Wachimbaji waandamana wilayani Bariadi wakimkataa Mwekezaji

Mgogoro wa mara kwa mara kati ya wachimbaji wadogo na watu wanaopewa leseni za uchimbaji na tume ya madini katika mgodi wa Bulambaka ulioko katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu umeingia katika sura mpya, anaripoti Derrick Milton (Simiyu).
Wachimbaji wadogo wadogo wakiwemo wamiliki wa mashamba wa Mgodi wa Bulumbaka ulioko katika Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, wakiwa na mabango walipoandamana kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bariadi na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo. (Picha na Derick Milton).

Mgogoro huo umewalazimu wachimbaji wadogo kuandamana katika Ofisi ya Mkuu wa wilaya na mkuu wa Mkoa, huku wakiwa wamebeba mabango yenye jumbe za kumkataa mwekezaji aliyepewa leseni ya uchimbaji kwenye mgodi huo.

Wakiongea na waandishi wa habari, wachimbaji hao wakiwemo wamiliki wa mashamba, wamesema wameamua kufanya maandamano ili kupaza sauti zao kwa viongozi wakuu wa taifa.

Wamesema kuwa hatua zilizotumika kupatikana kwa mwekezaji huyo, zimegubikwa na usiri mkubwa, huku wakitaja uwepo wa viashiria vya rushwa katika upatakanaji wake.

“Kwanza hii leseni imetolewa haraka haraka katikati ya kipindi cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais John Pombe Magufuli, tulijiuliza kwa nini itoke sasa hivi? Na kwa haraka kiasi hicho? Tulipouliza wakasema huu ni utawala mpya siyo ule wa zamani wa Rais Magufuli, huo umepita," amesema Nyakelenge Gidioni.

Hata hivyo wachimbaji hao wamesema kuwa, wamiliki wa mashamba katika mgodi huo kwa muda wa mwaka mzima, wamekuwa wakiangaikia wapate leseni yao kutoka tume ya madini licha ya kukamilisha taratibu zote za uombaji.

“Tuliambiwa tuunde kikundi ili na sisi tupatiwe leseni ya uchimbaji, leo hii takribani mwaka mzima tumeangaika kupata hiyo leseni lakini tumeshindwa, ila huyu bwana aliyepewa yeye ameomba hivi karibuni na amepata haraka haraka wakati sisi tumeangaika mwaka mzima,” amesema Masuka Sahani mchimbaji.

Mmoja wa wachimbaji hao Masunzu Mboje amesema kuwa mwekezaji huo baada ya kufika kwenye mgodi huo, aliwataka wamiliki washamba kusaini hati ya makubaliano kwa nguvu huku wengine akiwapatia pesa (rushwa) ili waweze kusaini.

“Alipokuja alituita wenye mashamba akawa anatoa milioni 10 kwa kila mmoja, mimi nilikataa nikasema siwezi kusaini na kupokea rushwa hiyo mpaka nijue hatma yangu kwenye leseni hii, baadhi yetu walipokea,” amesema Mboje.

Aidha, wachimbaji hao wamesema mwekezaji huyo aliyepewa leseni, amekuwa na vitendo vya unyanyasaji, pamoja na wizi wa madini ambapo walieleza amewahi kukamatwa akitorosha mawe yenye madini.

"Gari lake lilikamatwa likitorosha madini kwenye mgodi namba moja, leo hii ndiye kapewa mgodi mzima kwa ajili ya kuchimba, amekuja lakini wenye mashamba hatujui hatma yetu, kama wachimbaji hatumtaki,”amesema Amos Mchambi.

Mkuu wa Wilaya Festo Kiswaga akiongea na wachimbaji hao, alisema kuwa Ofisi yake haitambui leseni hiyo na wala hawezi kuongea jambo lolote juu ya mgogoro huo kwa sababu alitoa maelekezo na yameshindwa kutekelezeka na ofisi ya madini mkoa.

“Mimi najua kila kitu kinachoendelea uko, na hiyo leseni imetoka kinyemela na ofisi yangu haitambui, ila siwezi kusema lolote, niwatake nendeni kwa mkuu wa mkoa, maana ofisi yangu imeshindwa kwani nimetoa maagizo ila wamegoma kutekeleza,” amesema Kiswaga.

Naye mwekezaji huyo Hussen Makubi akiongea na waandishi wa habari juu ya tuhuma hizo, amesema kuwa yeye na wenzake wanaounda kikundi cha Buruwadu 4 Mine ndiyo wamepewa leseni ya kuchimba kwenye mgodi huo.

“Siyo kweli kuwa mimi ndiye nimepewa leseni, ila ni kikundi ambacho wapo hao wenye mashamba, mimi ni mwenyekiti wa kikundi, tupo watu 39 na hizo tuhuma siyo kweli, tulifuata taratibu zote zinazotakiwa,” amesema Makubi.

Makubi amesema kuwa leseni hiyo amepewa kihalali na hakuna vitendo vya rushwa kama wachimbaji hao walivyodai, huku akiiomba serikali kuingilia kati kwani shughuli za uchimbaji zimesimama kwa sasa.

Hata hivyo, alipotafutwa Ofisa Madini hakuweza kupatakana kwa haraka, kwani alikuwa kwenye kikao cha kamati ya ulinzi na usalama mkoa kilichokuwa kikiendelea katika ofisi ya mkuu wa mkoa kujadili suala hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news