, mkazi wa Msewe amewataka wananchi kujitokeza na kueleza madhara na changamoto walizozishuhudia au kuzipata kutokana na matukio ya uchaguzi wa mwaka 2025.

Ansokolo amesema, matukio yaliyotokea katika kipindi hicho yamempa msukumo wa kuwataka wananchi kushiriki katika mchakato wa uchunguzi, akisisitiza kuwa ni muhimu kuyajadili na kuyafanyia kazi kwa lengo la kuimarisha amani na upendo miongoni mwa Watanzania.

Amesema, ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa unaweza kusaidia kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mazingira bora ya kuzuia kujirudia kwa matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.

“Ni vyema wananchi tukajitokeza kwa wingi kueleza madhara na changamoto zilizotokana na matukio ya mwaka uliopita, ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa na hali kama hiyo isijirudie katika nchi yetu. Tunapaswa kudumisha amani na upendo,” amesema Ansokolo.
Juma Chavala mkazi wa Stopover Ubungo.

Naye Juma Chavala mkazi wa Stopover ametoa wito kwa wakazi wa Ubungo kushirikiana na tume hiyo kwa kuwasilisha taarifa na madukuduku yao, akieleza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kusaidia uchunguzi kufikia malengo yake.

Chavala amesema, anaamini kuwa maoni na ushahidi wa wananchi unaweza kusaidia Tume kupata uelewa mpana kuhusu matukio yaliyojitokeza na changamoto zilizohitaji kushughulikiwa.

Ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kutumia nafasi hiyo kwa uwajibikaji na kutoa maelezo wanayoyafahamu, ili uchunguzi uweze kuzingatia taarifa zinazotolewa na watu wenye uzoefu au ufahamu wa matukio hayo.

“Mimi kama mkazi wa Ubungo, nawaomba wananchi wenzangu tutoe taarifa na kero zetu ili kuisaidia Tume hii kufanyia kazi madukuduku yetu. Ni muhimu vijana na wazee tushirikiane katika mchakato huu kwa manufaa ya nchi yetu,” amesema Chavala.
Aika Raymond Manyanga mkazi wa Kibamba.

Kwa upande wake, Aika Raymond Manyanga mkazi wa Kibamba amewahimiza wananchi wa Ubungo kuunga mkono kazi ya Tume iliyoteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuchunguza matukio yaliyotokea katika kipindi cha uchaguzi, akisema lengo ni kusaidia kujenga mazingira ya amani na utulivu nchini.

Manyanga amesema, ushiriki wa wananchi ni sehemu muhimu ya mchakato wa uchunguzi, kwani unaweza kuwezesha maelezo kuhusu matukio yaliyotokea kufikishwa kwa Tume kwa ajili ya kuchunguzwa.

Wito wa wananchi hao unaangazia umuhimu wa ushiriki wa jamii katika mchakato wa uchunguzi wa matukio yanayohusu usalama na amani, huku wakisisitiza haja ya kutoa taarifa kwa uwazi na kwa kuzingatia ukweli wa kile mtu alichokiona, kukisikia au kukifahamu.

Vilevile, wamesisitiza kuwa, amani na utulivu ni misingi muhimu kwa maendeleo ya nchi, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika juhudi za kulinda usalama wa watu na mali zao, kuheshimu taratibu zinazotumika katika mchakato wa uchunguzi na kuchangia katika kujenga mazingira ambayo tofauti za maoni zinaweza kushughulikiwa kwa njia za amani.Barabara ya Juu ya John Kijazi wilayani Ubungo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here