Mwanadiaspora Agnetta Kamugisha afunguka mengi kuhusu Rais Magufuli

Ni wazi kuwa, kuna Watanzania wengi wanaishi nchi mbalimbali duniani. Watanzania hawa wana kaliba mbalimbali za kiuchumi na weledi. Kwa kutambua thamani na umuhimu wa Wanadiaspora hao na ili Serikali iweze kunufaika na Watanzania hao wanaoishi Ughaibuni imeanzisha Kitengo Maalum katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ili kuratibu waweze kushirikiana na Serikali katika kukuza uchumi, anaripoti Mwandishi Diramakini.

Maeneo ambayo Serikali inaweka mkazo ni kuwahimiza watanzania wenye uwezo, mmoja mmoja au kwa kikundi waweze kuwekeza nyumbani. Kufuatia jitihada hizo watanzania wengi wamewekeza katika ununuzi wa nyumba zinazojengwa na mashirika ya hifadhi ya jamii kama NSSF.

Aidha, benki nyingi kama CRDB, zimeanzisha huduma maalum kwa ajili ya Diaspora zinazowawezesha kusafirisha fedha zao kwa gharama nafuu. Eneo lingine ni la utaalam, kwani Diaspora wengi wamesoma na kuwa na utaalam wa aina mbalimbali ambao unahitajika kwa maendeleo ya Tanzania.

Serikali pamoja na sekta binafsi imekuwa ikiwatumia wenye utaalam huo katika maeneo ambayo ni vigumu kupata wataalam hao hapa nyumbani. Mfano ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Dkt.James Mataragio.

Pia kutangaza vivutio vya Tanzania. Diaspora wamekuwa watu muhimu mno katika harakati za kutangaza vivutio vya utalii katika maeneo yao wanayoishi. Serikali imekuwa inasaidia kuwapa taarifa kupitia vipeperushi na wao wamekuwa wakisambaza kwa jamaa zao na marafiki.

Mbali na hayo,Diaspora wamekuwa wakijitolea sana kusaidia watanzania wenzao kwa kutoa vifaa mbalimbali hospitalini na kwa walemavu ikiwemo wakati wa majanga. Misaada imekuwa ikitolewa kwa mmoja mmoja au kuhamasishana kwa makundi kupitia jumuiya zao.

Mwanadiaspora Agnetta Kamugisha ambaye kwa sasa ni Systems Analyst katika Taasisi ya Elimu ya Mkoa wa North Carolina, Marekani ni Mtanzania mzaliwa wa Ishozi mkoani Kagera. Alifika Marekani mwaka 1979 huku elimu ya Sekondari akisomea Illinois na Chuo Kikuu amesoma North Carolina State University nchini Marekani. Mama huyu amesomea Bachelor of Computer Engineering.

Pia ni mmoja wa waasisi wa Kampeni ya Dhibiti Mlipuko wa Corona (COVID-19 Tanzania Campaign). Kampeni hiyo ilikusanya mamilioni ya fedha na kununua vifaa vya kinga. Kamugisha ndiye alitoa wazo hilo kwa Watanzania wengine huko Ughaibuni na likaleta matokeo chanya.

Agnetta Kamugisha pia ni Mkurugenzi wa Nshomile Village Foundation. Hii ni taasisi isiyokuwa ya kiserikali nchini Marekani inayosaidia Kyelima Shule ya Msingi, Ishozi, Kagera. Kwa sasa wanajenga madarasa mawili.

Kabla ya kustaafu miaka miwili ijayo ili kurejea nchini Tanzania, anasema kuwa, licha ya kujisomesha mwenyewe, yeye na Watanzania waliofanikiwa kusomeshwa na Serikali wanapaswa kutambua kuwa wana deni kubwa kwa ajili ya kuliendeleza Taifa lao, kwani wengi wao wanaoishi Ughaibuni wamesahau sana kutenda mambo muhimu kwa ajili ya Taifa.

Mwanadiaspora Agnetta Kamugisha. (DIRAMAKINI).
Mwandishi Diramakini amefanikiwa kufanya mahojiano ya ana kwa ana na Agnetta Kamugisha na kuyaweka wazi mambo mbalimbali yahusuyo Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Magufuli. Endelea...

Mwandishi Diramakini: Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli inahitaji sana ushirikiano baina ya Watanzania waliopo nchini na Diaspora hii ikijumuisha pia wawekezaji kutoka nje, unadhani nini kifanyike ili kuyawezesha haya kutendeka kikamilifu;

(a) Kuyafikia matokeo makubwa katika sekta ya utalii 

Agnetta Kamugisha:Tukiwa na uraia pacha itatupa bidii kubwa ya kuitangaza nchi yetu na vivutio vyake vingi. Diaspora wanakuja nyumbani kutembelea familia zao. Pamoja na kuleta rafiki zao. Kwa hiyo Serikali iwawekee vivutio ili waweze kutalii ndani ya nchi kwa wingi.Mheshimiwa Rais anafanya kazi nzuri ikiwo kurahisisha usafiri wa ndani na nje ya nchi.

  

Ni muhimu sana abiria kufanya 'connections' bila usumbufu, vivyo hivyo tumeona namna ambavyo anaimarisha sekta ya usafirishaji wa anga kupitia ujenzi wa viwanja vya ndege na ununuzi wa ndege kubwa hii ni hatua kubwa na muhimu.

(b) Uwekezaji katika viwanda vikubwa ikiwemo madawa ya binadamu na mawasiliano

Agnetta Kamugisha:Kuwezesha diaspora kushirikiana na Watanzania, tungeliomba Bunge Tukufu kufikiria kutoa urai pacha au Hadhi Maalumu kwa Wanadiaspora. Itawapa urahisi wa kuwekeza nyumbani bila kuwa na wasiwasi. Itapunguza utata wa watu kuchukuwa mali za Wanadiaspora kwa sababu hawana haki za kumiliki kama wazawa. Ni vigumu kuwashawishi wawekezaji wasio kuwa wazawa kama Mwanadiaspora sio raia.

(c)Sekta ya elimu yeye ushindani na inayotoa wasomi bora kwa ajili ya kuliendeleza Taifa katika nyanja mbalimbali.Unaweza kutumia uzoefu wako wa huko Marekani.

Agnetta Kamugisha:Sekta ya elimu kwa muda mrefu sana ilisimama kuboresha hususani mikoani. Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli alifanya uamuzi mzuri kutoa elimu bure. Hii ilisadia watoto waliokuwa hawaendi shule kwa kukosa uwezo. Elimu ni sekta ambayo Diaspora inaweza kuchangia zaidi.

Ingawa Diaspora wengi wanafanya mengi Tanzania, lakini tunaweza kusaidia sana shule tulizosoma. Wengi hatujarudisha chochote tangu tumalize. Mimi binafsi niliaza kusaida shule ya msingi kijijini kwetu baada ya Rais Magufuli kuchaguliwa na kuonyasha moyo wa kuchapa kazi.

Kwa hili nawawapa changamoto Diaspora wasisahau shule walizosoma. Hizi shule ziliwekeza kwetu, tuwajibike kwa kurudisha fidia kwa wananchi na sio kuilaumu Serikali. Kwa kweli mimi nilipata msingi mzuri sana wa elimu ya msingi Tanzania ambayo imeniwezesha kufika nilipo kimaisha. Kwa hiyo ni wajibu wangu kuisaidia shule. Mimi binafsi naelewa kwamba elimu bure iliongeza idadi ya wanafunzi. Kwa hili nasaidia ujenzi wa madarasa.

Mwandishi Diramakini:Nini hasa Watanzania wanapaswa kukitambua kutoka kwa Rais Dkt.Magufuli ambacho wageni huko nje wanakisema mara kwa mara na wanatamani wangekuwa na kiongozi wa mfano wake?

Agnetta Kamugisha:
Amerudisha nidhamu, uadilifu, uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii. Amepunguza rushwa. Hii imesaidia sana kuepusha Wanadiaspora na wananchi kuzungushwa. Tanzania ilikuwa inasifika kwa utulivu wake, lakini hii Awamu ya Tano imeleta sifa kubwa sana kwa Tanzania hususani miundombinu kama barabara, hospitali, ndege, meli, treni, umeme, elimu bure na mengine mengi.

Rais Magufuli anajulikana sana kwa kuchapa kazi, huipenda nchi na wananchi wake. Mimi na familia yangu tunazifaidi ndege. Hatuna haja ya kupitia Entebbe na kutumia hela yetu Uganda, ambayo sasa hivi tunaitumia Tanzania. Kikubwa zaidi, wengi huku wanatamani kukutana na Mheshimiwa Rais Magufuli ili waweze kupata maarifa ya uzalendo uliotukuka kutoka kwake kwa ajili ya kuendelea kupigania maslahi ya Taifa letu tuwapo nje na ndani ya nchi.

Mwandishi Diramakini:Watanzania wanawezaje kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliani (TEHAMA) kuzikabili changamoto za kila siku hususani kuboresha uchumi wao na kupunguza gharama za kuendesha shughuli zao?

Agnetta Kamugisha:Kitu kikubwa sana amefanya Mheshimiwa Rais JPM ni kusambaza umeme mikoani mpaka huko vijijini. Kuwa na umeme na barabara ni vitu muhimu sana kwa kuleta maendeleo ya nchi na wananchi. Wanafunzi wa shule za vijijini na wilayani wataweza kufanya shughuli za maabara ambayo inaongeza ujuzi kwenye masomo. Pia umeme utawezesha watu wengi kutumia komyuta pamoja na simu na kujifunza vitu vingi kwenye mitandao kwa ajili ya kuwapa maarifa mapya ambayo wanaweza kuyatumia kuboresha maisha.

Mwandishi Diramakini:Yapi ambayo kila ukikaa na kutafakari unaona Dkt.Magufuli ndiye kiongozi mwenye maono chanya kwa kuwa ni mtekelezaji zaidi kuliko kusema?

Agnetta Kamugisha: Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli amepiga vita rushwa, ametoa elimu bure, kaondoa wafanyakazi hewa na safari za nje zisizokuwa za msingi. Anatatua shida za wananchi akifanya safari za ndani.

Mwanadiaspora Agnetta Kamugisha. (DIRAMAKINI).

Pia msimamo wake wakati wa virusi vya Corona (COVID-19) alielewa kwamba wananchi wataathirika zaidi kwa kuwafungia ndani muda mrefu. Miji kama Dar es Salaam watu wangekufa kwa njaa. Amepunguza ujambazi. 

Kutokana na ubora wa barabara ajali zimempunguwa. Pia mwendo kasi umepunguza kero za usafiri.Usafiri wa Dar es Salaam ulikuwa mugumu sana na kusabisha watalii wasizunguke mji na kununua bidhaa mbalimbali. Mfano Mtalii anayeunganisha Dar es Salaam na ndege ya usiku kurudi kwao anaishia uwanja wa ndege badala ya kwenda mjini.

Mambo mengine yanayotupa nguvu na imani kubwa kwake ni namna alivyoweza kufanya makubaliano mapya na mikataba ya Wachina na makampuni ya uchimbaji, vitendo ambavyo vimeleta manufaa makubwa kwa Watanzania.

Mwandishi Diramakini: Ni kwa namna gani uongozi wake umewezesha kuimarisha mahusiano na Diaspora?

Agnetta Kamugisha: Ingawa hajatutembelea, anatuma wawakilishi kwenye makongamano yetu. Rais Magufuli kwa kiwango kikubwa sana na cha pekee, ameweza kuwagusa Wanadiaspora kwa kusimamia miundombinu. Mambo makubwa aliyoyafanya ya ujenzi wa barabara, madaraja, reli, meli, ndege, umeme, na mengine mengi.


Mwandishi Diramakini:Ni yapi mategemeo yako kwa Taifa?

Kwa kweli nimefurahishwa sana na juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano, amefanya mambo mengi Tanzania kwa muda mfupi na kuibadilisha nchi.

Agnetta Kamugisha: Amejenga misingi ya kufanya mengine mengi miaka mingine mitano ijayo. Tanzania itaendelea kukuwa kiuchumi na kuvutia wawekezaji na watalii. Kila mmoja wetu anapaswa kutambua kuwa, kubadlisha Rais itaangamiza uchumi wa nchi.Huwezi kuwa huru bila kuwa na uchumi,nawatakia Uchaguzi mwema Watanzania wote.Mungu ambariki sana Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli na Mungu ibariki Tanzania na wananchi wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

1 Comments

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here