WAKANDARASI WAZEMBE KUPOKONYWA MIRADI YA MAJI

Serikali itawapokonya na haitowapa tena kazi ya kujenga miradi ya maji Wakandarasi wanaoshindwa kuikamilisha kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa, anaripoti Mohamed Saif (Mwanza).

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi akisisitiza jambo wakati wa ziara yake kwenye miradi ya maji Wilayani Sengerema.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa tamko hilo Februari 25, 2021 wakati wa ziara yake kwenye mradi wa maji wa wa vijiji vya Buyagu, Kalangalala na Bitoto Wilayani Sengerema mkoani Mwanza.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi, Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Sengerema, Mhandisi Cassian Wittike alisema ulikuwa ukitekelezwa na Mkandarasi mzawa Kampuni ya D4N Construction Limited ya Wilayani Kahama ambaye alishindwa kuukamilisha kwa mujibu wa mkataba wake.

"Mradi huu ni miongoni mwa miradi tuliyorithi kutoka kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 2019 na haukua umekamilika kutokana na uwezo mdogo wa mkandarasi," alimueleza Naibu Waziri.

Mhandisi Wittike alisema kwamba mradi ulianza kutekelezwa tangu Desemba 2013 na ulipaswa kukamilika Juni, 2014 kwa gharama ya shilingi bilioni 1.7 lakini mkandarasi alishindwa na hivyo RUWASA ilimpokonya na ukakamilishwa kwa mfumo wa force account.

"Mkandarasi aliyepewa jukumu alishindwa kuukamilisha na hivyo tuliuchukua na kuanza kutekelezwa na wataalam wa RUWASA Sengerema kuanzia mwaka 2019 na sasa hivi tupo kwenye majaribio na umeanza kutoa maji," alisema Mhandisi Wittike.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi akishuhudia majaribio ya kutoa maji kutoka kwenye mradi wa Buyagu- Kalangalala-Bitoto.

Kufuatia maelezo hayo na hali halisi ya mradi aliyoishuhudia, Naibu Waziri Mahundi alisema amesikitishwa na mkandarasi huyo mzawa kwa kupewa mradi na kushindwa kukamilisha kwa zaidi ya miaka sita na hivyo alitoa wito kwa wakandarasi wazawa kote nchini kuacha ubabaishaji kwani waliaminiwa na waone umuhimu wa katunza imani hiyo kwa Serikali yao.

“Wakandarasi wazawa tunapenda kufanya kazi nanyi na tunatarajia kuona mnafanya kazi kwa uaminifu na weledi naamini hili linawezekana, mambo ya ubabaishaji yalikwishapitwa na wakati na tena si kwa Serikali hii ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli,” alisisitiza Mhadisi Mahundi

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi alipofanya ziara kwenye tenki la maji la mradi wa Buyagu, Kalangalala na Bitoto Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza. 

Alibainisha kwamba Serikali haitoongeza muda na haitomvumilia mkandarasi mzembe na badala yake atapokonywa na atawekwa kwenye orodha ya wakandarasi ambao hawana sifa ya kukabidhiwa kutekeleza miradi ya maji kote nchini.

Alituma salam kwa mkandarasi huyo D4N Construction kwamba ajihesabu kuwa miongoni mwa wakandarasi walio kwenye orodha ya kutopewa tena shughuli yoyote kwenye sekta ya maji.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi (katikati) akimsikiliza Meneja wa Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Sengerema, Mhandisi Cassian Wittike (kulia).

"Mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi inavyopasa atanyang'anywa mara moja na hatopewa tena kazi nyingine, hapo ajue amejifuta na ameingia rasmi kwenye orodha ya wakandarasi wasiokuwa na sifa wala uwezo wa kujenga miradi ya maji," alisisitiza Mhandisi Mahundi.

Aliongeza kwamba hali ya uzembe wa baadhi ya wakandarasi hususan wazawa inamsikitisha Rais. Dkt. John Pombe Magufuli hasa ikizingatiwa kwamba dhamira yake ya kuwainua wazawa haileti tija kusudiwa.

"Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli anafarijika kuona wakandarasi wazawa wanapata kazi ya kujenga miradi lakini bahati mbaya baadhi yao kwa kukosa uzalendo wanamuangusha kwa kushindwa kutekeleza vyema miradi wanayokabidhiwa," alisema Naibu Waziri Mahundi.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi alipotembelea tenki la maji la mradi wa Buyagu, Kalangalala na Bitoto Wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.

Naibu Waziri Mahundi vilevile alisisitiza kwamba Serikali inawaonya na haitowavumilia wakandarasi wenye tabia ya kutumia fedha wanazolipwa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji na badala yake wanaipeleka kwenye masuala mengine yasiyohusiana na kusudio hilo.

"Wakandarasi mnapaswa kutambua fedha mnayolipwa ni kwa ajili ya kujenga miradi na sio kufanyia matumizi mengine sasa bahati mbaya hua fedha hii mnaipeleka kwenye matumizi tofauti na hii inasababisha mshindwe kutekeleza miradi kwa ubora uliyokusudiwa na kwa wakati sahihi," alisisitiza Naibu Waziri Mahundi.

Aidha, Naibu Waziri Mahundi alisisitiza kuzingatia suala la thamani ya fedha kwenye ujenzi wa miradi ambapo aliwataka wataalam wote wanaohusika na usimamizi wa ujenzi wa miradi kuhakikisha wanalipa umuhimu.

“Mliopewa jukumu la kusimamia miradi nyinyi ni wataalam na sio kila kitu kinacholetwa na mkandarasi mnakubaliana nacho, vingine havina tija zaidi ya kuongeza gharama ya mradi ambayo pengine tungeweza kuipunguza na fedha hiyo ikatumika kutekeleza mradi mwingine japo mdogo,” alielekeza Mhandisi Mahundi.

Naibu Waziri Mahundi amehitimisha ziara yake ya siku mbili Mkoani Mwanza kwa kutembelea miradi ya maji ya Buyagu-Kalangalala-Bitoto, Mwaliga-Nyamahona, Magulukenda na Nyampande ya Wilayani Sengerema.

Post a Comment

0 Comments