Sera ya Fedha ya BoT yachochea upatikanaji mikopo nafuu, uwekezaji na uzalishaji nchini

NA GODFREY NNKO

SERA ya viwango vya riba inayotekelezwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ina mchango mkubwa katika kuelekeza mwenendo wa riba zinazotozwa na benki za biashara, gharama za mikopo na upatikanaji wa mitaji kwa wananchi na wafanyabiashara.
Kupitia kiwango cha riba cha Benki Kuu (Central Bank Rate- CBR), taasisi hiyo huelekeza utekelezaji wa sera ya fedha kwa kusimamia ukwasi katika mfumo wa benki na kuathiri viwango vya riba katika soko la fedha, hatua inayosaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi nchini.

Akifafanua kuhusu utekelezaji wa mfumo huo, Meneja Msaidizi wa Idara ya Sera ya Fedha ya BoT, Bw. John Mero amesema, kiwango cha riba katika soko la mikopo ya siku saba baina ya benki (Seven-Day Interbank Rate) ni kiungo muhimu katika kusambaza athari za mabadiliko ya CBR kwa taasisi za fedha.

Bw. Mero ameeleza hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa sera ya fedha kwa kutumia kiwango cha riba cha Benki Kuu, katika siku ya kwanza ya semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari.

Amesema, CBR hutumika kama kiashiria kikuu cha mwelekeo wa sera ya fedha, huku kiwango cha riba cha siku saba katika soko la mikopo baina ya benki kikionesha namna maamuzi ya Benki Kuu yanavyoathiri viwango vya riba za muda mfupi.

Pia, amefafanua kuwa soko hilo huwezesha benki za biashara kukopeshana fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ukwasi wa muda mfupi. Hivyo, mabadiliko ya viwango vya riba katika soko hilo huonesha hali ya upatikanaji wa fedha ndani ya mfumo wa benki.

Bw. Mero amesema, BoT hutumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha kuhakikisha kiwango hicho kinabaki ndani ya wigo unaozunguka CBR ili kuratibu ukwasi na kuhakikisha maamuzi ya kisera yanafikia malengo yaliyokusudiwa.

Amesema, Benki Kuu inapoongeza CBR, gharama za upatikanaji wa fedha kwa benki huongezeka, hali inayoweza kuchochea benki za biashara kurekebisha viwango vya riba wanavyotoza wateja wanaokopa.

Hatua hiyo husaidia kudhibiti kasi ya mahitaji ya mikopo na matumizi katika uchumi, hivyo kuchangia usimamizi wa mfumuko wa bei na kuimarisha utulivu wa uchumi.
Kwa upande mwingine, kupunguza kiwango hicho kunaweza kupunguza gharama za upatikanaji wa fedha kwa benki za biashara, na hivyo kuweka mazingira yanayoweza kuchochea utoaji wa mikopo kwa ajili ya uwekezaji, uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi.

Hata hivyo, Bw. Mero amebainisha kuwa, viwango vya riba vinavyotozwa na benki za biashara huamuliwa kwa kuzingatia mambo mbalimbali yakiwemo gharama za amana za wateja, kiwango cha hatari ya wakopaji, mikopo isiyorejeshwa kwa wakati pamoja na gharama za uendeshaji.

Amesema, kutokana na vigezo hivyo, mabadiliko ya CBR hayaathiri moja kwa moja viwango vyote vya riba kwa kiwango na kasi inayofanana, kwa kuwa kila taasisi huzingatia mazingira yake ya kibiashara na tathmini ya hatari kabla ya kupanga gharama za mikopo.

Katika kuonesha mwenendo wa shughuli za kifedha nchini, takwimu zilizowasilishwa na Bw. Mero zimeonesha kuwa, mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa asilimia 33.4 Septemba 2026, huku ujazi mpana wa fedha ukiongezeka kwa takribani asilimia 25.7.

Ukuaji huo unaonesha kuimarika kwa shughuli za utoaji wa mikopo na ongezeko la ukwasi katika uchumi, mambo yanayochangia kupanuka kwa fursa za uwekezaji na uzalishaji katika sekta mbalimbali.

Vilevile, katika kuimarisha zaidi mazingira ya upatikanaji wa mikopo, BoT inaendelea kuchukua hatua za kupanua wigo wa dhamana zinazokubalika, kuboresha mifumo ya taarifa za wakopaji na kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha.

Aidha, Benki Kuu inaendeleza elimu ya fedha na matumizi ya huduma za kidijitali, pamoja na mfumo wa kulinganisha bei za huduma za kifedha unaowawezesha wateja kupata taarifa kuhusu viwango vya riba na gharama nyingine zinazotozwa na taasisi mbalimbali.

Bw. Mero amesema, upatikanaji wa taarifa sahihi na uelewa wa kutosha kuhusu huduma za kifedha ni muhimu katika kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wanapohitaji mikopo, huku ukichochea ushindani na uwazi katika utoaji wa huduma hizo.

Ameeleza kuwa, Tanzania ilianza kutekeleza mfumo wa sera ya fedha unaozingatia viwango vya riba ya Benki Kuu kuanzia Januari 2024, baada ya kuachana na mfumo wa awali uliotegemea usimamizi wa ujazi wa fedha.
Mabadiliko hayo yalilenga kuboresha namna maamuzi ya Benki Kuu yanavyosambaa katika mfumo wa fedha na uchumi kwa ujumla, pamoja na kuweka wazi zaidi mwelekeo wa sera ya fedha.

Aidha, mageuzi hayo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha ufanisi wa soko la fedha, kuboresha upatikanaji wa mikopo na kuweka mazingira yanayochochea uwekezaji, uzalishaji na ukuaji wa biashara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here