DAR ES SALAAM- Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye pia ni Msarifu wa Benjamin William Mkapa Foundation (BMF), Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa wito kwa Serikali, washirika wa maendeleo na sekta binafsi kuimarisha ushirikiano na vyanzo endelevu vya ufadhili ili kuboresha huduma za afya na kuhakikisha zinawafikia wananchi kwa ufanisi.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo Novemba 12, 2026 katika Mkutano wa Mwaka wa Msarifu na Washirika wa BMF uliofanyika Hoteli ya Serena, Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa kulinda urithi wa Hayati Rais Benjamin William Mkapa na kuendeleza mifumo imara ya afya.
Katika mkutano huo, Rais Dkt. Mwinyi ameshuhudia utiaji saini wa makubaliano manne ya ushirikiano kati ya BMF na wadau mbalimbali, yakiwemo Wizara ya Afya Zanzibar, Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar, Benki ya NBC na Clouds Media Group, kwa lengo la kuimarisha huduma za afya, rasilimali watu na huduma za kidijitali.
Ameipongeza BMF kwa kutimiza miaka 20 ya mchango wake katika sekta ya afya, huku akiwataka wadau kuendelea kuiunga mkono ili kuongeza tija na kuimarisha huduma za afya nchini na katika ukanda wa Afrika.
Tags
Benjamin William Mkapa Foundation (BMF)
Dkt. Hussein Ali Mwinyi
Habari
Huduma za Afya
Ufadhili Sekta ya Afya
























