TPLB yatoa adhabu kali, Stand United, Prisons na maafisa waandamizi wakumbwa na faini, vifungo

Na DIRAMAKINI 24| Dar es Salaam

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu, wachezaji, makocha na mwamuzi kutokana na makosa ya kinidhamu yaliyojitokeza katika michezo ya Ligi ya Championship na First League, ikiwamo vurugu, kuchelewesha mchezo na ukiukwaji wa sheria za soka.
Katika maamuzi hayo yaliyotolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi baada ya kikao chake cha Novemba 19, 2026, klabu ya Tanzania Prisons imepigwa faini ya Sh milioni tano, huku Stand United ikitozwa Sh milioni moja kutokana na makosa yaliyofanywa na wahusika wake wakati wa michezo husika.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano ya TPLB, Stand United imeadhibiwa kufuatia mashabiki wake kuwafanyia fujo waamuzi wakati wa mapumziko ya mchezo dhidi ya KenGold uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Mashabiki hao walionesha kutoridhishwa na uamuzi wa waamuzi kukataa bao lililofungwa na timu yao.

Hata hivyo, hali hiyo ilidhibitiwa baada ya muda mfupi. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 47:61 ya Ligi ya Championship inayohusu udhibiti kwa klabu.

Katika mchezo mwingine wa Championship uliowakutanisha Bandari Tanzania na Kigamboni United, ambao Bandari ilishinda kwa bao 1-0, mwamuzi wa kati Florentina Zabron kutoka Dodoma ameondolewa katika orodha ya waamuzi kwa kipindi cha miezi sita.

Hatua hiyo imechukuliwa baada ya kubainika kuwa alionyesha mapungufu katika uamuzi na usimamizi wa mchezo kutokana na kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za soka. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 42:1(1.8) ya Ligi ya Championship.

Aidha, Tanzania Prisons imekumbwa na faini ya Sh milioni tano baada ya vijana wake waokota mipira (Ball Boys) kubainika kuchelewesha kwa makusudi kurejesha mipira uwanjani kila ilipotoka nje wakati wa mchezo dhidi ya KMC, ambao Prisons ilishinda kwa bao 1-0.

Licha ya mwamuzi kuwaonya mara kadhaa, vijana hao waliendelea na mwenendo huo, hali iliyosababisha klabu hiyo kuwajibishwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:61 inayohusu taratibu za mchezo.

Katika Ligi ya First League, TPLB imefuta adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa kocha wa Barberian FC, Salim Hamisi, wakati wa mchezo dhidi ya Magnet FC uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0 kwa Magnet.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya Kamati kupitia taarifa za wasimamizi wa mchezo na kujiridhisha kuwa kocha huyo hakustahili kuonyeshwa kadi hiyo. Hatua hiyo imezingatia Kanuni ya 12:7 ya Ligi ya First League kuhusu usimamizi wa ligi.

Wakati huohuo, wachezaji Kasto Lucas wa Hausung FC na Joseph Mkoga wa Dar City wamefungiwa michezo mitatu kila mmoja na kutozwa faini ya Sh 500,000 baada ya kuhusika katika tukio la kupigana mara baada ya mchezo kati ya timu zao kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Adhabu hizo zimetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 41:5 ya Ligi ya First League inayohusu udhibiti kwa wachezaji.

Katika tukio hilo hilo, kocha msaidizi wa Dar City, Rajabu Lugembe, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh milioni moja kwa kosa la kumshambulia mwamuzi, kitendo kilichochangia kuzuka kwa vurugu na kusababisha wachezaji wa timu hizo kupigana baada ya mchezo.

Lugembe ameadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) inayohusu udhibiti kwa makocha na maofisa wengine wa ufundi.

Vilevile, kocha msaidizi wa Pan African, Emmanuel Gabriel, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh milioni moja baada ya kupatikana na hatia ya kutumia lugha chafu na za vitisho dhidi ya klabu ya Magnet FC katika mchezo uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0 kwa Magnet.

Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 45:2(2.1) ya Ligi ya First League.

Maamuzi hayo yanaendelea kusisitiza msimamo wa TPLB katika kusimamia nidhamu, uwajibikaji na uzingatiaji wa kanuni za mashindano ili kulinda hadhi na uadilifu wa soka la Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here