Wanafunzi 27 ni miongoni mwa mateka walioachiwa huru Nigeria

Mwakilishi wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) nchini Nigeria, Peter Hawkins amesema amefarijika kupokea habari iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu ya kuachiliwa kwa wanafunzi 27 wa Chuo cha Sayansi cha Serikali huko Kagara, anaripoti Mwandishi Diramakini (Mashirika).

Ni wanafunzi ambao walitekwa nyara kutoka shule yao zaidi ya wiki moja iliyopita na kwamba anatarajia kurudi kwao salama katika familia zao.

"Wakati wanafunzi walioachiliwa huru wanaporudi kwa familia zao, naungana na familia ya mwenzao Benjamin Habila, aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa shambulio la usiku shuleni. Fikra zangu na sala ziko pamoja na familia ya Benjamin, ambao wamepata hasara kubwa,”amesema.

Aidha, kiongozi huyo wa UNICEF nchini Nigeria alisema tukio la kushambulia shule huko Kagara, kama vile lile lililotokea katika shule ya sekondari ya wasichana ya serikali Jangebe kwenye jimbo la Zamfara Ijumaa na mengine kama hayo yaliyotokea kabla, hayakutakiwa kutokea na kwamba watoto hawapaswi kulengwa katika mashambulizi, hususani katika maeneo ambayo wanategemea kuwa salama, shuleni.

“Mashambulio kwenye vituo vya elimu ni ukiukaji mkubwa wa haki za watoto. Watoto hawapaswi kamwe kuwa walengwa wa shambulio na bado, mara nyingi sana nchini Nigeria wamekuwa waathirika wa mashambulio kwenye shule zao,” amesisitiza Hawkins.

Taarifa yake hiyo imefafanua kuwa mashambulio kama hayo si tu yanapuuza haki za watoto kupata elimu, pia hufanya watoto kuogopa kwenda shule, wazazi wanaogopa kupeleka watoto shuleni.

Hawkins ametoa wito akisema, "tunapokaribisha habari za kuachiliwa kwa wanafunzi wa Kagara waliotekwa nyara, naomba serikali kuharakisha hatua juu ya kuachiliwa na kurudishwa salama kwa wanafunzi waliotekwa nyara wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Serikali Jangebe, na watoto wote wa shule waliotekwa nyara ambao bado hawajaachiliwa,"ameongeza.

Awali Msemaji wa gavana wa jimbo la Niger, Mary Noel-Berje alilieleza shirika la habari la Ujerumani, dpa kwamba walioachiwa huru walitekwa nyara kutoka kwenye shule iliyo karibu na mji wa Kagara katika eneo hilo.

Wakati huo huo wasichana 317 waliotekwa nyara kutoka kwenye shule moja ya sekondaru katika mji wa Jangebe, katika jimbo la Zamfara siku ya Ijumaa asubuhi pia bado hawajulikani walipo.

Utekaji nyara unaofanywa na makundi ya kujihami umeongezeka nchini Nigeria katika miezi ya hivi karibuni. Wasichana na wanawake hulazimishwa kuolewa na wapiganaji au kuwa washambuliaji wa kujitoa muhanga huku wengine wakitumika kama vibarua.Aina nyingine ya utekaji nyara inafanywa na magenge ya wahalifu kwa nia ya kudai kulipwa fidia.---UNnes/dpa.

Post a Comment

0 Comments