Awali akizungumza wakati akiipokea msaada huo wa vifaa tiba ambavyo vinatumika kupima kiasi cha Oxijeni katika mwili wa mwanadamu, Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia afya, Mhe Dkt. Festo Dugange amewapongeza Watanzania hao waishio Marekani kwa kuthamini juhudi za Serikali ya Nchi yao za kujenga na kukarabati miundombinu mbalimbali ya afya nchini. Alisema ili kuhakikisha kuwa jukumu hilo linatekelezwa kikamilifu, Naibu Waziri ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka 2021/22 serikali imetenga shilingi bilioni 65 kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba.
“Serikali imefanya kazi kubwa ya ujenzi wa Miundombinu na katika mwaka wa fedha 2021/22 tumeweka kwenye bajeti ya dawa na vifaa tiba kama hivi na vingine kiasi kinachofikia Bil.65, hivyo kwa jitihada hizi za wadau hawa na wengine wote watakao kuja hapo baadaye ni ishara kwamba lengo letu la kuweka vitendanishi na dawa litatimia,” amesema Mhe Naibu Waziri Dkt. Dugange.
Akiongea kwa niaba ya Watanzania waishio nchini Marekani, rais wa DICOTA, Dkt. Frank Minja, amesema, wanaona fahari ya kuchangia vifaa hivyo ambavyo vitakwenda kugawiwa kwenye ngazi ya Hospitali za Wilaya na kutumika na watanzania wenzao na kuahidi ni mwanzo ambapo wanatarajia kufanya mengi zaidi kwa kushirikiana na Serikali na Mbunge Lugangira katika Sekta hii ya Afya.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya Dkt. Grace Magembe, amesema kuwa atahakikisha kuwa vifaa vilivyopokelewa vinatunzwa ili viweze kudumu kwa muda mrefu.
Hafla ya kukabidhi vifaa tiba ilifanyika Makao Makuu ya Ofisi ya Rais TAMISEMI jijini Dodoma na kuhudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Huduma za Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe na Katibu Mtendaji wa Tume ya Utumishi wa Walimu Paulina Mkwama.
