Rais Magufuli amtumbua Kigogo wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Matumizi ya Ardhi, Dkt. Steven Justice Nindi, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Joseph Magufuli. (Picha na Maktaba).

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi John Kijazi imeeleza kuwa, Mhe. Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kuanzia leo tarehe 17 Januari, 2021.Nafasi hiyo itajazwa baadaye.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Januari, 2021 amewasili Mjini Bukoba mkoani Kagera ambapo kesho ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha VETA Mkoa wa Kagera na kuzindua shule ya sekondari Ihungo ambayo imejengwa upya baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi lilitokea Septemba 2016. 

Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli amewasili Mjini Bukoba akitokea Chato Mkoani Geita.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wananchi wa Muleba wakati akiwa njiani kuelekea Bukoba mkoani Kagera leo tarehe 17 Januari 2021. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Wananchi wa Kemondo wakati akieleka Bukoba mjini mkoani Kagera leo tarehe 17 Januari 2021.
 
Akiwa safarini, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Muleba na Kemondo ambapo amewashukuru kwa kumpigia kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu zilizomwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili. 

Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wananchi hao kuwa Serikali itahakikisha ahadi zilizowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM (2020-2025) zinatekelezwa ili kuinua ustawi wa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa. 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Mheshimiwa Rais Dkt.Magufuli amezitaka taasisi na mamlaka zote zinazohusika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, miundombinu ya elimu, afya na maji kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kwamba yeye atafuatilia kwa ukaribu. 

Amewahakikishia wananchi wa Muleba kuwa barabara ya Kanyambogo – Nshamba (kilometa 5) itajengwa kwa kiwango cha lami, na ameagiza barabara ya Muleba – Rubya (kilometa 19) ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami iitwe Barabara ya Mujungi (Mjungi Road) ikiwa ni kutambua mchango mkubwa Marehemu Mhandisi Leopord Mjungi ambaye wakati wa uhai wake alisanifu na kusimamia ujenzi wa barabara nyingi hapa nchini.

Post a Comment

0 Comments