Serikali yaendelea kuimarisha uratibu wa maandalizi ya AFCON 2027

Na DIRAMAKINI 24| Dar es Salaam

SERIKALI imeendelea kuimarisha uratibu wa maandalizi ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, kwa kuzikutanisha Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ili kutathmini maendeleo ya maandalizi na kuweka mikakati ya kukamilisha utekelezaji wa majukumu yaliyobaki kwa wakati.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 16, 2026 jijini Dar es Salaam katika kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali, kilichoongozwa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Dkt. Jim Yonazi.
Kikao hicho kililenga kupitia na kutathmini hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya mashindano hayo, hususan utekelezaji wa miradi ya miundombinu, upatikanaji na matumizi ya bajeti, uratibu wa shughuli za kisekta pamoja.

AFCON 2027 itaandaliwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Kenya na Uganda. Kwa upande wa Tanzania, mashindano hayo yatafanyika katika vituo vya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar, hatua inayotarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi, kukuza sekta ya utalii na kuitangaza nchi kimataifa.
Katika kuhakikisha maandalizi yanakamilika kwa wakati, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara na Taasisi nyingine zinazohusika, inaendelea kuratibu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati. Miradi hiyo inajumuisha ujenzi na ukarabati wa viwanja vya mashindano, viwanja vya mazoezi, barabara na miundombinu mingine wezeshi itakayosaidia kufanikisha mashindano hayo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here