Waziri Kikwete aagiza Usiri wa Taarifa za Watumishi kulindwa

NA VERONICA MWAFISI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amefungua kikao kazi cha Maafisa Rasilimaliwatu na Maafisa Sheria jijini Tanga na kutoa maelekezo mahususi katika kulinda ustawi wa Utumishi wa Umma na taifa kwa ujumla.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati akifungua kikao kazi cha Maafisa Sheria na Maafisa Rasilimaliwatu kilicholenga kutambua changamoto za utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na Kanuni zake kilichofanyika leo tarehe 06 Oktoba, 2026 jijini Tanga.

Akifungua kikao kazi hicho leo Oktoba 6, 2026, Mhe. Kikwete amesema, katika siku za karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya Mamlaka za Nidhamu kutoa taarifa za mashauri ya kinidhamu kwenye vyombo vya habari kinyume na Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma.

Kufuatia tabia hiyo, Mhe. Kikwete amezielekeza Mamlaka zote za nidhamu katika Taasisi kuzingatia usiri wa taarifa binafsi za watumishi wakati wa kujadili ajenda za mashauri ya kinidhamu.
Amesema, pia katika mchakato wa kushughulikia masuala ya nidhamu, kama ilivyoelekezwa katika Sheria na Kanuni, watu wote ambao hawatokuwa wanahusika katika mchakato wa uendeshaji wa mashauri ya nidhamu hawatapaswa kuwepo wala kujua kile kilichoendelea katika ushughulikiwaji wa shauri hilo.

Vilevile, amesema, mamlaka za nidhamu hazipaswi kutangaza maamuzi ya mashauri ya nidhamu katika vyombo vya habari kama inavyojitokeza mara kwa mara katika baadhi ya Halmashauri na badala yake zinapaswa kufuata utaratibu ulioainishwa katika Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma kupitia Kanuni D. 28 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma Toleo la mwaka 2009.
“Ninatambua kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI tayari wameshatoa maelekezo kupitia barua. Na mimi kama Msimamizi wa Utumishi wa Umma kupitia hadhara hii nimetoa melekezo yangu, ni mategemeo yangu kwamba maelekezo haya yatatekelezwa ipasavyo na tutaendelea kulinda hadhi na heshima ya Utumishi wa Umma,” ameongeza.

Amewataka Maafisa Utumishi hao kuwa wabunifu katika kutatua changamoto za Watumishi wa Umma, akisisitiza pamoja na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo lakini busara pia itumike, wakiona wanashindwa kufanya hivyo ni vema wakawasiliana na Ofisi ya Rais-UTUMISHI kuona namna ya kufanya.

Amesema, Serikali inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 imeweka wazi malengo yake kuhakikisha mazingira ya Utumishi yanakuwa bora kupitia kaulimbiu ya “KAZI NA UTU.” “Mtoe haki kwa wakati ili kuwapatia ari Watumishi wa Umma kufanya kazi,” ameongeza.

Aidha, ameendelea kuhimiza matumizi ya kidijitali katika Utumishi wa Umma. “Serikali tumefanikiwa sana, naendelea kuwashukuru wataalamu wa e-GA na Maafisa TEHAMA sasa hivi hakuna kukutana kutana.”
Katika hatua nyingine Mhe. Kikwete amesisitiza utoaji huduma unaozingatia wananchi katika maeneo makuu manne ambayo ni upatikanaji (accessibility), uitikivu (responsiveness), uwazi (transparency) na uwajibikaji (accountability) katika utoaji huduma.

Amesema,katika upatikanaji wa huduma, Serikali inalenga kuhakikisha Taasisi za umma zinasikiliza maoni na kurekebisha taratibu zao ili kutatua changamoto halisi kwa haraka, kutoa taarifa kwa uwazi ili wananchi waelewe jinsi maamuzi yanavyofanywa na jinsi rasilimali za umma zinavyotumika na Watumishi wa umma wanapaswa kuwajibika kwa wananchi.

“Hii yote ni kuhakikisha kuwa kuna ushirikiano mkubwa kati ya Mtoa huduma ambaye ni Mtumishi wa Umma na Mpokea huduma ambaye ni Mwananchi.

“Mhe. Rais anataka sisi watoa huduma tuwe karibu na wananchi, tunahitaji utulivu na uadilifu katika kutatua kero za wananchi. Mtumishi wa Umma anatakiwa kuwa na nyaraka muhimu katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo Katiba ya Nchi, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Ilani ya Chama cha Mapinduzi."

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu –UTUMISHI, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI kama msimamizi na mtunzaji Mkuu wa Sheria ya Utumishi wa Umma, imekuwa na jukumu la kukutana ili kukumbushana Taratibu na Sheria kwa lengo la kuwekana sawa katika uzingatiwaji wa Sheria.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Hilda Kabisa amesema jumla ya watumishi 218 kutoka Sekretarieti za Mikoa, Taasisi za Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa wamealikwa kushiriki kikao kazi hicho.
Mada mbalimbali zimewasilishwa katika kikao kazi hicho ikiwemo Usimamizi wa Maadili na Malalamiko katika Utumishi wa Umma, Ushughulikiaji wa Mashauri ya Nidhamu katika Utumishi wa Umma, Ushughulikiaji wa Malimbikizo ya Mishahara kwa Watumishi wa Umma waliopandishwa vyeo, waliofukuzwa kazi na kurejeshwa katika Utumishi wa Umma na Mamlaka za Rufaa, Ushughulikiaji na Ulipaji wa Mafao kwa Watumishi wa Umma baada ya kustaafu, Ushughulikiaji wa Uhamisho, Upandishwaji Vyeo na Ubadilishwaji Kada katika Utumishi wa Umma.

Kikao kazi hicho kimelenga kubaini na kutambua changamoto za Utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298 na Kanuni zake za mwaka 2022. Na kinawashirikisha Maafisa Rasilimaliwatu na Wanasheria kufanya kazi kwa pamoja ili kuimarisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Watumishi wa Umma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here