Mabaharia, wafanyakazi wa ndege waombewa kipaumbele chanjo dhidi ya Corona

Mashirika matano ya Umoja wa Mataifa yametoa wito wito kwa Mabaharia na wahudumu wa ndege kuchukuliwa kama ni watoa huduma walio mstari wa mbele na hivyo kupewa kipaumbele katika chanjo dhidi ya virusi vya Corona (COVID-19).

Miongoni mwa mashiirika hayo ni pamoja na Shirika la Usafiri wa Anga (ICAO), Shirika la Umoja wa Mataifa afya Duniani (WHO), Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM), Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Majini (IMO) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi Duniani (ILO) ambayo yametoa taarifa ya pamoja yakitoa wito huo.

Kwa mujibu wa mashirika hayo,Corona imesababisha athari mbaya kwa maisha ya binadamu na uchumi wa Dunia na usafiri wa baharini na angani ambazo ni nyanja muhimu ambazo zinategemewa na biashara ya kimataifa na uhamaji na ni kitovu cha ukwamuaji endelevu wa kijamii na kiuchumi.

Mashirika hayo yameeleza kuwa, zaidi ya asillimia 80 ya biashara ya ulimwengu kwa kiasi huhamishwa na usafirishaji wa baharini ambapo uchumi wa Dunia unategemea mabaharia milioni mbili kote Duniani ambao wanaendesha meli za kibiashara duniani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mabaharia wameathiriwa sana na vizuizi vya kusafiri vilivyowekwa wakati wa janga la COVID-19 na tangu Januari 2021, inakadiriwa kuwa mabaharia wengine 400,000 wamekwama kwenye meli za kibiashara, kwa muda mrefu wakati mikataba yao imeshamalizika na hawawezi kusafirishwa huku idadi kama hiyo ya mabaharia wanahitaji haraka kujiunga na meli.

Aidha, kwa mujibu wa UNnews, kwa upande wa safari za anga, taarifa ya pamoja ya mashirika hayo ya kimataifa imesema usafiri wa anga wa abiria ulibeba abiria wapatao bilioni 5.7 mwaka 2019 wakati ambapo usafirishaji wa ndege unawakilisha asilimia 35 ya thamani ya bidhaa zilizosafirishwa kwa njia zote pamoja.

Idadi ya wataalam wote wa usafiri wa anga walio na leseni, wakiwemo marubani, wadhibiti trafiki wa anga na mafundi wataalamu wenye leseni ya utunzaji, walikuwa 887,000 mwaka 2019, kulingana na takwimu za wafanyikazi wa ICAO.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa,utekelezaji wa sheria kali za afya ya umma kwa wafanyakazi wa anga, pamoja na amri ya kusalia majumbani kujikinga na janga la COVID-19, vimesababisha athari kubwa katika utendaji na pia gharama kubwa.

"Usafiri wa baharini na anga hutegemea mabaharia na wafanyakazi wa ndege, ni wafanyakazi muhimu wanaohitajika kusafiri kuvuka mipaka kila wakati, hali ambayo inaweza kusababisha kuhitaji kuwasilisha uthibitisho wa chanjo ya COVID-19 kama sharti la kuingia nchi zingine.

"Hii ni licha ya pendekezo la WHO kwamba, kwa wakati huu, nchi hazipaswi kuanzisha mahitaji ya uthibitisho wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa kusafiri kimataifa kama hali ya kuingia, kwani bado kuna mambo muhimu ambayo hayajulikani kuhusu ufanisi wa chanjo katika kupunguza maambukizi na upatikanaji mdogo wa chanjo hiyo. Tunarudia wito wetu kwa nchi ambazo hazijafanya hivyo kuhakikisha inawachukulia mabaharia na wahudumu wa usafiri wa ndege kuwa ni wafanyakazi muhimu na wanastahili kupewa kipaumbele katika kupata chanjo dhidi ya COVID-19,”ilifafanua taarifa hiyo.

Picha na NICHOLAS HUYNH/U.S. NAVY

Post a Comment

0 Comments