PARIS- Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amewasili Paris nchini Ufaransa, akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Jukwaa la 25 la Kimataifa la Uchumi Afrika linalotarajiwa kufanyika tarehe 25 Novemba 2026 katika Kituo cha Mikutano cha OECD, mjini Paris, Ufaransa.
Mheshimiwa Balozi Omar amepokelewa na Mwenyeji wake, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Said Othman Yakubu na kufanya kikao cha kupitia agenda kwa ajili ya maandalizi ya ushiriki wa Jukwaa hilo.
Jukwaa hilo linaandaliwa chini ya kaulimbiu “Kufadhili Mabadiliko ya Kiuchumi ya Afrika”, na linakusanya watunga sera, washirika wa maendeleo, taasisi za ufadhili wa maendeleo, wawekezaji na wadau wengine mbalimbali kujadili mabadiliko ya kiuchumi ya Bara la Afrika na vipaumbele vya ufadhili wa maendeleo.
Mheshimiwa Balozi Omar amealikwa kushiriki kaama mwajopo (panelist) katika Panel ya kwanza yenye kichwa “Kuelekea Upatikanaji wa Deni la Gharama Nafuu na Endelevu kwa Afrika katika Nyakati za Migogoro ya Kimataifa”.
Panel hiyo itajadili namna nchi za Afrika zinavyoweza kusawazisha gharama na vihatarishi vya deni la kitaifa na mahitaji ya ufadhili kwa ajili ya mabadiliko ya kiuchumi, pamoja na nafasi ya washirika wa kimataifa katika kuwezesha upatikanaji wa ufadhili kwa masharti bora zaidi.
Aidha, Jukwaa hilo litajadili changamoto zinazowakabili nchi za Afrika katika kukusanya ufadhili wa maendeleo wakati huu ambapo masharti ya ufadhili yanazidi kuwa magumu, mzigo wa kulipa madeni unaongezeka na nafasi ya kibajeti imepungua.
Majadiliano yatalenga mbinu za kupata ufadhili wa gharama nafuu na endelevu, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, na kutafuta suluhisho la ufadhili zitakazosaidia mabadiliko ya kiuchumi.
Jukwaa hilo pia litashuhudia uzinduzi wa ripoti ya Africa’s Development Dynamics 2026: Managing Debt for Transformation (“Mienendo ya Maendeleo ya Afrika 2026: Kusimamia Deni kwa Mabadiliko”), iliyoandaliwa kwa pamoja na Kituo cha Maendeleo cha OECD na Tume ya Umoja wa Afrika.
Ripoti hiyo inatarajiwa kutoa mwongozo kwa nchi za Afrika katika kusimamia deni na kuhakikisha ufadhili unachangia kwa vitendo katika mabadiliko ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya bara hilo.
Miongozi mwa ujumbe kutoka Wizara ya Fedha ulioambatana na Mhe. Balozi Omar katika mkutano huo ni Naibu Katibu Mkuu, Bi. Asha Khamisi Abdulah na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Rished Bade.






