Rais Dkt. Mwinyi: Tumuombe Mwenyenzi Mungu atupe mrithi mwenye dhamira njema kama Maalim Seif

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaomba Waumini wa Dini ya Kiislamu kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili apatikane kiongozi mwingine wa nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mwenye nia njema na dhamira njema kama Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad, anaripoti Mwandishi Diramakini.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dk. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza na Waumini wa Kiislam wa Masjid Raudha Daraja Bovu Wilaya ya Magharibi “A” Unguja, baada ya kumalizika kwa Sala ya Ijumaa, iliofanyika katika Masjid hiyo leo 26-2-2021, na kupokea shukrani zao.(Picha na Ikulu).

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti Raudhwa uliopo Darajabovu madukani, Jimbo la Shauri Moyo, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamu zake kwa Waumini wa Msikiti huo ambao ujenzi wake umekamilika baada ya kutekeleza ombo lao.

Alisema kwamba Zanzibar ilipofika ni pazuri sana na Wazanzibari ni wamoja kwani zamani waumini walikuwa wakichagua miskiti ya kusali lakini leo wote wanasali pamoja na kumuomba MwenyeziMungu kuongeza hali hiyo kwani hiyo ndio dini na misikiti ni nyumba za MwenyeziMungu.

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kuna kila sababu ya kuendeleza hali ya umoja, amani na mshikakano kwani MwenyeziMungu ameshawaweka Wazanzibari kwenye mstari na ni vyema hali hiyo ikaendelezwa kwa manufaa ya wananchi wote.

Katika salamu zake hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Wazanzibari wote wanahuzunika kwa kuondokewa na kiongozi wao mahiri Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad hivyo ni vyema wakamuombea dua popote pale walipo.

Alieleza kwamba Maalim Seif Sharif Hamad alishiriki kikamilifu katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo imeleta maridhiano na kupelekea Zanzibar kuwa ya amani, yenye umoja na mshikamano.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa maridhiano yamepelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano ambapo hapo mwanzo vitu hivyo havikuwepo na wananchi walikuwa tayari wameshapotea lakini Mwenyezi Mungu ameleta rehema zake hizo.

Akitoa shukurani kwa mfadhili aliyemalizia ujenzi wa msikiti huo ambao waumini wake walimuomba Rais siku alipokwenda kusali katika msikiti huo mnamo Januari 08, 2021 na kuwakubalia ombi lao na ndipo alipojitokeza mfadhili huyo na kumwambia kwamba amuachie yeye aifanye kazi hiyo.

Rais Dk. Mwinyi akieleza kiini cha ujenzi huo, alimtaja Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ndiye aliyempa ujumbe kwamba Waumini wa Msikiti huo wanataka kusali pamoja nae ili wamueleze matatizo yao na ndipo akatekeleza ombi hilo na waumini hao kumuomba kumalizia msitiki huo.

“Nimetoka kusuli hapa nikapigiwa simu na Muumini mwenzetu kwamba umepewa ombi la kujenga msikiti naomba uniachie mie....na kama alivyosema Imamu Jumatatu watu wakawa washafika hapa tayari kuanza ujenzi...mie mwenyewe sijapata kuona spidi ya ujenzi huu”,alisema Alhaj Dk. Mwinyi.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa pongezi na shukurani kwa mdhamini wa ujenzi wa msikiti huo pamoja na msimamizi wake Sheikh Feisal Kindy.

“Siku tuliyokuja kusali na kupewa ombi la ujenzi wa msikiti huu tuliambiwa kwamba ukijenga msikiti MwenyeziMungu anakujengea kasri Peponi, nikasema na mimi naitaka hiyo kasri kwa hivyo, nakushukuruni kwa kunipa ombi hili lakini leo nimesimama kwa kumuomba Mwenyezi Mungu hilo kasiri lisiwe langu peke yangu bali liwe kwa mfadhili wetu, na mimi, na waliotusimalia ujenzi na nyinyi mlioomba lakini na Maalim Seif Sharif Hamad”, alisema Rais Dk. Mwinyi.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi amepokea ombi la kuwa mlezi wa Msikiti huo pamoja na kuwa mlezi wa Kamati yote inayosimamia msikiti huo.

Alhaj Dk. Mwinyi alilipokea ombi la Waumini wa Msikiti huo la kutaka kumaliziwa jengo la msikiti wao ambapo aliahidi kuwasaidia ili msikiti huo uweze kusalika vyema na Waumini wote wa eneo hilo waweze kupata nafasi nzuri ya kuweza kufanya ibada.

Mapema Sheikh Ali Fakih Abdallah akitoa hotuba ya sala ya Ijumaa alieleza kwamba kutoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kuna manufaa makubwa mbele yake.

Sheikh Ali Faki Abdallah alisisitiza haja ya kukatazana mabaya na kuelekezana mazuri huku akieleza kwamba sifa za wenye akili ni wale wenye kutekeleza ahadi ambazo wamekwua wakiziahidi na hawaendi kinyume na ahadi hizo walizoziahidi.

Akitoa shukurani kwa Waumini wa msikiti huo walimpongeza na kumshukuru Alhaj Dk. Mwinyi kwa kutekeleza ahadi zake za kuhakikisha ujenzi wa msikiti wao huo unakamilika kwani zaidi ya miaka kumi jengo hilo la msikiti lilishindikana ujenzi wake.

Sheikh Ali Faki alisema kuwa Alhaj Dk. Mwinyi amefanya kitendo hicho kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na hakufanya kama Rais, ama ana uwezo mkubwa na kumueleza kwamba kila mmoja katika eneo hilo la Darajabovu anamuombea dua Alhaj Dk. Mwinyi kutokana na wema aliowafanyia.

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi alifika nyumbani kwa kizuka wa Marehemu Seif Sharif Hamad huko Mbweni na kuonana nae pamoja na familia yake na ya Marehemu huku akitumia fursa hiyo kumuomba kizuka pamoja na wanafamilia kuwa na subira na Mwenyezi mungu atawafanyia wepesi.

Akiwa huko nyumbani kwa Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad ambapo Mama Mariam Mwinyi na Alhaj Dk. Mwinyi, Rais Dk. Mwinyi alimuahidi kizuka huyo kwamba ataendelea kushirikiana nae wakati wote yeye pamoja na Serikali anayoiongoza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news