NHIF: Hizi ndiyo taarifa sahihi kuhusu dawa katika Kitita cha Huduma

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema kuwa, taarifa zinazosambaa mitandaoni kuhusu
kuondolewa kwa baadhi ya huduma za dawa katika Kitita cha Huduma zinazotolewa na mfuko kwa wanachama wake hazina ukweli wowote.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga akitoa ufafanuzi mbele ya waandishi wa habari (hawapo pichani) jijini Dodoma leo kuhusu taarifa ambazo hazina ukweli zinazosambazwa mitandaoni.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Bernard Konga wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Taarifa hizo zimeanza kusambaa kwa kasi tangu jana tarehe 4 Septemba 2020 na kuzua hofu kubwa miongoni mwa wanachama na wadau wetu, lakini pia kuharibu na kupunguza imani ya mfuko ambayo imejengeka kwa wanachama na wananchi kwa ujumla katika utoaji wa huduma za matibabu.

"Kutokana na kusambaa kwa taarifa hizi. Mfuko umeona usikae kimya na badala yake utoke na kutoa taarifa kwa umma kwa kuzungumza na vyombo vya habari ili kuondoa sintofahamu ambayo imekuwepo kwa wadau wetu na ufafanuzi wa mfuko juu ya huduma zake ni kama ifuatavyo;

"Mfuko ulifanya maboresho makubwa sana katika huduma zake ikiwemo eneo la dawa ambapo mwaka 2016, jumla ya dawa 522 zilijumuishwa katika kitita cha mafao. Mwaka huu tena, jumla ya dawa 21 zimeongezwa ambazo zikinyambulishwa zinaleta ongezeko la jumla ya dawa 71.

"Hivyo orodha yetu kwa sasa ina dawa iliyonyumbulishwa ambazo ni jumla ya dawa 975, hizi zinalipiwa na mfuko ikilinganishwa na 694 iliyokuwepo mwaka 2015, NHIF Mfuko umeingia mikataba ya huduma na watoa huduma ambayo inaelekeza namna ya kuwahudumia wanachama wa mfuko, hivyo ni vyema makubaliano hayo yakazingatiwa kwa maslahi makubwa ya wanachama ambao wamelipa fedha zao kabla ya kuugua na endapo kuna changamoto yoyote juu ya utaratibu wa huduma ni vyema kuwasiliana na mfuko na sio kutoa taarifa zinazoleta mkanganyiko ndani ya jamii,"amefafanua Mkurugenzi Mkuu huyo.

Ameongeza kuwa, mikataba hiyo ni ya miaka mitatu na utekelezaji wake hufanyika kwa kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo ile ya uwasilishaji wa madai.

"Watoa huduma wanashauriwa kuzingatia haya na endapo kuna changamoto yoyote, basi mfuko kupitia ofisi zake za mikoa itashirikiana na mtoa huduma ili kutatua changamoto husika na mwanachama asipate madhara yoyote.

"Mfuko umekuwa na utaratibu wake wa mawasiliano na wanachama, watoa huduma na wadau wake yanapotokea mabadiliko au maboresho ya aina yoyote, hivyo wanachama wanatakiwa kupata taarifa kupitia njia sahihi zinazotumiwa na mfuko ikiwemo tovuti yake, kurasa za mfuko za mitandao ya kijamii na Kituo cha Huduma kwa Wateja.

"Mfuko unawaomba wanachama wake mara wanapokutana na changamoto yoyote wakati wa kupata huduma vituoni wawasiliane na mfuko ili kupata msaada wa haraka na kuchukua hatua endapo mwanachama amenyimwa haki yake anayopaswa kuipata,"amefafanua.
NHIF inakushauri popote unapoona taarifa hii ikisambazwa kwa makusudi ya kupotosha umma ifute na uipuuze maana haina ukweli wowote. Zinazoendana soma hapa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news