Waziri Ummy ameagiza kuchukua hatua wakuu wa vitengo vya ukaguzi wa ndani wa halmashauri 54 ambao hawakukagua taarifa za hesabu za mwisho kabla ya kuziwasilisha kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Ameendelea kufafanua kuwa hoja nyingi zilizotajwa na CAG zinatokana na baadhi ya watumishi wa halmashauri kutowajibika ipasavyo au kujihusisha na vitendo vya ubadhirifu.
Waziri Ummy amesema kuna waweka hazina waliohusika na uandaaji wa taarifa za hesabu za mwisho ambao hawakutekeleza kukamilifu wajibu wao wa kutunza kumbukumbu za fedha na kuandaa taarifa sahihi kinyume na memoranda ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2009 Agizo la 27(3).
Kutokana na changamoto hizo amezitaka Halmashauri ziliopata hati mbaya na zeye shaka ziwabainishe wataalam wa fedha wenye CPA (T) ambao walisaini taarifa za hesabu za mwisho kuthibitisha kwamba taarifa hizo ni sahihi na hazina makosa.
Hata hivyo amewataka wataalam hao wafikishwe kwenye bodi ya wahasibu na wakaguzi (NBAA) ili wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa taaluma zao.
Pia, amewataka wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanavijengea uwezo wa kuvitumia ipasavyo vitengo vya ukaguzi wa ndani kwa kuwapatia mafunzo ya mifumo ya kielektroniki, kuwatengea bajeti za kutosha na kutekeleza kwa wakati mapendekezo yote wanayotoa ili wakati wa ukaguzi kusiwe na dosari.
Kuhusu upotevu wa mapato, Waziri Ummy amezitaka ofisi za wakuu wa mikoa na halmashauri kuhakikisha zinaimarisha usimamizi wa mapato ya ndani ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mapato yote yaliyopo mkononi yanapelekwa benki.
Hatua hiyo imetokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyotolewa hivi karibuni kwa umma ikionesha Halmashauri nane zilipata hati chafu huku 53 zikipata hati zenye mashaka.
Akizungumza leo na waandishi wa habari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ummy Mwalimu, amezitaja Halmashauri nane zilizopata hati mbaya kuwa ni Halmashauri za Wilaya za Itigi, Singida, Shinyanga, Momba, Igunga, Sikonge, Urambo na Manispaa ya Tabora.
Kuhusu Halmashauri 53 zilizopata hati zenye shaka, amesema mikoa yenye Halmashauri nyingi ni Mkoa wa Dodoma (Halmashauri 7), Kigoma (Halmashauri 6), Mwanza, Ruvuma na Tanga (zina Halmashauri 4 kila moja), Mikoa ya Iringa, Mara, Geita, Shinyanga na Dar es Salaam (Halmashauri 3 kila moja).
Mikoa mingine 10 ina Halmashauri 1 mpaka 2,huku Halmashauri za Wilaya za Buhigwe, Songea na Butiama zimepata hati hiyo kwa miaka miwili mfululizo.
“Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Nidhamu zihakikishe kuwa hatua stahiki zinachukuliwa kwa Wakuu wa Vitengo vya Ukaguzi wa Ndani wa Halmashauri 54 ambao hawakukagua taarifa za hesabu za mwisho kabla ya kuziwasilisha kwa CAG,”amesema Waziri Ummy.
Pia, amesema Wakuu wa Mikoa wahakikishe Wanashiriki Mikutano Maalum ya Mabaraza ya Madiwani katika Halmashauri kujadili taarifa za CAG na kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yote ya CAG pamoja na kuratibu kufanyika kwa uhakiki wa majibu ya hoja zote za ukaguzi na Ofisi yake ipate taarifa za utekelezaji na Mpangokazi kabla ya Mei 31, mwaka huu.
“Halmashauri zilizopata hati mbaya na hati zenye shaka ziwabainishe, Wataalam wa Fedha wenye CPA (T) ambao walisaini taarifa za hesabu za mwisho kuthibitisha kwamba taarifa hizo ni sahihi na hazina makosa wafikishwe Bodi ya Wahasibu na Wakaguzi (NBAA) ili wachukuliwe,” amesema.
Waziri Ummy amebainisha maelekezo mengine kuwa ni Wakurugenzi kuhakikisha wanavijengea uwezo na kuvitumia ipasavyo vitengo vya ukaguzi wa Ndani.
Kuhusu kutorejeshwa kwa mikopo inayotolewa kwa Vikundi vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Waziri huyo aliagiza Halmashauri kusimamia utekelezaji wa kanuni za utoaji na usimamizi wa mikopo za mwaka 2019 na kuchukua hatua stahiki kwa kikundi kitakachoshindwa kurejesha mkopo.
