OSLO, NORWAY- Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameshiriki ufunguzi wa Jukwaa la Biashara la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Nordic na Afrika (Nordic–African Foreign Ministers’ Business Forum), lililofanyika jijini Oslo, Norway Novemba 19, 2026.
Jukwaa hilo limezileta pamoja nchi 30 za Afrika na nchi za Nordic kujadili mbinu za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kuchochea uwekezaji na kufungua fursa mpya za biashara kati ya nchi za Afrika na Nordic.Viongozi wa Serikali, wawekezaji, wajasiriamali na wadau wa sekta binafsi wamekutana kujadili namna ya kubadilisha fursa za kiuchumi zilizopo barani Afrika kuwa miradi yenye tija, inayozalisha ajira na kuchangia maendeleo endelevu.
Ushiriki wa Tanzania unaendana na azma ya nchi ya kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kuvutia mitaji, teknolojia na ubia wa kimkakati utakaosaidia kuongeza uzalishaji, kukuza biashara na kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.Mkutano wa nchi za Nordic na Afrika umeanza rasmi leo na utafanyika kwa siku mbili (Novemba 19 na 20) huku kaulimbiu ya Mkutano wa mwaka huu ikiwa ni “Dialogue in an Era of Uncertainty. United for a Prosperous Future,” (Mjadiliano katika Zama za Kutokuwa na Hakika. Muungano kwa kesho yenye Ustawi).
Kwa Tanzania, majadiliano hayo yana umuhimu katika kufungua fursa za uwekezaji kwenye sekta za kimkakati zikiwemo nishati, miundombinu, kilimo, viwanda, madini na teknolojia.
Kupitia majadiliano hayo, nchi za Afrika na Nordic zinatafuta namna ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiteknolojia, kuongeza thamani ya rasilimali zinazozalishwa Afrika na kujenga viwanda vinavyoweza kushindana kimataifa.
Ushiriki wa Tanzania ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na nchi za Nordic, huku msisitizo ukiwekwa katika kugeuza mahusiano ya kidiplomasia kuwa fursa halisi za biashara, uwekezaji, ajira na maendeleo kwa Watanzania.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe, ambaye pia ni Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Mhe. Amon Murwira ametoa wito wa kuondokana na utegemezi wa misaada ya maendeleo na kuelekea katika mfumo wa kutegemeana kwa manufaa ya pande zote.
Pia, amesisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya rasilimali za asili ndani ya Afrika, kuharakisha maendeleo ya viwanda, kuwezesha uhawilishaji wa teknolojia na kupanua biashara ya kimataifa.
Nchi 30 za Afrika ambazo zimeungana na nchi tano za Nordic katika ufunguzi huo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Ghana, Nigeria, Afrika Kusini, Angola, Benin, Botswana, Côte d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Misri, Eritrea, Liberia, Libya, Malawi, Morocco, Msumbiji, Namibia, Senegal, Sierra Leone, Somalia, Sudan Kusini, Togo, Tunisia, Zambia na Zimbabwe.







